25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: TANZANIA HAITAKIWI KUWA OMBAOMBA

RIPOTI: Rais Dkt. John Magufuli akipitia ripoti ya Kamati ya kwanza ya Wataalam wa Jiolojia iliyoiundwa kwa ajili ya kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyopo kwenye mchanga wa madini (Makinikia) baada ya kukabidhiwa Ikulu, Dar es Salaam jana.PICHA: IKULU

 

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

WAKATI kamati maalumu ya kuchunguza kontena 277 za mchanga wa dhahabu ikionyesha ndani yake kuna madini yenye thamani ya Sh trilioni 1.441 huku mamlaka zikisema gharama ya madini hayo ni Sh bilioni 112.1, Rais John Magufuli, amesema kwa kontena 3,600 zinazosafirishwa kila mwaka, Tanzania ingetakiwa kuwa inatoa misaada badala ya kuwa ombaomba.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti na kamati hiyo jana, Rais Magufuli alisema: “Kwa haraka haraka madini ya dhahabu tu (yaliyo kwenye kontena 277) ni kama vile kuna malori mawili yenye uzito wa tani saba na Land Rover ama Pick-up moja. Wastani wa makontena yanayosafirishwa kwa mwezi ni kati ya 250 hadi 300 hivyo, kwa mwaka ni zaidi ya 3,600.

“Kwa miaka 10 zimesafirishwa kati ya tani 171 hadi 200 za dhahabu. Ni kitu cha kuumiza mno, ni cha aibu. Katika hili Watanzania wote tushikamane.

“Ukienda hospitali watu wanakosa dawa, vitanda, shuka, shule madarasa hayatoshi na madawati tunachangishana. Tunahangaika kukopa kujenga reli kumbe fedha zinamwagika tu hapa, inaumiza sana.”

Rais Magufuli alisema kutokana na rasilimali zilizopo, Tanzania haikupaswa kuwa ombaomba bali ilipaswa kusaidia nchi nyingine.

“Nchi yetu it was supposed to be a donor country (ingetakuwa kuwa inatoa misaada), lakini tunaonekana ni masikini. Sifahamu tunatakiwa kuombewa kwa imani zipi, wachungaji mliweke taifa hili kwenye maombi,” alisema Rais Magufuli.

ULINZI MAALUMU

Rais Magufuli alisema alilazimika kuitafutia ulinzi kamati hiyo ili kuhakikisha wanafanya kazi zao bila kuingiliwa na mtu yeyote.

“Pamoja na yote haya bado wapo waliojitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huo na majina tunayo. Kuna mtu mmoja anaitwa profesa wakati yeye ni daktari akaanza kuzungumza wakati hayo hayajui.

“Ni kwa sababu ya jeuri ya fedha walizopewa. Hatuna ushahidi, lakini ukiona mtu anazungumza vile, lazima ujue hazungumzi bure bali kuna kitu,” alisema.

Alisema fedha ambazo zimepotea zingeweza kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ya ujenzi wa miundombinu, afya na elimu.

SIRI YA KUMFUKUZA PROF. NTALIKWA

Rais Dk. Magufuli alisema alilazimika kumfukuza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa baada ya kusema kuwa katika makontena hayo madini ya dhahabu yaliyopo ni gramu 0.02.

Machi 26, mwaka huu, Rais Magufuli alimfukuza kazi Profesa Ntalikwa baada ya ziara ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyetembelea bandarini kukagua makontena yenye mchanga wa madini.

“Nilipoona anaulizwa na wabunge na kusema uzito wa madini ya dhahabu ni gramu 0.02 nilishindwa kuvumilia nikamfukuza saa hiyo hiyo. Huu ni unyama na aibu kwa mtu uliyesomeshwa na Watanzania halafu unajibu ‘stupid answer’. Nilifikiri nichague wasomi wazuri wa kuziendesha wizara, lakini wasomi wenzao ‘wame-prove wrong’,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles