VATICAN CITY, Vatican
WAUMINI wa Kanisa Katoliki wasiotaka mabadiliko ambao mara nyingi wamekuwa wakimshutumu kiongozi wa kanisa hilo, Papa Francis kwa kutofuata mafundisho na asili ya ukatoliki na sasa wanashuku ameondoa utaratibu wa kuibusu pete yake.
Wanasema hayo wakionyesha video iliyochukuliwa juzi katika mji wa Loreto nchini Italia ambako Papa anaonekana akiukwepesha mkono wake kwa Wakristo Wakatoliki waliokuwa wakijaribu kuibusu pete yake.
Picha za televisheni rasmi za hapa zinaonyesha Papa Francis akiwa amesimama alipokuwa anaupokea msululu wa watu kwa dakika 13 na kuwapokea watawa takriban 113 wakiwamo wa kike na wakuu wa parokia, mmoja mmoja au wakiwa wawili.
Picha hizo zinaonyesha katika kipindi cha dakika 10 za kwanza, watu 14 wakimsalimia kwa mkono kiongozi huyo bila kuinama kuibusu pete yake.
Katika kipindi hicho, watu 41 waliinama kwenye mkono wa Papa Francis kwa kuonyesha ishara ya kubusu pete yake na wengine hata kuibusu.
Baada ya dakika 10 za mwanzo, mwenendo wa Papa ukabadilika, mstari wa salamu ulionekana kusonga kwa kasi.
Katika kipindi cha dakika 53 kipindi cha pili, Papa Francis alianza kutupa mkono wake mbali na watu 19 waliokuwa wakijaribu kumuinamia na kuibusu pete yake na mtu mmoja ambaye alikuwa na bahati mbaya alijikuta akibusu mkono wake baada ya Papa kuukwepesha ghafla mkono wake.
Hata hivyo pamoja na picha kuonyesha hali hiyo, wachambuzi wa masuala ya dini wanasema kuwa huenda ikawa kwamba Papa alikuwa na haraka ya kumaliza shughuli ya kuwasalimia waumini kwa sababu alitumia muda zaidi kuwasalimia watu wengi wakiwa kwenye viti vya walemavu, mbele ya kanisa .
Wachambuzi hao wanasema kuwa Pete ya Upapa, inayovaliwa kwenye kidole cha pete cha mkono wa kulia, huenda ikawa ni ishara kubwa zaidi ya mamlaka ya Papa kutokana na kwamba anapofariki dunia mara moja huwa inaharibiwa kuonyesha mwisho wa uongozi wake.
Inaelezwa pia kuibusu pete ya Papa mara kwa mara huwa ni jambo linalotia hofu kwa wengi kwa sababu kwa karne kadhaa ni jambo linalohusishwa na ishara ya dini au siasa.
Wanasema mwaka 1963, aliyekuwa Rais wa Marekani, John F Kennedy, aliyekuwa Mkatoliki, aliamua kwa makusudi kutoubusu mkono wa Papa Paul VI walipokutana Vatican kwa hofu ya kutowapa nafasi wakosoaji wake waliosema rais mkatoliki analazimika wakati wote kuutii uongozi wa Roma.