26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Nyuma ya pazia ajali za viogozi, watumishi serikalini

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

AJALI zinazohusisha gari za viongozi wa vyama, serikali na watumishi wa umma zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara, hali inayoibua maswali katika jamii. Tatizo hili linaonekana kuzidi kushika kasi siku hadi siku na hivyo kushtusha watu wengi.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria asilimia 90 ya ajali zote hutokea katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, licha ya kuwa kuna idadi ndogo ya magari.

WHO linakadiria watu milioni 1.25 hufariki dunia kwa ajali za barabarani duniani, idadi ambayo ni sawa na vifo vya watu 3,400 kila siku na waathirika wengi wakiwa ni vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 29.

Kwa mujibu wa Shirika hilo, kati ya asilimia 49 ya vifo vyote vinavyotokea kwa ajali za barabarani waathirika wengi huwa ni abiria, watembea kwa miguu, waendesha pikipiki, baiskeli na madereva wa magari.

 

Mwaka 2018

Anasema hivi sasa wanazo takwimu za kipindi cha Januari hadi Mei ambazo zinaonesha kumetokea jumla ya ajali 408 ikiwa ni pungufu ya ajali 109 ikilinganishwa na kipindi cha Januari hadi Mei, 2017 ambapo zilitokea ajali 607.

“Takwimu za kipindi cha Januari hadi Mei, 2017 zinaonesha kulikuwa na vifo 302 na majeruhi 455 wakati Januari hadi Mei, 2018 kumetokea vifo 302 na majeruhi 344 ikiwa ni pungufu ya majeruhi 111,” anabainisha.

 

Vyanzo vya ajali

Anasema visababishi vikuu vya ajali hizo ni sababu za kibinadamu kwa kiwango cha asilimia 86.4, ubovu (uchakavu wa vyombo) asilimia 7.7 na sababu za kimazingira kwa asilimia 5.9.

“Ndani ya sababu za kibinadamu kuna mjumuisho wa sababu nyingi ikiwamo ulevi, uzembe, katika mwaka 2016 jumla ya ajali 2,583 zilitokana na uzembe wa madereva na mwaka 2017 jumla ya ajali 1,573,”  anasema.

Anasema kwa upande wa sababu za kimazingira hujumuisha ubovu wa miundombinu na hali ya hewa.

 

 

Viongozi na watumishi wa umma

Kamanda Sokoni anasema Machi 29, 2018 katika eneo la Bwawani, mkoani Morogoro, wabunge sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walinusurika kifo kufuatia ajali ya gari walilokuwa wakisafiria.

Anasema chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni mwendo kasi wa dereva wa gari hilo.

Anasema Mei 21, 2018, eneo la Msoga Chalinze, mkoani Pwani, gari lenye namba za usajili STK 5923 la Wizara ya Viwanda na Biashara lililokuwa na maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) lilipata ajali wakiwa njiani kuelekea Dodoma.

Anasema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili papo hapo na mmoja alijeruhiwa akawahishwa hospitalini kwa matibabu. Chanzo cha ajali hiyo pia ilikuwa ni mwendo kasi.

Anasema Julai 30, 2018,  huko Geita, Msemaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Shadrack Sagati, alifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria na watumishi wengine wa wizara hiyo kupata ajali na kupinduka.

Anataja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendokasi wa dereva na kwamba watumishi waliokuwa wamejeruhiwa waliwahishwa hospitalini kwa matibabu.

Anataja ajali nyingine kuwa ni ile ya iliyotokea Agosti 4 mwaka huu, ikihusisha gari la Serikali lenye namba za usajili STL 5718 alilokuwa akisafiria Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, lilipata ajali mkoani Manyara.

Anasema katika ajali hiyo, Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Hamza Temba, alipoteza maisha papo hapo na wengine akiwamo dereva walijeruhiwa.

Anataja chanzo cha ajali kuwa ni dereva alikuwa mwendo kasi na akajaribu kumkwepa Twiga aliyeingia barabarani ghafla katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Burunge, inayopakana na Hifadhi ya Tarangire na Manyara.

Anasema kitendo hicho kilisababisha gari kupinduka na kuua.

Taarifa katika mitandao mbalimbali zinaonesha Machi 6, 2018, Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdalah Chikota, akiwa na waandishi wa habari watatu ndani ya gari lake, walipata ajali katika eneo la katikati ya vijiji vya Navikole na Chawi mkoani Mtwara.

Ilielezwa kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari lao kupinduka na hivyo kuwasababishia majeruhi katika sehemu mbalimbali za miili yao.

Mei 11, 2018, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Jesca Kishoa, naye alinusurika kifo kufuatia ajali aliyoipata eneo la mataa ya ‘Area’ D mkoani Dodoma wakati alipokuwa akielekea bungeni.

Agosti 9, 2018 gari la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Magereri, lenye namba za usajili T 348 CSR lilipata ajali eneo la Issuna, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva wake Thomas Maro, ambaye alifariki dunia papo hapo.

Septemba 4, mwaka huu, Msafara wa Rais Dk. John Magufuli, uliokuwa ukielekea Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, ulipata ajali katika Kijiji cha Kasuguti, Kata ya Kisorya, baada ya magari manne kugongana.

Ilielezwa katika eneo hilo ambako barabara ilikuwa ikijengwa, waandishi wa habari wawili walijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kupinduka.

Septemba 9, mwaka huu, msafara wa Rais Magufuli ulipata ajali tena, ambapo gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari wa Mkoa wa Simiyu, liligongwa na magari mengine yaliyokuwa katika msafara huo Mhanuzi wilayani Meatu, baadhi walijeruhiwa na kuwahishwa hospitalini kwa matibabu.

Oktoba 21, mwaka huu, asubuhi huko eneo la Manyoni, gari la Wizara ya Kilimo likiwa na maofisa watano lilipinduka na wote waliokuwa katika msafara huo walifariki dunia papo hapo.

 

Tamko la Waziri Lugola

Agosti 4, mwaka huu, akizungumza na waandishi wa habari, mkoani Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alionya viongozi kutokuwa chanzo cha mwendo kasi usio wa kawaida barabarani.

Aliwataka kuwahimiza madereva wao kupunguza mwendo ili kuepuka ajali zinazojitokeza.

“Viongozi tusiwe chanzo cha mwendo kasi, sisi tuwe ‘speed’ gavana,” anasema Waziri Kangi wakati alipokuwa akizindua Baraza jipya la Taifa la Usalama Barabarani.

Ni ukweli kwamba ajali nyingi zinazohusisha gari za viongozi zilizotokea nchini mwendo kasi umekuwa ukitajwa kuwa chanzo kikuu.

 

Safari za usiku

Kassim Jumanne (si jina lake halisi), anasema amekuwa dereva tangu mwaka 1995 na kuanza rasmi kuendesha gari za viongozi mwaka 2006 baada ya kupata mafunzo maalum katika Chuo Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Anasema changamoto kubwa aliyokuwa akiipata ni wakati alipokuwa akilazimika kusafiri usiku na kiongozi aliyekuwa akimendesha hasa kuelekea jijini Dodoma.

“Najua hili litakuwa linawapa changamoto hata madereva wengine wa viongozi na watumishi wa umma, kwani ni vigumu kujua gari inayokuja mbele yako ni kubwa au ndogo.

“Usipokuwa makini unaweza kusababisha ajali kwani utadhani gari ni ndogo kumbe ni kubwa, inahitaji umakini wa hali ya juu ikibidi kupunguza mwendo ili uweze kuendelea na safari mkiwa salama,” anasema.

Anasema wakati mwingine huwa wanajikuta wakiendesha gari mwendo kasi, lakini nikuambie ukweli wapo viongozi ambao hawataki kabisa kuendeshwa hivyo.

 

Vikao vya Bunge

Anasema hiki ndicho kipindi ambacho huwa kigumu kwa madereva kwa sababu ndicho chenye pilika nyingi kuliko hata vipindi vingine kazini.

“Viongozi huhitaji kuwahi kwenye vikao, tena ikiwa ni kipindi cha Bunge ndiyo kabisa, madereva nao hutaka kuwahi mapema wakatafute mahala pa kulala (hoteli) ambako ni salama,” anasema.

 

Madai ya posho

Anasema wakati akiwa kazini aliwahi kukumbana na kadhia hii kwamba wapo baadhi ya viongozi ambao huwa hawawapatii madereva wao posho.

“Japo sikukumbana nalo sana…Kimsingi mnapokwenda safari unatakiwa kupatiwa posho yako yote ikiwamo pia fedha ya dharura, lakini mkiondoka safari kuna baadhi ya viongozi ilikuwa kama humwambii akupatie basi unaweza kujikuta hupewi kabisa ingawa imeidhinishwa.

“Sasa hali ile huwa inamuweka dereva katika wakati mgumu, anakuwa na mawazo hasa anapoifikiria familia yake aliyoiacha nyumbani hivyo, kujikuta akisababisha ajali,” anasema.

 

Gwiji usalama barabarani anena

Gwiji wa Masuala ya Usafirishaji na Uchukuzi Tanzania na Mbobezi wa Usalama Barabarani nchini, Henry Bantu, anasema ni suala linalosikitisha.

“Kwa kawaida magari ya viongozi yanatakiwa kuendeshwa na madereva walio mahiri, wanaojitambua na ambao wamefundishwa vilivyo na kufundwa pamoja na kupitia zile kozi za udereva wa kujihami,” anasema.

Bantu anasema ni lazima dereva ajue wakati wowote anapoendesha gari anazungukwa na hatari, ambazo kwa kawaida zimegawanyika katika makundi mawili, hatari zilizopo na hatari zinazotegemewa.

 

Kuzingatia muda

Anasema dereva wa kujihami lazima awe anazingatia na kuheshimu muda, kwa mfano, kama ni muda wa kupumzika apumzike na pengine apumzishwe.

Anasisitiza kama kuna safari ya kiongozi ni lazima dereva aambiwe mapema ili ajipumzishe na ajiandae kisaikolojia.

“Lakini kumetokea fununu kwamba kutokana na

jukumu tulilonalo sasa la kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhamia Dodoma, viongozi wengi wanashtukia wana shughuli za kufanya kwenye ofisi ndogo Dar es Salaam, lakini pengine zikazuka nyingine za haraka kwenye ofisi mpya Dodoma.

“Kwa hiyo, kiongozi anamuhamasisha dereva wake waende Dodoma kwa haraka ambapo matokeo yake inawaweka viongozi hao kwenye hatari ya kupata ajali,” anatoa mfano.

 

Jinsi ya kupambana nazo

Anasema mafunzo ya kina ya namna na jinsi ya kutumia barabara zetu kwa usalama zaidi ndiyo mwarobaini wa kupunguza ajali za barabarani.

Gwiji huyo anasema madereva wanapaswa kutambua kwamba nafasi ya kuwa dereva wa kiongozi yeyote yule ni ‘nyeti’ na ni suala linalohitaji umakini.

 

Safari za kushtukiza

Anasema ajali nyingi za uso kwa uso, za kuchochora (kuacha njia) au gari kupinduka (mystery single vehicle crashes), zina uhusiano mkubwa na hali ya uchovu wa dereva na uyumbishaji mawazo.

“Kumkurupusha dereva, kwa kumpa taarifa ya safari ndani ya muda mfupi nalo ni jambo linalosababisha matatizo barabarani,” anasema Bantu.

 

Sakata la vyeti feki

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali (Taifa), Saidi Kapande, anathibitisha kuwa ajali zinazotokea hivi sasa na kuhusisha magari ya viongozi, zinatokana na baadhi ya madereva wanaowaendesha viongozi kutokuwa na uzoefu wa kutosha na kwamba leseni zao zilikuwa ni za ‘magumashi’.

“Kuna vyanzo vingi vya ajali lakini kwa upande wa ajali zinazohusisha gari za serikali naweza kusema tatizo kubwa ni madereva wengi wageni hivyo hawana uzoefu wa kutosha,” anasema.

Anasema wengi waliokuwa na uzoefu wa kutosha waliondolewa kazini kutokana na kukosa vyeti halali.

Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Dk. Leonard Ndumbaro, anasema awali kulikuwa na changamoto ambayo tayari  imefanyiwa kazi.

“Uhakiki wa vyeti uliwagusa kada zote za watumishi wa umma, lakini si kweli kwamba ajali za viongozi na watumishi wa umma zinatokana na  kuondolewa kazini kwa madereva wakati wa uhakiki ule.

“Kwa mfano, ajali iliyohusisha gari ya Waziri Kigwangwalla dereva alikuwa anakwepa twiga aliyekuwa akikatisha barabarani, kuna suala la ubovu wa miundombinu .

“Siamini kwamba ajali zinazotokea ni kutokana na madereva kukosa sifa au uzoefu, ajira za utumishi wa umma zinaendana na kada husika, sifa za dereva wa serikali zimeidhinishwa katika muundo wa madereva wa Serikali kama ilivyo, sifa za waandishi wa habari wa serikali zimeizinishwa katika muundo wao na hata kada zinginezo,” anasema.

Anasema muundo huo umeainisha sifa zote anazotakiwa kuwa nazo dereva, anapaswa kufanya nini ikiwa anataka kupanda cheo kazini.

 

Kauli ya Adadi

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wa Masuala ya Usalama Barabarani Tanzania, Adadi Rajab, anasema ili kukabili ajali hizo kila mmoja anapaswa kuwajibika katika nafasi yake.

“Ajali nyingi zinatokana na kiongozi mwenyewe, kwa sababu anaona dereva anaenda kasi, lakini hamwambii apunguze mwendo, anamuacha. Kimsingi zinaweza kuzuiwa na kiongozi kwa kumdhibiti dereva wake.

“Kwa upande mwingine trafiki nao wanachangia hizi ajali maana huwa wanaona kabisa gari zinakimbizwa lakini hawawakamati, hawachukui hatua za kisheria, wanawapa heshima,” anasema.

 

Kwanini hawachukuliwi hatua?

Mwanasheria wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Deus Sokoni, anasema si kweli ingawa changamoto ipo kwani madereva hao hutumia kivuli cha nafasi zao (kuendesha viongozi) kuwabeza askari pindi wanapowasimamisha.

 

Nini kifanyike?

Balozi Adadi anasema: “Ni kweli ajali za viongozi zimeripotiwa kwa wingi  hivi karibuni, wakati mwingine viongozi wanakuwa na kazi nyingi ikiwamo vikao vya Bunge lakini pamoja na hayo inabidi waangalie maisha yao na madereva wao kwa sababu ajali ni ajali.

“Ni lazima wafuate sheria za usalama barabarani, wasikimbie barabarani na madereva wadhibitiwe ipasavyo,” anasema.

 

Matengenezo ya barabara

Anasema ni muhimu barabara zikakarabatiwa ili kuepusha ajali za mara kwa mara.

 

Ajira zisiwe za upendeleo

Bantu ajira za kundi hili ni muhimu zifanyike kwa umakini zaidi, uchaguzi wake uwe wa kitaalamu na si kuangalia cheti pekee.

“Ni vema pia dereva naye ‘akajiongeza’ kujua mapema ni safari za namna gani na lini kiongozi anayemuendesha anaweza kuzifanya, kwa sababu naye ni binadamu wakati mwingine anaweza kusahau kumjulisha mapema dereva juu ya safari inayotegemewa.

 

Kozi za rejea

“Viongozi wasiwe ndiyo wahamasishaji wakuu wa mwendokasi wakiwa wanasafiri, pia wasisahau kuwaruhusu madereva kuhudhuria kozi za rejea angalau mara moja kila baada ya miaka miwili.

“Kozi za namna hiyo husaidia kuwaimarisha madereva na kuwaongezea uzoefu na maarifa stahiki ya taaluma,” anasema Bantu.

 

Usiri wa safari

Anaongeza “Madereva wanapaswa kujua pia kumuendesha kiongozi ni tofauti na kuendesha tu watu au abiria wa kawaida, kunatakiwa usiri kutegemeana na aina ya safari.

 

Trafiki Makao Makuu

Kamanda Sokoni anasema ni kweli kwamba licha ya kozi maalum (VIP) wanayopatiwa, madereva wanahitaji mafunzo ya ziada.

“Wanapaswa kupata mafunzo ya udereva wa kujihami (defensive driving), lazima wafundishwe kwa sababu ajali hizi zinaleta hasara kubwa,” anasema.

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waandishi waliochaguliwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia mradi wa Bloomberg (BIGRS).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles