25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JAFFO AFAGILIA MCHANGO WA SHULE BINAFSI

Na MWANDISHI WETU, MWANZA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, amesifu mchango wa shule binafsi kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuiinua sekta ya elimu hapa nchini.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa siku moja wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (TAPIE).

Alisema mchango wa shule hizo umesaidia  kuifanya Tanzania ionekane kuwa iko katika hali nzuri kielimu kwa kutoa vijana waliofuzu kimasomo na kuwa na uwezo kuiwakilisha katika mikutano mbalimbali ya nchi za nje.

Mkutano huo wa siku moja ulikuwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha sekta ya elimu kwa kuwaleta pamoja wawekezaji na wamiliki wa shule binafsi kuwa na jukwaa la mijadala na midahalo kuhusu uendeshaji wa shule na maslahi ya jamii nzima.

“Kwa kweli shule binafsi zimekuwa zikisaidia kwa kiwango kikubwa katika kuinua elimu ya nchi yetu kwa kutoa vijana waliofuzu vizuri kimasomo na kuipatia sifa Tanzania, ingawa mnafanya vizuri, niwaombe muwe waaminifu katika kipindi hiki cha mitihani ya kidato cha nne inayotarajia kuanza hivi karibuni,” alisema.

Naye Rais wa TAPIE, Ester Mahawe, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), alisema Serikali na wananchi kwa ujumla watambue taasisi hiyo ni chombo kinachowapatia fursa wamiliki kuwa sehemu ya uandaaji wa sera, miongozo na sheria za kuendeshea, kuwa kiungo muhimu na mshiriki wa kuisaidia serikali katika kuongeza fursa ya elimu kwa vijana wa Kitanzania na uboreshaji wa utoaji wa elimu hapa nchini.

“TAPIE  inahakikisha maslahi ya wamiliki wa shule binafsi hapa nchini yanalindwa na kutetewa katika ngazi na idara zote za serikali na ikumbukwe changamoto za uwekezaji katika sekta ya elimu ni nyingi sana, kuanzia umiliki wa ardhi, kodi na tozo mbalimbali,” alisema na kuongeza:

“Sheria na miongozo isiyo rafiki kwa wamiliki, gharama za wafanyakazi, mikopo yenye riba kubwa nk, hivyo kwa sasa tunahitaji chombo chenye maono na dhamira ya dhati ili kuona mitaji yetu na nguvu zetu zinazotumika zinakuwa na tija na zinalindwa kimfumo,” alisema Mahawe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles