32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Utata kung’olewa Meya Ubungo

 MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM 

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema chama hicho hakijamfukuza uanachama Diwani wa Ubungo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na wala hakijawahi kujadili suala lolote kuhusu yeye. 

Mnyika alitoa kauli hiyo jana, siku moja baada ya kusambaa barua iliyodaiwa kuandikwa na mtu aliyejitambulisha kama Katibu Kata ya Ubungo, Asheri Mlagwa ambaye hata hivyo amekanusha kuhusuia na barua hiyo. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema alishamwandikia barua Mkurugenzi wa Maniapaa ya Ubungo, kumtaka afute barua yake aliyoandika na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambayo inaonesha uongozi wa Chadema pia umepewa nakala japokuwa bado hawajakabidhiwa nakala hiyo. 

“Chama kinamtambua Jacob kama mwanachama, diwani na Meya wa Manispaa ya Ubungo. Pamoja na barua hii tumemtaka afute barua yake kwani utaratibu wa hatua za kinidhamu upo wazi kwa mujibu wa Katiba. 

“Mstahiki Meya pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na nimemweleza Mkurugenzi kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu Ibara ya Sita kifungu cha Saba inaeleza wazi hatua za kinidhamu kwa mwanachama mwenye nafasi. 

“Kiongozi wa kitaifa isipokuwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti , mamlaka yao ya nidhamu itakuwa ni Kamati Kuu ya chama Mstahiki Meya kwa kuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama na mmoja wa madiwani ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama. 

 “ Lakini kwa barua hii tumemweleza vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kwamba taratibu hata kama mstahiki Meya asingekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu kwa nafasi yake tu ya umeya, utaratibu wa kinidhamu unaongozwa na muongozo wa chama ambapo chama kina muongozo wa kusimamia wabunge, halmashauri wakiwamo madiwani na viongozi wa vijiji na mitaa na katika mwongozo huu sehemu E inahusu hatua za kinidhamu kwa wabunge na mameya. 

“Ambapo kwa hatua za kinidhamu za mameya ni tofauti na hatua za kinidhamu za madiwani wa kawaida, mameya hatua zao za kinidhamu zimeelezwa katika kipengele cha pili I: Kinasema kama kwa mfano maana hadi sasa hatujapokea malalamiko yoyote juu ya mstahiki Meya Jacob na hata kama kungekuwa na malalamiko juu ya utovu wa nidhamu au tatizo lolote inapaswa yafikishwe kwa Katibu Mkuu kwa maandishi ili yafikishwe kwenye kamati ya maadili ya taifa,” alisema Mnyika . 

Alisema kwa hiyo kwa mwongozo huo hata kama asingekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kwa nafasi yake tu ya umeya masuala yake hayawezi kushughulikiwa na ngazi ya kata wala wilaya au ngazi ya kanda, bali yanapaswa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu. 

“Mimi kama Katibu Mkuu wa chama sijapokea malalamiko yoyote kuhusiana na mstahiki meya wa manispaa ya Ubungo. Baada ya kupata hizi taarifa kwenye mitandao ya kijamii pia tulifanya ufuatiliaji ili kuona pamoja na kuwa je kuna kitu chochote kimetokea kwenye ngazi za chini za chama? 

“Na nimebaini kwamba kinachotajwa 

 kwenye barua ya mkurugenzi kuwa eti kuna kikao kimekaa cha kamati ya utendaji ni jambo ambalo si la kweli na hakuna kikao chochote cha kamati kilichokaa cha Kamati ya Utendaji ya Kata kuhusu kujadili hatua za kinidhamu za mstahiki meya na tumethibitisha kwamba ambaye anaelezwa kuwa amesaini barua, Asheri Mlagwa si Katibu wa Chadema wa Kata ya Ubunge ila Katibu wa Chadema wa Kata anaitwa Ezekiel Miraji,” alisema. 

KAULI YA JACOB 

Akizungumza muda mfupi baada ya kusambaa kwa barua hiyo ya kufukuzwa kwake uanachama ambayo hata hivyo ilidaiwa baadaye kuwa ni ya kughushi, diwani huyo wa Ubungo, Boniface Jacob alikanusha taarifa na barua hiyo akiwa na Asheri Mlagwa akieleza kuwa hakuhusika kwa kuwa tayari alishaondoka katika uongozi wa kata hiyo. 

Jacob alisema ameshtushwa na barua hiyo ambayo bado chanzo chake hakijajulikana na kwamba yeye bado ni mwana Chadema na hakuna kikao chochote cha chama kilichokaa hata kumjadili tu. 

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, Meya anafukuzwa na Kamati Kuu na Diwani anafukuzwa na uongozi wa Kanda lakini kwa kuthibitishwa na Kamati Kuu.

Alisema kwa mujibu wa Katiba hatua za kumfukuza Diwani au Mbunge hazihusiani moja kwa moja na uongozi wa kata, japokuwa unaweza kutoa mapendekezo ambayo yanapelekwa kwenye Kanda na kwenye Kamati Kuu. 

“Tunaendelea kuwasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ambaye alipokea barua hiyo ili atoe mwanga kuhusu wahusika waliopeleka barua hiyo ofisini kwake ili hatua za kisheria zichukuliwe, kwa kuwa wameghushi na pia wamefanya hivy kujaribu kunichafulia jina langu,” alisema. 

Kwa upande wake, Asheri Mlagwa ambaye jina lake lilitumika kuonyesha kuwa yeye ndiye Katibu wa Chadema Kata ya Ubungo, alikanusha kuhusu barua hiyo ya kumfukuza uanachama Jacob, akieleza kuwa hajawahi kuandikana kwamba hata sahihi iliyowekwa kwenye barua hiyo si ya kwake. 

Alisema anashangaa kuona jina lake likitumika katika barua hiyo kwa kuwa yeye 

 tayari alishaachia uongozi wa kata hiyo na katibu alishabadilishwa muda mrefu. 

Alisema taarifa hizo zipuuzwe kwa kuwa si za kweli na kwamba yeye hakuhusika kwa namna yoyote kwa kuwa si kiongozi wa chama kwa sasa na aliachia nafasi hiyo ili aweze kutekeleza maukumu yake mengine kikamilifu. 

BARUA YA MKURUGENZI 

Katika barua iliyoonesha kuandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Aprili 2, 2020 yenye kumbukumbu KUMB:NA. CAB./74/216/01/07 kwenda kwa Mstahiki Meya, Boniface Jacob, ilimweleza kuhusu kupokea nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kwake uanachama. 

“Kutokana na barua hiyo kunitaarifu kuwa “Umefukuzwa Uanachama” kuanzia 

tarehe 28/04/2020, nachukua nafasi hii kukutaarifu rasmi kuwa umekoma kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa mujibu wa kitungu cha 

39(2)(f) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa sura ya 292 toleo la Mwaka 2015 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 73(1)(e) na (f) ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo za Mwaka 2019. Sheria na kanuni hizo zinazofafanua kwamba “Mjumbe atapoteza sifa kuwa Mjumbe wa Halmashauri endapo atakoma kuwa mwanachama wa chama cha Siasa kilichompendekeza kuwa mgombea wa kiti cha udiwani. 

“Kwa kuwa umekoma kuwa Mjumbe wa Halmashauri, pia umepoteza sifa ya kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuanzia tarehe ya barua hii, hivyo unatakiwa kukabidhi ofisi pamoja na vifaa au mali yoyote ya Manispaa ya Ubungo ikiwemo gari kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo. 

Haya hivyo, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuthibitisha kupokea barua hiyo inayodaiwakuwa ya kughushi na yeye kuandika baru hiyo ya kumtaka meya huyo kukabidhi vifaa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic alisema hawezi kuzungumza suala hilo kwa muda huo na kutaka apigiwe baadaye kwa alikuwa kwenye kuratibu shughuli za uboreshaji wa daftari wa uandikishaji wapigakura vituoni. 

Hata hivyo, alipotafutwa kwa mara nyingine kama alivyoagiza simu yake iliita bila kupokelewa hadi tunakwenda mitamboni. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles