MWANDISHI WETU
TUNAFAHAMU katika jamii yetu wapo watoto wanaokulia katika vituo vya yatima kwa sababu ama wazazi wao wamefariki, hawajulikani waliko au hawana uwezo wa kuwapa matunzo. Wengine wanaishi katika mazingira magumu bila uangalizi wowote rasmi. Hawa nao inawezekana hawana wazazi au wana wazazi wasioweza kuwatunza.
Kwa upande mwingine, wapo watu wazima wenye shauku ya kutunza watoto lakini hawana watoto wa kuzaa au basi wanahitaji kuwasaidia watoto hawa. Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu kisheria kuwasaidia watu wenye nia ya kuasili mtoto kwa kufuata taratibu za kisheria.
Kuasili ni haki anayopewa mtu –mwenye sifa– kutambulika kisheria kama mzazi wa mtoto. Mtoto anapoasiliwa, mzazi aliyemzaa anapoteza haki na wajibu kama mzazi. Badala yake mzazi aliyemuasili mtoto atakuwa na haki, wajibu na majukumu ya kiuzazi kwa mtoto. Maana yake ni kuwa ikiwa mzazi aliyemuasili mtoto atafariki, mali zake zote zitarithiriwa na mwanawe wa kuasili.
Nani anaweza kuasili mtoto
Ndugu au mtu yeyote anayeishi Tanzania mwenye umri wa miaka 25 na angalau mwenye miaka 21 zaidi ya mtoto anayeasiliwa; mwanamke asiyeolewa aliye raia wa Tanzania au wenza –mke na mume– waliokubaliana kumwasili mtoto kwa maslahi ya mtoto. Mahakama itabidi ijiridhishe kwamba wenzi hao wamekubaliana kumuasili mtoto.
Sheria hii inamruhusu mwanamume kutuma maombi ya kumwasili mtoto ikiwa mahakama itajiridhisha kwamba yapo mazingira maalumu yanayohalalisha utaratibu huo. Wenzi wanaoishi bila kuwa na ndoa inayotambulika kisheria hawawezi kukubaliwa kuendelea na utaratibu wa kumuasili mtoto. Ndio kusema watu wanaoishi kinyumba bila kuwa na ndoa hawawezi kuasili mtoto.
Hata hivyo, ili maombi yoyote ya kumuasili mtoto yakubalike, lazime mwombaji awe ameishi na mtoto husika kwa angalau miezi sita mfululizo kabla ya tarehe ya maombi husika.
Mwombaji asiye raia wa Tanzania anaweza kuasili mtoto ikiwa ameishi Tanzania kwa angalau miaka mitatu mfululizo; amemlea mtoto kwa angalau miezi mitatu chini ya uangalizi wa afisa ustawi wa jamii; hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai na mahakama ya nchini kwake inaheshimu na kutambua maombi yake.
Utaratibu wa kufuata
Sheria ya Mtoto inaelekeza kwamba maombi ya kuasili mtoto yatatumwa Mahakama Kuu baada ya kupata ridhaa ya mlezi au mzazi wa kumzaa mtoto. Mahakama itajiridhisha ikiwa mlezi au mzazi wa mtoto husika anaelewa matokeo ya mwanawe kuasiliwa na ikiwa kweli ameshindwa kumtunza mtoto au amekuwa na tabia ya kumnyanyasa mtoto.
Katika mazingira ambayo mzazi au mlezi hana uwezo wa kutoa ridhaa mahakama lazima ijiridhirishe kuwa utaratibu wa kumuasili mtoto unazingatia maslahi ya mtoto na kwamba matakwa ya mtoto yamezingatiwa. Kwa mtoto mwenye umri wa angalau miaka 14 lazima ridhaa yake izingatiwe isipokuwa kama mtoto hana uwezo wa kujieleza.
Katika maombi ya kuasili mtoto, taarifa zifuatazo zitahitajika. Tarehe na mahali alikozaliwa mtoto; jina, jinsia na jina la ukoo la mtoto kabla na baada ya kuasiliwa; jina, jina la ukoo, anuani, mahali pa kuzaliwa, mahali anapoishi, uraia na kazi ya mzazi anayemuasili mtoto.
Wakati utaratibu wa kuasiliwa mtoto ukiendelea kufanyiwa kazi, mtoto atakuwa chini ya uangalizi wa afisa ustawi wa jamii na hatasafirishwa nje ya nchi bila ruhusa ya mahakama.
Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.