24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

UTPC, IMS wakutanisha waandishi vijana kujadili uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa

Na Clara Matimo, Mwanza

Jumla ya wanachama 10 kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC) pamoja na wanafunzi 15 vijana wanaosomea fani ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT) kilichopo jijini Mwanza wamekutana kwenye mdahalo uliolenga kujadili kuhusu uhuru wa kujieleza na haki ya kupata  taarifa.

Afisa Programu kutoka UTPC, Victor Maleko, akizungumza jambo kwenye mdahalo huo.

Mdahalo huo uliofanyika Novemba 21, 2022 jijini Mwanza uliandaliwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC) Kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kusaidia Vyomba vya Habari(IMS) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Switzerland(SDC).

Akizungumza wakati akifungua mdahalo huo, Mgeni rasmi ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya UTPC, Paulina David, aliwataka waandishi wa habari kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kuepuka kuipa jamii ambayo inawaamini taarifa za upotoshaji na kujiweka salama kwa kutovunja sheria zinazohusu tasnia ya habari.

“Tasnia ya habari nchini inakabiliwa na changamoto nyingi zinazoathiri moja kwa moja dhima ya uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa hasa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali, sheria kadhaa  zinazoelezea uhuru wa habari na wa kujieleza  ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi na upatikanaji wa taarifa.

“Sheria hizo zinafanya vyomba vya habari kwa sasa kupitia waandishi wa habari kushindwa kuandika kwa kina habari za kiuchunguzi (IJ)na habari nyingine hivyo imani yangu baada ya mdahalo huu mtakuwa mabalozi wazuri kwa waandishi wengine kuhusu uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa pasipo kuvunja sheria zinazohusu uhuru wa habari,”alisema Paulina.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT), Martin Nyoni,akiwasilisha mada kuhusu vijana wanavyoweza kuchochea uhuru wa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko, akiwasilisha mada inayohusu uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha upatikanaji wa uhuru wa habari, aliwashauri waandishi wa habari waendelee kufanya kazi kwa kufuata weledi wa taaluma yao kwani tasnia ya habari inawategemea.

“Nyie ni vijana kwa hiyo katika tasnia nyie ndiyo wahariri na viongozi wa kesho fanyeni kazi zenu kwa kufuata misingi ya taaluma ya habari someni sheria zinazohusu tasnia ya habari ili mjue jinsi ya kujilinda mnapotimiza majukumu yenu maana kutokujua sheria haikulindi utakapovunja sheria,”alisema Soko na kuongeza.

“Binafsi naishukuru serikali ya awamu ya sita  inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha nia ya kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria za sekta ya habari ambazo zinaonekana si rafiki sana katika tasnia ya habari ikiwemo sheria ya huduma za vyomba vya habari ya mwaka 2016,”alisema Soko.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT), Martin Nyoni, alisema vijana wanaweza kuchochea uhuru wa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii kwa kuongeza uelewa juu ya matumizi ya mitandao hiyo pamoja na kuelewa sheria zinazoongoza mitandao ya kijamii kwani itasaidia kuepuka taarifa za upotoshaji.

“Vijana tumieni haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa iliyopo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 kwa kutengeneza maudhui yenye kuleta mabadiliko katika jamii kwani taifa linawategemea jambo la muhimu ni kutumia fursa hiyo pasipo kuvunja sheria,”alisema Nyoni.

Mjumbe wa Bodi ya UTPC, Paulina David, akitoa hutuba yake  ya ufunguzi wa mdahalo wa wanafunzi na waandishi wa habari vijana kuhusu uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa.

Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, Alex Gwido aliiomba UTPC kufanya mchakato wa kutafsiri sheria zinazohusu tasnia ya habari kwa lugha ya kiswahili ili waandishi wengi waweze kuzielewa kwa ufasaha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles