24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti: Asilimia 72 hawaelewi tiba ya mionzi

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) umeonyesha kuwa asilimia 72 ya wananchi hawana uelewa kuhusu vipimo na tiba ya mionzi huku asilimia 64 ya wagonjwa wakipata huduma hiyo kwa kuwaamini madaktari.

Akizungumza na MTANZANIA wakati wa mahojiano maalumu, mtaalamu bingwa wa matumizi ya mionzi katika taasisi hiyo, Steven Mkoloma, alisema hali hiyo ya uelewa mdogo inaweza kusababisha wagonjwa kuchelewa kutibiwa na hata wengine kupoteza maisha kwa kuhofia matibabu hayo.

Utafiti huo uliofanyika katika mikoa mitano nchini ukihusisha watu 30 kwa kila mkoa, pia ulibaini asilimia 54 ya madaktari wa ngazi zote walikuwa na ufahamu kuhusu vipimo na tiba mionzi.

“Huu ni utafiti ambao ulikuwa unaangalia ufahamu na uelewa wa jamii kuhusu mionzi inayotumika katika uchunguzi  wa magonjwa na tiba kwa Tanzania, utafiti huu ulifanyika katika mikoa mitano tofauti ukiuliza swali moja, na mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Kilimajaro, Mwanza, Mbeya na Ruvuma.

“Katika kila mkoa kulikuwa na washiriki 30 ikiwa 10 ni wagonjwa ambao waliandikiwa kufanya vipimo vya X-ray au matibabu yanayohusisha mionzi, 10 madaktari na 10 wananchi ambao hawajawahi kuandikiwa kufanya vipimo vinavyohusiana na mionzi.

“Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kwamba asilimia 72 ya watu ambao hawakuandikiwa vipimo hivyo walikuwa na ufahamu mdogo wa mambo ya mionzi, asilimia 64 ya wagonjwa walikuwa na ufahamu mdogo, lakini asilimia 54 tu ya madaktari katika ngazi zote kuanzia ‘clinical officer’ na ‘specialist’ walikuwa na ufahamu wa mambo ya mionzi.

“Lakini pamoja na kwamba hawa wagonjwa na raia ambao hawajaandikiwa vipimo vya miozi ufahamu wao ulikuwa mdogo, lakini walikuwa na ujasiri wa kuendelea kupata huduma za mionzi huku kigezo kikubwa ambacho walikitazama ni imani yao kwa daktari,” alibainisha mtafiti huyo.

Alisema majumuisho ya utafiti huo yanaonyesha ufahamu mzima wa mambo ya miozi kwa Watanzania uko chini.

Alieleza kuwa sababu za asilimia 54 ya madaktari kuwa na uelewa ni baada ya kupata mafunzo shuleni.

“Hali hiyo inajulisha kuwa kuna haja ya elimu kutolewa zaidi hata kwa wahudumu wa afya.

“Kazi inatakiwa kufanyika kwa sababu kama hawa asilimia 72 hali ni hiyo, na ambao wamekwenda kufanya huduma kwa sababu wana imani na daktari na wakakutana na daktari ambaye hana ufahamu, ni rahisi kuahirisha huduma kwa sababu ya kukosa taarifa sahihi.

“Tunashauri Serikali na mamlaka zinazohusika na taarifa kwa jamii kuweka utaratibu ambao wahudumu wa afya wa kada mbalimbali pamoja na wananchi wataweza kupata taarifa za kutosha,” alisema Mkoloma.

Alisema uchunguzi wa kansa unahusisha sana mionzi, lakini matibabu inategemea mionzi, kwa hivyo kama mgonjwa au jamii watakuwa na taarifa sahihi, wanaweza kupata watu wengi wa kupata vipimo au matibabu na hivyo kupunguza kiwango cha wagonjwa wanaochelewa kufika hospitali au kupoteza maisha kabla hawajafika.

“Kimsingi watu wanaogopa kwa sababu wanaamini mionzi inaua seli, lakini kisayansi hutibu kwa sababu eneo linalofikiwa na mionzi ni lile tu ambalo lina tatizo, tunaua zile seli na kuruhusu mwili kutengeneza seli mpya ambazo hazina ugonjwa,” alisema Mkoloma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles