23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

JPM AZIGOMEA NCHI ZA ULAYA

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amesema Tanzania inauona mkataba wa mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA) sawa na ukoloni mwingine.

Kauli hiyo aliitoa jana mbele ya mawaziri na viongozi mbalimbali wa serikali za Tanzania na Uganda baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Yoweri Museveni aliyemtembelea Ikulu, Dar es Salaam.

Katika hotuba ambayo ilirushwa mubashara na televisheni ya TBC 1, Rais Magufuli alisema mkataba wa EPA hauna faida kwa Tanzania, hivyo kuufuata ni sawa na kutumikia ukoloni mwingine ambao unaletwa kwa sababu ya mambo mengi.

“Kwa ujumla tumezungumza pia suala la EPA, nimemweleza kwamba sisi Tanzania tunaona EPA haina faida, ni ukoloni mwingine, huwezi ukazungumzia juu ya kujenga viwanda na wakati huo huo unashindana na watu wenye viwanda vikubwa.

“Hili tumezungumza kwa undani na tumekubaliana na rais kwamba wale wataalamu ambao walitusaidia sisi kutoa maelezo mazuri, watakwenda Uganda nako wakatoe maelezo mengine zaidi na yeye kwa msimamo wake amesema huwa anapenda kufanya kitu cha faida,” alisema Rais Magufuli.

Katika hoja hiyo, Rais Museveni alipopewa nafasi ya kuzungumza, alisema kuja kwa jambo la kushoto kumesababisha wengine kwenda kushoto na wengine kwenda kulia.

“Jambo dogo namna hii tunagawanyika,  ndiyo maana nimesema hapana nina ulazima wa kwenda na kujadili na Rais Magufuli kwa sababu hili jambo si juu ya EPA bali ni juu yetu sote.

“Linatuhusu sisi kwa sababu ni sawa na jeshi, kwamba ukiambiwa kushoto geuka sote tunageuka, sasa kama mnaambiwa kushoto geuka wengine wanageuka kulia basi gwaride litaharibika, kwahiyo nimekuja hapa tukaongea, pia nimekuwa na maongezi na watu wa Kenya ili kuwa na msimamo mmoja,” alisema Museveni ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili.

Alisema pamoja na kutafuta msimamo mmoja juu ya suala hilo, lakini majadiliano yanatakiwa yalainishwe ili yasije yakasababisha mkwamo.

Mazungumzo hayo kati ya Rais Magufuli na Museveni kuhusu EPA yamekuja baada ya Tanzania kukataa kusaini mkataba huo Oktoba Mosi mwaka jana.

Msimamo huo wa Tanzania tayari ulikuwa umeungwa mkono na Burundi huku nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenya, Rwanda na Uganda zikiwa tayari zimesaini mkataba wa EPA.

Awali Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais Museveni, wanaangalia kujenga bandari ya nchi kavu mkoani Mwanza ambayo itakuwa maalumu kuhudumia wafanyabiashara wa Uganda.

Pia alizungumzia ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, ambalo alitaka mkandarasi aanze ujenzi mara moja.

“Inawezekana vikawapo vitu vidogo vidogo vikawa vinabebwa na mwekezaji, hivyo vinaweza vikabebwa wakati ujenzi unaendelea, lakini mwekezaji asitafute visingizio vidogo vidogo bali afanye kazi, alitakiwa kuanza ujenzi jana (juzi),” alisema.

MJADALA WA EPA

Novemba 10 mwaka jana, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walijadili mkataba wa EPA na hoja mbalimbali za kuishauri Serikali zilipendekezwa.

Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema mkataba huo hauna manufaa kwa nchi.

Katika maelezo yake, Zitto aliwasihi wabunge wenzake kwamba unapofika wakati nchi inapokwenda kupambana na wengine lazima wabunge kuwa kitu kimoja.

“Siridhishwi na mjadala unapokwenda kwa sababu hatuoni aibu kutofautiana katika jambo ambalo huko tunakokwenda tunakwenda kupigwa na wenzetu.

“Nitawaambia kitu kimoja kwanini Kenya wamesaini. Jibu lake ni biashara ya maua ndiyo imewafanya Kenya waone potelea mbali kuhusu EAC bora wasaini,” alisema Zitto.

Alisema wabunge wanatakiwa kujiuliza mara mbili kwa nchi kama Kenya ambayo ina uchumi mkubwa zaidi ya Tanzania kuwa tayari kuvunja umoja wa EAC kwa sababu ya maua.

“Mnarushiana mishale hii, hili si jambo la chama kimoja, naomba tunapojadili tuitazame nchi,” alisema.

Katika muktadha huo, Zitto alitaja masharti kadha wa kadha ambayo yanaifanya Tanzania kusita kusaini mkataba wa EPA.

Alitaja sehemu ya masharti ya mkataba huo ni kuondoa kodi kwa bidhaa ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Alisema kwa masharti ya namna hiyo, nchi ya Ethiopia imekataa kukubaliana na nchi za EU kwa hoja kwamba wanataka kwanza kuimarisha uwezo wao wa ndani.

“Unaporuhusu kutokutoza kodi za bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi na unaporuhusu bidhaa kutoka EU kuingia hapa nchini bila kodi, maana yake ni kwamba hutakuwa na kodi ya bidhaa zote kutoka EU, kwahiyo tukikubali kwa ujumla EAC yote tutapoteza Euro bilioni 3.6 (Sh trilioni 8) na kwa Tanzania peke yake tutapoteza dola milioni 823 na hesabu hizi zimefanywa na EU wenyewe.

“Nini ambacho kinatakiwa kifanywe? Kunatakiwa kuwe na mfumo wa kufidia hiyo hasara, lakini EU wamekataa kufidia hiyo hasara,” alisema.

Zitto alikwenda mbali kwa kupendekeza kuwa itakuwa ni faida kubwa kwa Tanzania kama mkataba wa EPA utasainiwa na Afrika nzima.

Naye Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), aliwahi kukaririwa akisema kuwa mkataba wa EPA hautambui nchi bali unatambua jumuiya.

Alipendekeza kuwa ni bora yangepelekwa mapendekezo ambayo yataufanya mkataba huo kutambua kila nchi.

“Alisema mkataba huo unatufanya sisi kuwa wazalishaji wa malighafi na tuwe soko lao, pia mkataba huu unapingana na ndoto ambayo Tanzania imekuwa nayo tangu tumepata uhuru.

“Wametuwekea masharti kwamba ukitaka kufanya ulinzi katika soko lako la ndani au maendeleo yako ya ndani, lazima upate uthibitisho kutoka kwao, wao ni nani, sisi sio nchi huru?” alihoji Bashe.

Alisema mkataba huo wa EPA lazima uwe wa kunufaisha pande zote.

MAGUFULI KUPELEKA BOMBARDIER UGANDA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema kuwa alimuomba Museveni kuruhusu ndege za Tanzania kufanya biashara na nchi yake.

“Tumemuomba Rais Museveni kuwa ndege zetu sita ambazo tumezinunua, nyingine zitafika mwakani mwanzoni, ziwe zinakwenda nchini mwake, Kampala na Entebbe na rais amesema hakuna tatizo, naamini kwa njia hiyo tutaimarisha biashara,” alisema.

Pia Rais Magufuli alisema japokuwa biashara kati ya Tanzania na Uganda imekua kutoka Sh bilioni 178.19 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 193.59 mwaka 2016 bado nchi hizi zinapaswa kuongeza zaidi na ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi zote mbili kushirikiana zaidi katika biashara na uwekezaji.

“Uwekezaji wa wafanyabiashara wa Uganda hapa nchini Tanzania una thamani ya Dola za Marekani milioni 46.05 na umezalisha ajira 1,447.

“Watanzania wanaoishi Uganda ni wengi kuliko wanaoishi katika nchi nyingine yoyote duniani, hii ina maana tunapaswa kushirikiana zaidi na kufanya biashara zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema ili kukuza biashara na Uganda, Tanzania imeanza kutekeleza miradi mikubwa ikiwamo ujenzi wa reli, bandari kavu ya Mwanza ikiwa ni pamoja na kukarabati meli ya MV Umoja itakayovusha mizigo hadi bandari ya Port Bell kupitia ziwa Victoria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles