WASHINGTON, MAREKANI
URUSI na Marekani zimerushiana maneno makali katika mkutano wa Umoja wa Mataifa juzi, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kwa kutishia kuanzisha mapambano mapya ya kutengeneza silaha.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa mataifa hayo mawili kwa upande wake China imesisitiza kuwa haitojihusisha kwenye makubaliano yoyote mapya ya makombora.
Mapema mwezi huu, Marekani na Urusi zilisitisha mkataba unaozuia kutengeneza makombora ya masafa mafupi – INF, uliofikiwa wakati wa enzi ya vita baridi, baada ya kila mmoja kumlaumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo.
Urusi inasema Marekani inajiandaa kwa “mashindano ya kujirundukia silaha.” Marekani kwa upande wake inasema haitaki “kupakata mikono” wakati Moscow inaendelea kujiimarisha kijeshi.
Urusi imependekeza kuitishwa kikao cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Marekani kufanya jaribio la nyuklia na kufyatua kombora la masafa ya wastani mapema wiki hii.
Kombora hilo ni miongoni mwa yale ambayo yamepigwa marufuku kufanyiwa majaribio.