SHAHIDI wa upande wa Serikali, Abdallah Mandai, katika kesi ya kuchoma Kituo cha Polisi Bunju A amedai kwamba aliegesha gari lake kituoni hapo aliporudi akalikuta limeharibiwa vibaya.
Shahidi huyo wa sita alidai hayo jana mbele ya Hakimu Thimos Simba wakati akitoa ushahidi wake kwa upande wa mashtaka.
Alidai aliegesha gari hilo kituoni hapo baada ya kuona barabara imezingirwa na kundi kubwa la watu wakiwamo wanafunzi, wakiandamana.
Alidai kuwa gari hilo lilikuwa T 803 AHM Corrolla na kwamba yeye alikuwa akitokea Mbezi ya Kimara akienda kazini kwake eneo la Bunju kwa Baharia.
“Baada ya kuona wahuni wamejaa barabarani na hakuna sehemu ya kupita niliamua kwenda kuegesha gari kituo cha.polisi kwani niliàmini hiyo ni sehemu salama, niliwakuta askari niliwasalimu na kuegesha gari hapo,”alidai.
Alidai akiwa kazini kwake baada ya nusu saa alipata taarifa kwamba kituo cha polisi kimechomwa moto na alikwenda kuangalia usalama wa gari lake.
Shahidi huyo alidai akiwa njiani aliona barabara imewekwa mawe, magogo na moto uliochomwa kwa matairi ya gari na alifika katika kituo hicho cha polisi alikuta kinawaka moto.
“Gari langu lilivunjwa kioo cha mbele, nyuma, pembeni pia niliibiwa simu moja na radio ya gari,” alidai. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho