SAFU yetu ni Love Talk, ambayo hutukutanisha kila Jumamosi na kupeana haya na yale kuhusiana na maisha ya uhusiano na mapenzi.
Bila shaka wengi tunajifunza mambo mapya kupitia safu hii. Naweza kusema hapa ndiyo sehemu pekee ya kupanua mawazo na kukuza ubongo wako juu ya mambo yanayohusu uhusiano na mapenzi.
Kama ni mara yako ya kwanza kuanza kupitia ukurasa huu, umekutana na kona muhimu sana. Huna cha kupoteza. Utajengeka kila siku.
Marafiki zangu, leo nimekuja na mada mpya baada ya kuhitimisha ile ya wiki iliyopita. Nina imani kuna mengi mliyojifunza. Mada ya leo inatokana na maswali mengi ya aina moja niliyoyapata kwa muda mrefu kutoka kwa wasomaji mbalimbali.
Hebu msikie huyu: “Pole na kazi kaka Shaluwa, kuna kaka nawasiliana naye. Kiukweli tumezoeana sana, juzi hapa amesema eti ananipenda na anataka kunioa. Mimi nipo Mbeya, yeye anaishi Dar es Salaam.
“Hatujawahi kuonana, zaidi ya kuzungumza kwa njia ya simu tu. Nilifahamiana naye baada ya kukosea namba, ndipo tukakubaliana kuwa marafiki. Tafadhali naomba msaada wako maana ninachanganyikiwa kabisa. Ni kweli ananipenda? Naomba msaada wako.”
Kilio kama hicho nilikipata pia kutoka kwa msomaji mmoja ambaye naye sitachapa jina lake gazetini. Huyu alisema: “Nimekutana na rafiki kwenye group moja la WhatsApp, tunawasiliana mara kwa mara, ninahisi kumpenda huyo msichana. Naye ana kila dalili za kunipenda, tatizo sijaanza tu kumweleza. Hivi, inawezekana kweli tukapendana kabla ya kuonana?”
Bila shaka kuna picha umeipata kupitia maswali ya wasomaji hao wawili. Niliwaahidi kuandika mada gazetini ambapo ndipo wangepata majibu yao. Je, wewe upo kwenye kundi gani?
Umewahi kukutana na jambo hilo? Unadhani unaweza kumpenda mtu kabla ya kukutana naye? Sauti pekee inaweza kumfanya mtu ampende mwenzake kwa dhati na mapenzi yao yakadumu? Twende tukajifunze.
INAWEZEKANA?
Hili ni jambo la kwanza linalotakiwa kupatiwa majibu kabla ya kuendelea na mada hii. Huu ni mtazamo hasi. Jibu kwa kifupi tu ni haiwezekani. Utawezaje kumpenda mtu ambaye hujamuona?
Misingi ya kumpenda mwingine ikoje? Kanuni zipo wazi; KUPENDA ndiyo jambo la kwanza, ambapo ukweli ni kwamba huanza na kutamani, sasa itawezekanaje kumtamani mtu ambaye hujawahi kukutana naye?
Baada ya kupenda, kuna mambo mengine ya msingi ambayo ni muhimu kuzingatiwa ili kujihakikishia kwamba uliyempata ni mwenzi sahihi. Kuna suala la kuchunguzana tabia n.k, yote haya yatawezekana vipi kufanyika kabla ya kukutana?
Najua ni wengi wamekumbana na hili ninalolizungumzia hapa, unashindwa cha kufanya na kubaki gizani. Leo utarudi kwenye mwanga! Unajua chanzo cha yote hayo ni nini? Twende kwenye kipengele kinachofuata.
HUANZA HIVI…
Chanzo kikuu cha udanganyifu huu wa mapenzi huwa ni vyombo vya mawasiliano. Mfano mtu amepiga simu amekosea namba…mara anaanza ‘uko wapi? Haina neno, tunaweza kuwa marafiki?’
Mazoea yakizidi, kila mmoja huanza kumwuliza mwenzake vitu anavyopendelea na mambo mengine. Baadaye wanatongozana! Huelezana mambo mengi sana na ahadi nyingi wakiamini kwamba wanapendana kwa dhati!
Hayo huwa mawazo ya ndani na misukumo ya tamaa, lakini ndani ya moyo huwa hakuna mapenzi. Uhusiano wa namna hiyo hata ukianza huwa unaishia njiani.
Wengi hawapendi kukubaliana na ukweli huo, lakini wanaojuta kupoteza muda, fedha na hisia zao kwa wenzi wa namna hii ni wengi zaidi kuliko wale ambao mwisho wao ulikuwa wa kuingia kwenye ndoa.
Bado kuna machache ya kufafanua zaidi kabla ya kuhitimisha mada hii, wiki ijayo tutamalizia, USIKOSE!
Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kupitia group la WhatsApp la Love Moment? Kama ndivyo karibu inbox, andika ujumbe wako ukitaka kujiunga na kundi hilo, nasi tutakuunganisha.