24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Utata wagubika uteuzi bosi wa Bandari

massaweNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI Serikali ikiendelea kuchukua hatua ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzani (TPA), suala la uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, limechukua sura mpya.

Hatua hiyo inakuja kutokana na kuwapo kwa usiri mkubwa unaohusu uteuzi wa mkurugenzi huyo mpya, atakayerithi mikoba ya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Awadh Massawe aliyeondolewa kazini.

Taarifa ambazo MTANZANIA imezipata kutoka chanzo kilichopo ndani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, zinaeleza kuwa Waziri mwenye dhamana na wizara za hiyo, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, alikuwa amtangaze mkurugenzi huyo  mwishoni mwa wiki.

Habari za uteuzi huo zilizagaa katika mitandao ya kijamii na kuzua gumzo miongoni mwa wafanyakazi wa TPA na wadau wengine juu ya nafasi hiyo.

Taarifa hizo zilidai kuwa Profesa Mbarawa, alikuwa amtangaze Ofisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (jina tunalihifadhi), kuchukua wadhifa huo.

“Wakati wowote kuanzia leo (Ijumaa iliyopita) waziri wetu atamtangaza mmoja wa wasaidizi wa CAG kuwa bosi mpya wa Bandari kwa hiyo subirini mtapata taarifa,” kilisema chanzo hicho kilicho karibu na Waziri Mbarawa.

Lakini hadi jana jioni wakati tunakwenda mitamboni, Waziri Mbarawa, alikuwa bado hajatoa tamko lolote, hali ambayo imeacha mjadala ukiendelea miongoni mwa wadau wa bandari.

Akizungumzia taarifa za uteuzi huo, mmoja wa watumishi wa siku nyingi TPA makao makuu, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, aliishauri Serikali kuliangalia suala hilo kwa umakini mkubwa kwa kuhakikisha anateuliwa mtu sahihi atakayeweza kuongoza TPA ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa.

“Utendaji kazi wa bandari ni tofauti na mashirika mengine, Mtendaji Mkuu wa Bandari anapaswa kuwa mtu ambaye amebobea katika masuala ya meli, ambapo kazi kubwa za meli ni kupakia na kupakua mizigo, ambalo ndilo jukumu mama la bandari.

“Kukusanya mapato pekee TPA hakutoshi, anatakiwa mtu ambaye anaijua TPA na kazi zake, sasa ni hatari kuongozwa na mtu ambaye kila kitu atalazimika kuuliza.

“Tutafurahi tukipata bosi ambaye hata Rais akimkurupusha usingizini na kumwuliza lolote lile kuhusu bandari atatoa maelezo bila kuomba muda wa kupata ushauri kutoka kwa wasaidizi wake.

“Mathalan huwezi leo hii kumchukua mchumi au mtaalamu wa hesabu na kumfanya Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, yote hii ni kwa sababu huduma zinazotolewa pale Muhimbili zinahitaji utaalamu maalumu.

“Hivyo nashauri viongozi wetu wenye mamlaka ya uteuzi wawe makini sana, wakifanya kosa katika uteuzi wa mtu wa kuongoza TPA, juhudi zote zilizofanywa na Serikali ya Rais Magufuli, zinaweza kupotea,” alisema.

Miongoni mwa matatizo ndani ya TPA yaliyoifanya Serikali kuchukua hatua kadhaa ni utoroshwaji wa makontena zaidi ya 2,000 suala ambalo lilibainika mwishoni mwa mwaka 2014 huku ikihusisha Bandari Kavu (ICDs) na vituo vya kuhifadhia magari yanayoingia nchini (CFS).

Utoroshaji huo unatajwa kusababishwa na uamuzi wa kuondoa majukumu ya kushughulikia mizigo kutoka menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam na kuyakabidhi kwa kamati ya watu watano wa makao makuu ya TPA, hatua ambayo ilitoa mwanya wa utoroshaji.

Uamuzi huo ulifanywa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Madeni Kipande, kupitia barua yake ya Februari 5, 2013, kumbukumbu namba DG/3/3/06, yenye kichwa cha habari “KUSIMAMIA TICTS, ICD’s na CFS.

Wateule wa Kipande watano waliochukua majukumu ya Bandari ya Dar es Salaam wakati huo ni Mkurugenzi wa Ulinzi, Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Teknohana, Mkurugenzi wa Utekelezaji na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MTANZANIA inazo Desemba 29, 2014, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam alimwandikia barua Meneja Ukaguzi wa Ndani wa bandari hiyo akimtaka kuzifanyia ukaguzi wa kina ICDs na CFS zote.

Katika barua hiyo ambayo nakala zilikwenda kwa Meneja Mapato, Meneja Masoko, Meneja Kitengo cha Makontena, Meneja wa Operesheni na Ofisa Mkuu wa Takwimu, ilisisitiza uharaka wa ukaguzi huo ambapo sehemu ilisomeka; “Please give this assignment high degree of urgency”.

Baada ya ukaguzi huo, ilibainika kuwa baadhi ya wafanyakazi wa TPA walihusika na utoroshwaji wa makontena, wafanyakazi ambao majina yao yalitajwa pamoja na taarifa nyingine muhimu.

Katika barua ya Februari 17, 2015 kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kwenda kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, wafanyakazi waliotajwa kuhusika walikuwa J. Azaar na S. Mtui (makontena 1,877), Joseph Kavishe (270), Lidya Kimaro na Happy-God Naftali (284), ambapo jumla ya makontena yote ni 2,431.

Baada ya kupewa ripoti hiyo ya ukaguzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Awadh Massawe, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya Mhandisi Kipande kung’olewa, alitoa maelekezo siku iliyofuata Februari 18, 2015 juu ya hatua za kuchukua.

Sehemu ya dokezo kuhusu hatua za kuchukua inasema; “Wahusika wote wasimamishwe kazi mara moja, aidha chukua hatua mara moja kwa wizi huu. Kesi za nidhamu zianze mara moja na nipate taarifa”.

Mbali ya kuchukua hatua hizo na nyinginezo, Agosti 10, 2015, alitengua uamuzi wa Kipande baada ya kubaini kuwapo usimamizi mbovu.

Katika barua yake ya Agosti 15, 2015 kwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam yenye kumbukumbu namba DG/4/3/02, pamoja na mambo mengine Massawe alisema; “Itakumbukwa kwamba katika waraka huo (wa Kipande) ilielekezwa kuwa jukumu la usimamizi wa shughuli za siku hadi siku za kiutekelezaji katika vituo hivyo utafanywa na kamati maalumu ya Makao Makuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles