Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli jana ametengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo anakuwa waziri wa tatu kufukuzwa baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.
“Ripoti hii haiwezi kupita hivi hivi, tutakuwa watu wa ajabu. ‘We have to do something’ wakati tunasubiri ripoti nyingine, mapendekezo yote ya kamati tumeyakubali.
“Ninampenda sana Profesa Muhongo, pia ni rafiki yangu, lakini kwenye hili ajitathmini na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo saa chache baadaye, taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilieleza kuwa Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Profesa Muhongo na nafasi yake itajazwa baadaye.
Pia aliivunja Bodi ya TMAA na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wake.
Rais Magufuli aliviagia vyombo vya dola viwachunguze watendaji wa wizara, akiwamo kamishna wa awali wa madini.
“Wafanyakazi wote wa TMAA wafuatiliwe na vyombo vya dola na hatua za kisheria zichukuliwe kuanzia leo (jana).
“Shughuli zote zinazohusu madini kuanzia leo (jana), vyombo vya ulinzi na usalama vianze kutumika hata kama ni kupeleka jeshi… kwa nini ukalinde kifaru halafu unasahahu vitu vinavyoleta kifaru,” alisema Rais Magufuli.
Alisema licha ya mwaka 2009 Sera ya Madini kuagiza kijengwe kiwanda cha kuyeyushia makinikia, lakini hadi sasa suala hilo halijatekelezwa.
“Smelter si tatizo na inaonekana palikuwa na makusudi yaliyofanywa na viongozi wa wizara husika, wameshindwa kusimamia TMAA, kuweka utaratibu wa kufuatilia makinikia.
“Walishindwa kitu gani, mbona wanasafiri kila mara kwenda Ulaya? Kamishna wa madini, waziri wanafanya nini?” alihoji Rais Magufuli.
AANDIKA BARUA KUJIUZULU
Wakati huohuo, muda mfupi baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, waziri huyo naye amemwandikia barua ya kujiuzulu.
Katika barua hiyo ambayo ilisambaa jana jioni katika mitandao ya kijamii, Profesa Muhongo alisema kwa muda aliokuwa katika nafasi hiyo, alijitahidi kufanya kazi kwa uwezo wake wote kuitumikia wizara hiyo.
“Napenda kukufahamisha kuwa nimejitahidi kufanya kazi kwa uwezo wangu wote kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini tangu uliponiteua kuwa waziri Desemba 12, mwaka 2015.
“Kutokana na ripoti iliyowasilishwa na kamati yako teule ya kuchunguza suala la makinikia na mapendekezo yaliyowasilishwa kwako kuhusu mikataba ya madini, utendaji wa Wakala wa Madini Nchini (TMAA) na wizara, nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya uwaziri kuanzia leo Mei 24, 2017.
“Mheshimiwa Rais, nashukuru sana kwa miongozo yako ya kazi ambayo daima imenisaidia sana kwenye utekelezaji wa majukumu yangu,” alisema Profesa Muhongo katika barua hiyo.