25.9 C
Dar es Salaam
Sunday, December 4, 2022

Contact us: [email protected]

Albino apotea mwezi

Josephat TornerESTHER MNYIKA NA BETHSHEBA WAMBURA (RCT), DAR ES SALAAM

CHAMA cha Watu wenye Albino Tanzania (TAS) kwa kushirikiana na Shirika la Under The Same Sun (UTSS), kimeviomba vyombo vya dola kusaidia kumtafuta mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana, Mkoa wa Pwani, Said Ismail (47) ambaye amepotea katika mazingira ya kutatanisha kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu wa TAS, Josephat Torner, alisema Ismail ambaye ni mtu mwenye albino, alitoweka tangu Januari 31, mwaka huu.

Alisema Ismail aliwaaga wenzake anaoishi nao kuwa anakwenda kuuza mboga za majani  katika Kijiji cha Mtipule kilichopo kati ya Kijiji cha Nyakenge na Kitongoji cha Kaloieni, lakini hadi sasa hajaonekana.

“Siku hiyo Ismail aliondoka akiwa amebeba kikapu chake cha mboga, alionekana katika klabu ya pombe za kienyeji  kwa mama mmoja ambaye jina lake limepelekwa polisi na ofisi za Serikali ya kijiji.

“Akiwa eneo hilo, anadaiwa aligombana na wenzake aliokuwa anakunywa nao pombe, ilipofika saa moja usiku aliondoka, lakini cha ajabu hajaonekana hadi sasa,” alisema Torner.

Alisema kabla ya kupotea, Ismail aliwahi kukatwa mkono na watu wasiofahamika mkoani Morogoro.

Torner alisema kutokana na hali hiyo, alihamishiwa kwa shemeji yake, Wiziri Bakari kwa ajili ya usalama zaidi.

Alisema baada ya kupotea, walitoa taarifa kituo kidogo cha polisi Kimanzichana, Mkuranga na kupewa RB namba  KIM/RB/50/2016 na Kituo cha Polisi Wilaya ya Mkuranga na kupewa RB namba MKU/PE/05/2016.

Torner alisema TAS na UTSS kwa pamoja wanaendelea na juhudi za kumtafuta, na wanasikitishwa kukithiri kwa matukio ya aina hiyo.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hassan Kafani, alisema baada ya kutokea tukio hilo, waliunda tume ya kumtafuta Ismail, lakini hadi sasa hawajafanikiwa kumpata.

Aidha Torner alisema mbali ya tukio hilo, kuna jaribio la kutekwa nyara mtoto mdogo wa kiume mwenye albino, Tito Nkuryu (3) ambaye anaishi  katika Kijiji cha Itilima, Mkoa wa Simiyu.

Alisema mtoto huyo aliyenusurika kutekwa Februari 16, mwaka huu, alihamishiwa Kijiji cha Itilima na kuhifadhiwa kituo cha kulelea watoto cha Lamadi.

Torner alisema kutokana na matukio hayo, ameiomba Serikali itunge sera ya kitaifa ya watu wenye albino na hatimaye kutunga sheria maalumu ili masuala yao yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Aliitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti na utaratibu ulio wazi wa kupambanua kati ya matabibu na watu wanaotumia tiba asili  kutibu maradhi na waganga wa kienyeji wanaopiga ramli, kujihusisha na uchawi wa kutumia viungo vya binadamu.

“Kuna madai ya viungo vya albino kuwatajirisha watu na kuwapa mafanikio ya kisiasa, hawa waganga wa kienyeji watafutwe, wakamatwe na shughuli zao  zifungwe mara moja.

“Tunaomba vyombo vya sheria kuhakikisha vinawakamata wakatili hawa, watafutwe na kukamatwa kisha wafikishwe mbele ya sheria,” alisema Torner.

Kutokana na hali hiyo, alimuomba Rais Dk. John Magufuli kukomesha mauaji dhidi ya watu wenye albino.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,538FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles