25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Urusi imeanza kuzalisha chanjo ya virusi vya corona

MOSCOW, URUSI 

URUSI imeanza kuzalisha chanjo ya virusi vya corona baada ya kugunduliwa hivi karibuni na taasisi ya Gamaleya.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Interfax, likinukuu wizara ya afya, Urusi inasema chanjo hiyo iliyogunduliwa na taasisi ya Gamaleya na kuwa ya kwanza kutengenezwa, itazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu.

Hata hivyo baadhi ya wanasayansi wanasema ipo hofu kwamba Urusi inaweza ikawa inaweka mbele kile kinachoonekana kama ufahari wa kitaifa kabla ya usalama. 

Katika hatua nyingine nchini Ujerumani kumekuwa na maambukizi mapya 1,415 katika kipindi cha masaa 24, na hivyo kufanya idadi jumla hadi sasa kufikia watu 222,828. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Taasisi ya magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch.

Juzi baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa hospitali nchini Madagascar zimekuwa zikikabiliana na ongezeko la maambukizi ya  Covid-19, huku rais wa nchi akiendelea kunadi dawa ya mitishamba anayodai ina uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Visa vya maambukizi vimeongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita katika kisiwa hicho, huku zaidi ya watu 13,000 wakiambukizwa virusi na wengine 162 kufariki kutokana na virusi vya corona, ambavyo vimesambaa karibu maeneo 22 ya nchi hiyo.

Licha ya ongezeka hilo la maambukizi, Rais Andry Rajoelina ameendelea kusimamia dawa hiyo ya kienyeji inayofahamika kama Covid-Organics, ambayo ilizinduliwa kwa kishindo mwezi Aprili.

Dawa hiyo ilitengenezwa na Taasisi ya Utafiti ya Madagascar kutokana na mmea wa artemisia – chanzo cha dawa inayotumiwa kutibu malaria – na mimea mingine kutoka Madagascar.

Kinywaji hicho kilinadiwa kama tiba ambayo inaweza kuzuia na kutibu corona miezi minne iliyopita na imekuwa ikitumiwa na watoto shuleni.

Watoto wa shule wamekua wakiombwa kutumia dawa hiyo ambayo haijathibitishwa kuwa tiba kuimarisha afya zao.

Mapema mwezi huu Rais Rajoelina alionekana akigawa dawa hiyo pamoja na bidhaa zingine muhimu kama vile mchele, mafuta na sukari kwa watu masikini katika mji mkuu, Antananarivo.

Rais Rajoelina alikosolewa vikali kwa kusababisha mkusanyiko wa watu wakati wa amri ya kutotoka nje lakini, mtazamo wake kuhusu janga la corona haijabadilika: 

“Janga hili halitachukua muda mrefu, ni wingu linalopita na tutaishinda.”

Pia alidai kuwa idadi ya watu walioambukizwa haikua juu katika mji mkuu ambako dawa hiyo ilikua imeanza kusambazwa miezi kadhaa iliyopita.

Shirika la Afya Duniani (WHO), inaunga mkono dawa za mitishamba lakini linataka uchunguzi wa kisayansi kufanyiwa dawa hizo kabla ya kuanza kutumiwa.

Kufikia sasa hakuna matokeo ya majaribio ya kimatibabu iliyotolewa kwa umma – japo hilo halijazuia dawa hiyo kutajwa kuwa chanzo cha fahari ya tiba asilia katika baadhi ya mataifa ya Afrika. 

Dawa hiyo imeagizwa na nchi kadhaa za Afrika

Serikali ya Madagascar imekua ikikabiliana na ukosoaji ndani na nje ya nchi kuhusu tiba hiyo ya mitishamba.

Hata hiyo watu wengi walio na virusi vya corona wanaanza kupona baada ya kupumzika kwa siku kadhaa- ni wale tu walio na changamoto zingine za kiafya walio katika hatari ya kupata ya kuzidiwa na maambukizi ya virusi.

Wizara ya Afya, imekuwa ikitoa wito wa kuzingatia uangalifu katika mpango huo – na kushauri hospitali kuwa Covid-Organic inaweza kumsaidia mgonjwa aliye na dalili kiasi na wala sio wale walio na magonjwa mengine kama kisukari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles