24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘UREMBO HUPONZA WANAWAKE KUPATA SARATANI’ – DAKTARI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Crispin Kahesa, amewashauri wanawake kuhakikisha wananyonyesha watoto kulingana na jinsi inavyoshauriwa na wataalamu wa lishe.

Dk. Kahesa alitoa ushauri huo hivi karibuni, alipozungumza na MTANZANIA Jumamosi katika mahojiano maalumu kuhusu saratani ya matiti, ambapo alisema miaka ya karibuni imeibuka tabia kwa baadhi ya wanawake kukwepa jukumu hilo.

“Matiti kwa mwanamke pamoja na kwamba hutengeneza maziwa ambayo ni chakula cha mtoto, pia ni sehemu ya mwili ambayo wengi huitumia kama urembo kwa ajili ya kuongeza mvuto.

“Kutokana na hali hiyo, wapo ambao hukwepa kunyonyesha kwa hofu ya kupoteza ule mvuto walionao, lakini niwaambie wazi kwamba, kitendo hicho kinawaweka kwenye hatari ya kupata saratani ya matiti baadaye kwenye maisha yao,” alisema.

Daktari huyo alisema kila mwaka katika taasisi hiyo hupokea wagonjwa wapya wapatao 5,500 ambapo kati yao, 700 huwa wana saratani ya matiti.

“Hiyo ni sawa na asilimia 12 ya wagonjwa wote tunaowapokea, wengi huja ugonjwa ukiwa katika hatua ya tatu na nne ambazo ni hatari zaidi na huwa ni vigumu kupona,” alibainisha.

Alisema ingawa wanaume nao huweza kupata saratani hiyo, hata hivyo hatari ipo kwa wanawake zaidi.

“Kibailojia mwanamke ana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti kuliko mwanamume, kwani ana kiwango kikubwa cha homoni ya Oestrojeni,” alisema.

Aliongeza: “Huwa tunapokea wanamume saba hadi wanane kila mwaka ambao wanaugua saratani hii, nadhani kwa sababu pia hawana mwamko wa kuja kupima.”

Daktari huyo alisema jamii bado haina uelewa wa kutosha juu ya ugonjwa huo na ndiyo maana mwezi Oktoba ulitengwa kuwa mwezi wa kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa huo.

“Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wananchi, wajitokeze kwa wingi siku ya Jumamosi (Oktoba 28, mwaka huu) ambapo hapa Ocean Road tutafanya matembezi ya hisani na upimaji bure kwa wote,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles