24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari Kavu Kwala yaanza kupokea mizigo

 MWANDISHI WETU – PWANI 

SHENA ya kwanza ya makontena 29 imewasili katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani kwa njia ya treni kutoka Bandari ya Dar es Salaam. 

Hii ni mara ya kwanza kwa Bandari hiyo kupokea kontena ambako inamaanisha kuanza rasmi kwa bandari hiyo iliyojengwa ili kusaidia kupunguza mlundikano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam. 

Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa treni hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki bandarini hapo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, alisema kuanza kwa bandari kavu ya Kwala ni hatua muhimu katika kumaliza changamoto ya msongamano inayoikabili Bandari ya Dar es Salaam. 

Alisema msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam umekuwa ukisababisha malalamiko kutoka kwa wateja na kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kusimamia mradi huo hadi kufikia kuweza kupokea treni ya behewa. 

“Bandari hii inafungua ukurasa mpya na mwanzo wa operesheni za kuondoa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam zoezi ambalo pia litapunguza kuingia kwa malori ya mizigo katikati ya jiji hivyo kupunguza foleni za magari na kulinda miundombinu ya Barabara zetu,” alisema Nditiye. 

Alisema amefarijika kuona kazi kubwa iliyofanyika ikiwemo ujenzi wa sakafu ngumu katika eneo kwa ajili ya kuhudumia makasha, ujenzi wa mitaro ya kuzuia mafutiko, miundombinu ya awali ya umeme, maji, Tehama, ulinzi, zimamoto, nyumba za watumishi na ofisi. 

Aidha aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TPA kuhakikisha bandari hiyo inatumika vizuri na kukamilisha ujenzi kwa kuzingatia vigezo vyote vya ubora. 

Pia alitoa changamoto kwa uongozi wa Wilaya ya Kibaha na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kutumia uwepo wa bandari hiyo ya Kwala kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa mkoa huo. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Profesa Ignas Rubaratuka, alisema mradi huo ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya tano kupunguza msongamano ndani na nje ya Bandari ya Dar es Salaam. 

Alisema mradi huo ni utekelezaji wa dhana ya hapa kazi tu ulioanza kufuatia maelekezo ya Serikali baada ya kuona eneo hilo linafaa zaidi kuliko lile la Kisarawe. 

Profesa Rubataruka alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Tanzania kutumia bandari zilizopo kwani utendaji na usalama umeimarika zaidi. 

“Tumeweza kurudisha heshima ya bandari kwa kuongeza ufanisi na kuimarisha usalama na bado tunaendelea na kuboresha bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara ili kuweza kuongeza ufanisi zaidi na kuvutia wateja wapya na kurudisha wale wa zamani ambao walituhama,” alisema. 

Akielezea utekelezaji wa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusidedit Kakoko alisema unatekelezwa kwa awamu katika eneo la hekta 60 ambazo ni sehemu ya hekta 500 za eneo lililotwaliwa na Mamlaka hiyo katika Kata ya Kwala. 

Alisema mradi huo ulioanza Februari 2017 unatekelezwa na Mkandarasi Suma JKT kwa gharama ya jumla ya Sh bilioni 47 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu. 

Mhandisi Kakoko alieleza kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha ufyekaji wa eneo la hekta 120, kulisawazisha, kujaza kifusi, kujaza matabaka ya changarawe na ujenzi wa reli kilomita 1.3 kutoka kituo cha Kwala hadi bandarini hapo. 

Awamu ya pili ilihususha kunyanyua tuta kumwaga zege na kuweka reli tano zenye urefu wa mita 500 kila na kuzungusha ukuta wenge urefu wa Kilomita 3.2. 

Kakoko alisema awamu hiyo pia inahusisha uwekaji wa miundombinu ya huduma za umeme, maji, mawasiliano na vizima moto pamoja na ujenzi wa nyumba za muda za watumishi na ofisi. 

Alisema hadi sasa mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 20.5 sawa na asililimia 45 huku mradi ukiwa asilimia 70 ukitarajiwa kukamilika Julai. 

Alisema awamu ya tatu itafuata ambayo ni ujenzi wa barabara ya kilomita 15.5 kwa kiwango cha changarawe ikiwa ni hatua za awali za kuijenga kwa kiwango cha zege. Barabara hii inaunganisha bandari kavu ya Kwala na barabara ya Morogoro eneo la Vigwaza. 

 Kakoko alisema pia bandari hiyo itaunganishwa na reli ya kisasa ya SGR ambayo itatumika kupeleka kontena mikoani na nje ya nchi. 

Aliongeza pia kuwa ujenzi wa bandari hiyo ya Kwala utahusisha sekta binafsi ambao wapewa maeneo ya kuweka ICD’s ndani ya eneo hilo ambapo miundombinu itakuwa inamilikiwa na TPA. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles