WAANDISHI WETU, DAR/MIKOANI
WAKATI pazia la urejeshaji fomu za kugombea nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani lililoanza Julai 14 mwaka huu likifungwa jana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa Mkoa wa Mara wamejitokeza wagombea ubunge 462 katika majimbo yote 10.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana wakati akitoa taarifa za uchukuaji na urejeshaji fomu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche alisema mwamko umekuwa mkubwa na wanachama wengi wamejitokeza kuchukua fomu.
Ngatiche alisema jimbo ambalo linaongoza kwa wanachama wengi kujitokeza kuomba nafasi ya kuchaguliwa na kuteuliwa kugombea kupitia CCM ni Bunda Mjini ambapo wamejitokeza wagombea 73.
Alisema kwa upande wa viti maalumu kupitia wanawake na vijana jumla ya wanachama 52 wamejitokeza kuomba nafasi ya ubunge.
Kwa upande wa Dar es Salaam, zaidi ya wanachama 220 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge na udiwani katika Ofisi za CCM Wilaya ya Temeka.
Akizungumzia zoezi hilo, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Temeka, Andrea Gwaje alisema wajumbe wote waliochukua fomu walifuata utaratibu uliowekwa na Kamati Kuu na hakukuwa na vurugu zozote.
“Zaidi ya wanachama 220 wamechukua fomu kwa nafasi za ubunge, udiwani na udiwani viti maalum na zoezi linakwenda vizuri”, alisema Gwaje.
Alisema kwa upande wa Jimbo la Temeka Julai 14 waliochukua fomu walikuwa 38 kati yao wanaume 36 na wanawake wawili na hakuna aliyerudisha fomu kwa siku hiyo.
Kwa upande wa Jimbo la Mbagala, waliochukua fomu walikuwa 41, wanaume 36, wanawake watano waliorudisha siku hiyo ni wanaume wawili.
Zoezi hilo liliendelea Julai 15 ambapo kwa Jimbo la Temeke walichukuwa 33 wanaume 24 na wanawake 9 na walirudisha ni wanaume 13 na mwanamke mmoja na kwa Jimbo la Mbagala walichukuwa 27 kati ya wanaume 24 na wanawake watatu na waliorudisha walikuwa wanaume 14 na wanawake watatu.
Aliongeza kuwa, Julai 16 katika Jimbo la Temeka waliochukua ni 12 wanaume 11 na mwanamke mmoja na waliorudisha 25 kati yao wanaume 21 na wanawake wanne.
Jimbo la Mbagala waliochukua fomu walikuwa 17 wanaume 15 na wanawake wawili waliorudisha fomu walikuwa 28 kati yao wanaume 26 na wanawake wawili.
Baadhi ya waliorudisha fomu jana kwa upande wa nafasi za ubunge ni Abubakar Sururu kwa Jimbo la Mbagala, Kakulu Kakulu Jimbo la Mbagala, George Gassaya Jimbo la Temeke na Sitta Kisinda nafasi ya Ubunge Jimbo la Mbagala.
Wengine waliorudisha fomu kwa nafasi za Ubunge ni Manesh Shahada kwa Jimbo la Mbagala, Mwandishi wa Habari Gloria Matola Jimbo la Temeka na Musa Mtulia kwa Jimbo la Temeke.
Katika Jimbo la Mpwapwa mkoani Dodoma waliochukua fomu za ubungeni 64 kwa Kibakwe wakiwa 19.
Kwa upande wa Dodoma Mjini, hadi zoezi hili linafungwa jana jioni, wagombea 58 walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Elirehema Nassari alisema mwamko umekuwa mkubwa ambapo mwaka 2015 waliojitokeza walikuwa wagombea 20.
Alisema kwa mwaka huu wagombea wanawake ni 6 ambapo alidai pia vikao vya kuanza mchujo vinatarajiwa kuanza Julai 21 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino, Everlina Jordan alisema kwamba mpaka majira ya saa 10 jioni jumla ya wagombea 35 wamejitokeza kugombea katika Jimbo hilo.
Alisema kati ya hao wanawake ni wanne huku vijana wengi wakiwa wamejitokeza.
Naye, Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino,Everlina Jordan alisema katika Jimbo la Mtera jumla ya wagombea 19 wamejitokeza kugombea huku mwanamke akiwa ni mmoja.
400 ARUSHA
Mkoani Arusha wagombea 432 wamechukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge majimbo na viti maalum kwa tiketi ya CCM, katika majimbo saba yaliyopo mkoa wa Arusha.
Katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Musa Matoroka, alisema awali waliochukua fomu walikuwa wagombea 434 ila wagombea wawili kutoka majimbo ya Monduli na Arusha Mjini hawakurejesha fomu.
Alisema kati ya 432 wagombea 318 ni wa majimbo huku 114 wakiwa wanatokea Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi,Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kupitia kundi la Mkoa, walemavu, wasomi na wafanyakazi.
Alisema Jimbo la Arusha Mjini walichukua fomu wagombea 92 ila mmoja hakurejesha, Arumeru Magharibi (61), Arumeru Mashariki (33), Karatu (53), Ngorongoro (14), Longido(12) na Monduli walichukua 25 ila wamerejesha fomu 24.
Kuhusu wabunge wa viti maalum na idadi zao kwenye mabano ni ,Jumuiya ya Vijana (30), Wazazi (9), U.W.T kupitia mkoa, walemavu, wasomi na wafanyakazi wakiwa (105),”alisema
“Nitoe wito kwa wagombea kuzingatia miiko ikiwemo kutokuchafua wenzao kwa upakana matope, kutokutoa rushwa.Mchakato wa kura za maoni utafanyika Julai 20 na 21 mwaka huu,kwa wale wa majimbo,”alisema.
CHADEMA ARUSHA
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kwa tiketi ya Chadema, Gibson Ole Meseyeki ameshindwa kwa kura tatu katika uchaguzi wa kura za maoni baada ya mgombea mwenzake, Ayoub Exaud kuibuka mshindi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe alisema Ole Meseiyeki alipata kura 93 huku mshindi akipata kura 93.
Kuhusu Jimbo la Arumeru Mashariki, Rebecca Mngodo ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoani Arusha, ameshinda kwa kura 118 huku Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha,Elisa Mungure akipata kura 109 kati ya kura zote 227 zilizopigwa.
Alisema uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho umefanyika katika majimbo manne ambayo ni Arumeru Magharibi, Longido Karatu na Arumeru Magharibi huku majimbo mitatu ambayo ni Ngorongoro, Arusha na Monduli yakifanya uchaguzi wao leo Jumamosi.
Alisema katika Jimbo la Karatu, aliyekuwa Mbunge Viti Maalum, Cecilia Pareso ameshinda kura za maoni huku Jimbo la Longido akishinda Michael Mokoro,ambaye ni mtaalam wa masuala ya utawala.
Alisema Arusha Mjini wanatarajia kupiga kura za maoni leo ambapo wagombea ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema,aliyekuwa Diwani wa Sombetini, Ally Bananga, Emma Kimambo pamoja na yeye(Katibu).
Jimbo la Tabora aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga ameshinda nafasi hiyo kwa kura 152 na kumshinda Martin Mussa aliyeambulia kura 43 kati ya 195 zilizopigwa.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Mwaifunga aliwataka wanachama wa Chadema kuacha siasa zisizo na staha kwa kuchafuana kwani inadaiwa siku moja kabla ya kura za maoni alitumiwa maofisa wa Takukuru akidaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi wa Chadema Kanda ya Magharibi, Paul Kayungilko aliwataka wanachama wote kuacha makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni.
Habari hii imeandaliwa na SHOMARI BINDA ,JANETH MUSHI-ARUSHA, MURUGWA THOMAS – TABORA, RAMADHAN HASSAN-DODOMA, SABINA WANDIBA NA CHRISTINA GAULUHANGA Dar es Salaam.