MOSCOW, URUSI
URUSI na China zimeulaani mkakati mpya wa usalama wa Marekani, ambao unalenga kukabiliana na mataifa hayo zaidi badala ya ugaidi.
Katika mkakati huo Marekani imeziainisha China na Urusi kuwa kitisho kikubwa zaidi kwake, ikiashiria kuachana na mkakati wa zaidi ya mwongo mmoja na nusu wa kukabiliana na wanamgambo wenye itikadi kali.
Moscow imeitaja sera hiyo ya Washington kuwa ‘ubabe usio na msingi’ na China ikisema ni ‘fikra ya enzi za vita baridi.’
Awali akiwasilisha mkakati huo mpya, ambao unabainisha vipaumbele vya Wizara ya Ulinzi ya Marekani kwa miaka kadhaa ijayo, Waziri wa Ulinzi Jim Mattis ameyaita China na Urusi kuwa ‘madola yanayobadili itikadi ya kisiasa’ yanayotafuta kuunda dola linalowiana na tawala zao za ‘mkono wa chuma.’
Mkakati wa usalama wa taifa, unawakilisha ishara ya karibuni ya dhamira ya utawala wa Rais Donald Trump kushughulikia changamoto za tishio la nguvu kutoka Urusi na China wakati huo huo akitaka kuboresha uhusiano nazo ili kuidhibiti Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.
“Tutaendelea kutekeleza kampeni dhidi ya ugaidi ambayo tunashiriki wakati huu, lakini ushindani wa kuimarisha nguvu yetu badala ya ugaidi, ndiyo kipaumbele cha usalama wetu wa taifa,” Mattis alisema katika hotuba wakati akiwasilisha waraka wa mkakati huo, wa kwanza wa aina yake tangu mwaka 2014.
Lakini akizungumza na waandishi wa habari juzi kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, alisema Marekani ilikuwa inatumia mkakati wa kibabe wa makabiliano.
“Inasikitisha kuona badala ya kuwa na majadiliano na  kutumia sheria za kimataifa, Marekani inajitahidi kudhihirisha uongozi wake kupitia mikakati na dhana za ukabilianaji,” alisema Lavrov na kuongeza kuwa Urusi iko tayari kwa mazungumzo na majadiliano kuhusu kanuni za kijeshi.
Ubalozi wa China nchini Marekani ilikosoa mkakati huo, ukisema Beijing inataka “ushikiano wa kimataifa” na si ‘udhibiti wa dunia.’
“Iwapo baadhi ya watu wanaiangalia dunia kupitia vita baridi, basi hatma yao ni kuangalia tu migogoro na makabiliano,” alisema msemaji wa ubalozi huo katika taarifa.