22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SERENGETI BOYS MSITUANGUSHE

LILIKUWA ni tukio la kihistoria pale kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, kilipopata nafasi ya kuliwakilisha Taifa katika michuano ya Afcon kwa vijana wenye umri huo nchini Gabon.

Kikosi hicho kilichofanya maandalizi ya kutosha hapa nyumbani ili  kuhakikisha kinafanya vema katika michuano hiyo, kitaanza safari yake ya kusaka ubingwa leo kwa kuivaa Mali kwenye Mji wa Libreville, Gabon.

MTANZANIA tunaamini vijana wamejiandaa vema tayari kwa mchezo huo, wakiwa chini ya kocha mwenye kiwango kizuri hapa nyumbani, Bakari Shime.

Safari ya Serengeti Boys kuelekea kwenye michuano hiyo ilikuwa ndefu na yenye changamoto nyingi, hakika vijana watakuwa wamejifunza mambo mbalimbali kupitia mechi za kirafiki walizofanikiwa kucheza.

Tunakumbuka kikosi hicho kiliweza kushuka dimbani mara saba kucheza michezo ya kirafiki ili kujijengea uzoefu.

MTANZANIA tulishuhudia kikosi hiki  kikifanikiwa kupata matokeo mazuri katika mechi hizo, ambazo ni dhidi ya Burundi, Ghana, Cameroon na Gabon.

Licha ya kujikuta kikipoteza mchezo wa marudiano dhidi ya Cameroon, hiyo haikuwa sababu ya kikosi  hicho kushindwa kuendelea na maandalizi yake kabambe, kuhakikisha kinaitoa Tanzania kimasomaso katika fainali hizo.

Tunaamini kwamba kipimo cha Serengeti Boys kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu zilizokata tiketi ya kushiriki fainali hizo, kinatosha kuifikisha mbali timu hiyo ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Kitendo cha vijana wa Serengeti kuwabana wenyeji wa fainali hizo Gabon kwa kutoa kipigo mara mbili mfululizo walipokutana nchini Morocco, ikiwamo kuifunga Cameroon katika mchezo wao wa awali, ni dhahiri kwamba wachezaji wameiva kwa mashindano.    

Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Serikali, ulifanya uamuzi sahihi kukipeleka kikosi hicho nchini Morocco kuweka kambi ya mwezi mmoja, kabla ya kuelekea nchini Gabon.

Tunazipongeza juhudi za Serikali kwa kuwa karibu na timu hiyo katika vipindi mbalimbali, tangu pale alipoteuliwa Waziri Nape katika wiraza hiyo na hata kipindi hiki ambacho gurudumu hilo lipo mikononi mwa Waziri  Harrison Mwakyembe.

Katika hali nyingine iliyoongeza ari kwa wachezaji na Watanzania kwa ujumla, ni mwaliko waliopewa vijana hao kwenda kupata nasaha kutoka kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu, hiyo imeweza kuonyesha jinsi gani kikosi hicho kina nafasi kubwa kwa Taifa letu.

Tukiwa wafuatiliaji wazuri wa hatua zote ambazo kikosi hiki kimeweza kupiga hadi kufika nchini Gabon, tumeridhishwa na maandalizi na tunaamini yatazaa matunda mazuri.

MTANZANIA tunaiombea dua na kuendelea kuhamasishana Watanzania kukiombea kikosi hicho  ili kiweze kutimiza malengo ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Ni vizuri vijana hawa wakafahamu kwamba, hakuna chochote wanachotakiwa kuwalipa Watanzania pamoja na Serikali yao zaidi ya ushindi.

Tunapenda kuwashauri wachezaji hawa kuendelea kujiandaa kisaikolojia katika mechi zote watakazocheza, huku wakiamini kuwa Tanzania inaweza kufika mbali hata kama wapinzani wetu ni miongoni mwa mataifa yaliyotutangulia katika maendeleo ya michezo.

Tunawaamini Serengeti boys, uongozi kwa maana ya Wizara na TFF, pia kamati maalumu ya uhamasishaji, tunaamini maandalizi yaliyofanywa yataleta tija katika mbio za Tanzania kuondoka katika kundi la kuwa wasindikizaji.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles