MOSCOW, URUSI -
WAZIRI wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema nchi hiyo imeanza kuweka kituo cha kudumu cha kijeshi nchini Syria, hatua ambayo imeidhinishwa na Baraza la Juu la Bunge la Urusi.
Hatua hiyo itajumuisha kukipanua kituo cha jeshi la majini cha Tartus ili kuweza kuwezesha meli 11 za kijeshi kutia nanga kwa wakati mmoja badala ya moja kama ilivyo sasa.
Kama sehemu ya makubaliano na Serikali ya Syria, Urusi pia itapewa fursa ya kudumu kutumia kituo cha jeshi la anga cha Hmeimim.
Urusi imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Rais wa Syria Bashar al-Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu nchini humo.