25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Uteuzi wa ma-DC wapongezwa

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza safu mpya ya wakuu wa wilaya na mikoa, wasomi mbalimbali wametoa maoni yao juu ya uteuzi huo, huku wengine wao wakisifia uteuzi huo na wengine kukosoa.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, walisema  wanaounga mkono uteuzi huo kutokana na kila kiongozi anayeingia madarakani hupanga safu ya watu wake ili atimize ahadi zake kwa wananchi.

Juzi Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa watatu na  wilaya 101, ambapo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi wakati akitangaza mabadiliko hayo,  alisema Rais amezingatia suala la umri kwa kuhakikish hakuna mkuu DC  anayezidi miaka 60.

Katika safu hiyo, waliobaki katika nafasi zao ni 39, huku 78 wakiteuliwa wapya.

Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Joseph (SAUT), Profesa Mwesigwa Baregu, alisema suala la Rais kuwaacha wakuu wa wilaya wengi wa zamani ni kutaka kuweka watu ambao watatii uongozi wake bila kuhoji.

“Wakati wa uchaguzi palikuwa na watu ambao ilisemekana wanamuunga mkono aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwanvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Edward Lowassa, inawezekana amewaondoa ili aweze kubaki na watu ambao kwa namna ya uongozi wake wawe wanatii yale anayoagiza bila kuhoji,” alisema Profesa Baregu.

Alisema bado hajaona vigezo vilivyotumika kuwaondoa  wakuu wa wilaya wa zamani  na kuweka wapya ambao utendaji wao haujulikani katika nafasi hiyo.

“Kuwaondoa na kuwateuwa wengine bila kuangalia vigezo kama uzoefu na utendaji kazi wao ni changamoto ambayo inatufanya tuwe na hofu ya kutokujua kitakachotokea,” alisema.

Alisema suala la kuweka ukomo wa umri si sahihi, kwa sababu wapo wazee wenye uwezo na uzoefu mkubwa vinginevyo liwekwe wazi katika sera za Taifa kwamba watumishi wa Serikali hawatazidi miaka 60.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, alitoa maoni yake kupitia ukurasa wake wa Facebook  na kusema haoni tatizo kuhusu walioteuliwa, bali maoni yake ni katika nafasi yenyewe ya ukuu wa wilaya katika mfumo wa utawala.
“Ukuu wa wilaya ni nafasi yenye sura nyingi, lakini zote za kisiasa. Kwa uzoefu wa nyuma na utaratibu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni sehemu ya kuwapa nafasi ya kukua kisiasa na kikada vijana wa chama tawala kupitia jumuiya yao ya UVCCM.

“Ni nafasi za kuwahifadhi makada wastaafu. Ni sehemu ya kuwasaidia waliogombea ubunge kupitia chama tawala na kushindwa. Hutumika pia kutoa fadhila kwa watu ambao wamekisaidia chama  kushinda uchaguzi kwa namna mbalimbali.”

Alisema nafasi ya nafasi hiyo, haina tija kwa Taifa na kwamba ni mzigo mkubwa  kwa kiongozi  ambaye alitangaza kubana matumizi.

Alisema kwa kutambua hayo, vyama vya upinzani viliweka katika ilani zao kipengele cha kufuta nafasi hizo kama sera muhimu ya kubana matumizi na kuzipa mamlaka kamili halmashauri.

“Siku nikipata nafasi ya kumsogelea mheshimiwa Rais nitamnong’oneza jinsi ambavyo kufuta nafasi ya ukuu wa wilaya ingemrahisishia kazi ya kuwahudumia maskini kama alivyopania,” alisema Profesa Mkumbo.

 

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Frofesa Bertha Koda, alisema haoni tatizo katika uteuzi huo kwani kila mtawala anatafuta watu atakao fanya nao kazi vizuri.

Pia alipongeza suala la kuteuwa vijana na kusema kwamba vijana wana nguvu na ari mpya na kwamba wazee waliostaafu wanapaswa wapumzike wawaache vijana wafanye kazi.

“Mimi sioni tatizo, kila mtawala anatafuta watu atakaofanya nao kazi vizuri na kwa suala la kuweka ukomo wa umri si mbaya kwasababu miaka 60 ni umri wakustaafu, ni vyema wakapumzika na kuwapa vijana nafasi ya kufanya kazi wana nguvu na ari mpya,” alisema Profesa Koda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu na Mhadhiri wa UDSM, Profesa Penina Mlama, alisema Watanzania wanachotakiwa kufanya ni kusubiri kuona namna safu hiyo mpya itakavyofanya kazi.

“Huyu ni rais mpya, ni sawa kuja na safu yake tunatakiwa tusubiri kuona wanavyochapa kazi kwasababu anaonekana anapenda vijana suala ambalo naona ni zuri,” alisema Profesa Mlama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles