29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Mkuu wa mkoa mwingine acharaza wanafunzi viboko

Mwandishi wetu, Songwe

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, amewachapa viboko wanafunzi watano wanaodaiwa kuchoma moto Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 26.

Wakati Mwangele akitekeleza tukio hilo, Oktoba mwaka jana Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, aliwachapa  viboko wanafunzi wa kidato ha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kwa madai ya kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.

Kwa upande wake Mwangela jana aliwachapa wanafunzi hao ikiwa ni baada ya kamati aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto uliotokea shuleni hapo Julai tatu mwaka huu kusem wanafunzi wawili Naftari Nganga na Collin Kisinga ndio waliochoma mabweni ya shule hiyo, huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo  na hawakuripoti.

Alisema wanafunzi hao  walianza mpango wa kuchoma moto mabweni Juni 28 kwa kununua vifaa vya kuchomea, ilipofika Julai 2 walijaribu kuchoma bweni lakini halikuwaka, Julai 3 walichoma bweni likawaka na kusababisha hasara hiyo na Julai 6 walifanya jaribio lingine la kuchoma moto ghala la chakula lakini halikuwaka moto.

Mwangela alitoa miezi mitatu kwa wazazi wa Naftari na Collin kila mmoja kulipa Sh milioni 7.3, mmiliki wa shule pia alibainika kuwa na uzembe wa kuweka vifaa vya kuzimia moto hivyo kutakiwa pia kulipa Sh milioni 7.3 huku mwalimu wa zamu siku ya tukio, mlinzi na patroni nao wakitakiwa kulipa Sh milioni 4 ili kufidia hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto.

Aidha Mwangela aliwaagiza maofisa elimu Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika shule zote ili kubaini endapo elimu ya tahadhari ya majanga ya moto na vifaa muhimu kwa ajili ya kuzima moto vimewekwa katika maeneo ya shule.

Pia aliwataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha tabia za kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao kwani taifa linawategemea wawe wananchi bora na viongozi au watendaji wa baadae.

Mama mzazi wa mwanafunzi Collin aliyedaiwa kuchoma moto shule, Agnes Kisinga, alisema kitendo alichofanya mtoto wake si kizuri na amesikitishwa sana huku akitoa wito kwa walimu kushirikiana na wazazi katika malezi na kuwaasa wanafunzi kuzingatia masomo.

Naye Mwanafunzi Denis Petro wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema tukio hilo limewasababishia hasara kwa kuwa vifaa vya shule viliteketea kwa moto huku akiwaasa  wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha matendo mabaya kama ya kuharibu mali za shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles