NA MWANDISHI WETU,
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetakiwa kuacha kuhoji uhalali wa kikao cha Wakati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya kikao Ikulu kwa madai kufanya hivyo ni kutumia rasilimali za umma kwa maslahi ya Chama.
Kutokana na hali hiyo viongozi wa chama hicho wametakiwa kutambua kwamba Rais Dk. John Magufuli ndiye Mwenyekiti wa taifa wa CCM na kwamba hata anapoamua kukutana na vizingozi wa upinzani hutumia kumbi za Ikulu.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar as Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka ilisema hoja hiyo iliyotolewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa CUF, Mbarara Maharagande, kushutumu hatua hiyo haina mwingine.
Shaka alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Maharagande kushutumu kikao cha CC cha juzi kufanyika Ikulu na kudai kutumia vibaya rasilimali za umma.
“UVCCM tunamwambia mwanasiasa huyo, amekwenda kombo, hajui kulinganisha wala kutofautisha mambo. Alichokisema ni porojo akifananisha na taarifa kwa umma ambayo ilikosa mantiki, haikuwa na kichwa wala miguu. Kwa kifupi hakueleweka na hakufahamika alichokusudia kukisema mbele ya Kaimu,” alisema.
Shaka alisema viongozi mbalimbali wa upinzani wamekuwa wakialikwa Ikulu na kutumia rasilimali hizo ikiwemo kuandaliwa chakula na vinywaji.
Pamoja na hilo alimtaka Maharagande kutumia muda na rasilimali za CUF kutatua mgogoro uliokigubika chama chao na kuwafanya viongozi wao kutokana katika meza moja.
“UVCCM tulitegemea angewaambia wananchi yuko CUF ipi, ile ya Mwenyekiti Professa Ibrahim Lipumba au ni mfuasi wa Katibu Mkuu Seif Sharif Hamad, angetujuza watamaliza lini mivutano yao, hatima ya kesi yao kama imekwisha au la na kutueleza kama viongozi wake wameafikiana, wamekubaliana au wanaelekea kukizika chama hicho kwenye kaburi ya sahau,” alisema.