23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti: Ongezeko la joto husababisha matatizo ya akili

HASSAN DAUDI Na MITANDAO

LICHA ya matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya kishirikina na msongo wa mawazo kutajwa kuwa ndio vyanzo pekee vya ugonjwa wa afya ya akilli, joto nalo limebainika kusababisha matatizo hayo.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Harvard kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT), umedai kuwa kwa kadiri dunia inavyoshuhudia ongezeko la joto, idadi ya watu wenye matatizo hayo huongezeka.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliotokana na takwimu zilizokusanywa kwa zaidi ya miaka 10, joto linapoongezeka kwa nyuzi (degree) moja tu, ongezeko la watu wenye tatizo hilo hufikia asilimia mbili.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2016, dunia ilishuhudia ongezeko kubwa zaidi la joto na kwa kuhusisha na utafiti huo mpya, ndicho kipindi kilichokuwa na vichaa wengi.

Kilichofanyika katika utafiti wa Harvard na MIT ni kuzikusanya takwimu za ongezeko la joto duniani kisha kuzilinganisha na taarifa au matukio ya ugonjwa wa akili.

Hapo ndipo ilipobainika kuwa miezi iliyokuwa na joto kali nchini Marekani na Mexico, kesi za wagonjwa wa akili nazo zilikuwa zikiripotiwa kwa kiasi kikubwa, tofauti na ilivyokuwa awali.

Mfano; kwa Marekani pekee, illionekana kuwa watu milioni mbili walipata tatizo hilo la akili na hata wengine kufikia hatua ya kujiua, ukiacha waliokuwa wakilazwa hospitali au kupelekwa kwa wanasaikolojia kupatiwa tiba ya ushauri.

Mapema mwaka huu, Chuo Kikuu cha Stanford nacho kilifanya utafiti unaofanana na huu, ambapo kilibaini kuwa kila joto lilipokuwa likiongezeka kwa nyuzi moja, matukio ya watu wenye matatizo ya akili nayo yaliongezeka.

Wakitoa mfano wa nchi za Marekani na Mexico, utafiti huo ulidai kuwa jumbe nyingi katika mitandao ya kijamii, hasa Twitter, zilikuwa za ajabu kwamba, waliokuwa wakizituma walionekana kutokuwa sawa kiakili, na matukio ya watu kujitoa muhanga yaliongezeka.

Utafiti huu mpya umedai kuwa kila joto linapoongezeka kwa nyuzi moja, Marekani imekuwa ikizalisha wagonjwa wa akili 88,000.

Hata hivyo, wakosoaji wa kazi iliyofanywa na vyuo na taasisi hizo za elimu, Havard na MIT, wamedai kuwa utafiti wao haujaonesha ni namna gani joto linalovyoweza kuchangia moja kwa moja katika kuiharibu afya ya akili ya binadamu.

Wakionesha kutopingana na kazi nzuri ilivyofanywa na wenzao hao, walishauri utafiti mwingine uangazie namna ubongo wa binadamu unavyoweza kuathiriwa na joto, hivyo kusababisha mtu kurukwa na akili.

Ifahamike kuwa Marekani kwa sasa inakabiliwa na tatizo hilo kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya taifa hilo lililopata uhuru wake mwaka 1776.

Marekani iliyokuwa chini ya Uingereza zama za ukoloni, imekuwa ikitumia fedha nyingi kuendana na kasi ya tatizo hilo, ambapo inaelezwa kati ya watu watano, mmoja anasumbuliwa na ugonjwa wa afya ya akili.

Katika hilo, wanasaikolojia wanakiri kuwa wakati wa joto, kiwango cha hasira huwa ni kikubwa, kwamba ni rahisi watu kukorofishana endapo tu watapishana kauli katika mazungumzo yao.

Wakati huo huo, watafiti wanasema huenda si joto pekee linaloweza kuwa chanzo kikubwa, bali pia majanga mengine ambayo yamekuwa yakitokea katika jamii, kama vile mafuriko, kimbunga, baa la njaa au radi.

Wanatoa mfano wa kile kilichotokea mwaka 2005 nchini Marekani, baada ya kimbunga cha Katrina, wagonjwa wa akili waliongezeka kwa asilimia nne, wengi wao wakiwa ni wale waliopoteza makazi, familia na mali zao kutokana na janga hilo.

Hivyo basi, utafiti wa Havard na MIT unaweza kuwa msaada mkubwa katika vita inayoendelea duniani kote dhidi ya shughuli za binadamu, hasa za kiuchumi, ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikichangia ongezeko la joto  au majanga mengine yaliyotajwa hapo juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles