22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Urais CCM wafukua mazito

picNa Waandishi wetu

IDADI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotangaza nia ya kuwania urais imezidi kuongezeka, huku kila mmoja akifukua mambo mazito.
Hatua hiyo, imekuja baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani jana kutangaza rasmi kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Makada hao, wanaungana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Charles Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Balozi Amina Salum Ali na Balozi Ali Karume waliotangulia kutangaza nia.

SUMAYE
Akitangaza nia yake jijini Dar es Salaam jana, Sumaye alisema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha anawafunga walarushwa, mafisadi na wahujumu uchumi kwa sababu wanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Alisema vitendo vya rushwa vinawanyima haki wananchi masikini, hivyo vinapaswa kusimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha vinaondoka.
“Hata enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikemea sana vitendo vya rushwa kwa sababu ni sawa na kuhujumu uchumi… nikichaguliwa nitawashughulikia kwa sababu mimi ni rais, nina uwezo wa kuwachukulia hatua watu hawa… si rais bwana, mimi ni mkubwa kuliko wote, nitakuwa na uwezo kufanya uamuzi,” alisema Sumaye.
Alisema kutokana na hali hiyo, watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria ili kuhakikisha haki inatendeka.
Sumaye alisema baadhi ya watu waliotangaza nia wengine wapo madarakani, lakini anashangaa wameshindwa kuchukua hatua yoyote ya kupambana na vitendo hivyo.
Bila kuwataja majina, Sumaye alisema kibaya zaidi watu hao wamekuwa wakiwadanganya wananchi kuwa watalishughulikia suala hilo.
“Nimeshangaa kuwasikia baadhi ya watangaza nia eti kuwa watashughulikia rushwa, mpaka sasa bado wapo madarakani, hivi wana nia njema kweli au wamegeuza fasheni ili kila mmoja aseme? Tunapaswa kuwaangalia usoni na kuwapima kama wana nia hiyo au,” alisema.
Alisema akifanikiwa kuingia madarakani, atahakikisha anaunda kamati maalumu ya kuchunguza mienendo ya rushwa na kuanzisha mahakama maalumu zitakazoshughulikia vitendo vya rushwa.
“Atakayehukumiwa kwa bakora atapigwa, mwenye kupelekwa jela atakwenda, lakini nitahakikisha walarushwa, mafisadi, wahujumu uchumi wanashughulikiwa ipasavyo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, ataweza kupambana na uovu wa aina yoyote ambao ni kikwazo cha maendeleo.

MUUNGANO
Kuhusu Muungano ambao umekuwa ukitikiswa na nyufa nyingi, Sumaye alisema unapaswa kudumishwa na kulindwa kwa masilahi ya Watanzania wote.

UCHUMI
Kwa upande wa uchumi, alisema katika kipindi cha utawala wake kama akiingia madarakani, atahakikisha unaimarika ili wananchi waondoke kwenye dimbwi la umasikini.
Alisema atashirikiana na wananchi ili kuinua sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na ujasiriamali, kuhakikisha vinakua kwa kasi na kuwawezesha wananchi kuwa na uchumi wa kipato cha kati.
Sumaye alisema licha ya sasa takwimu kuonyesha uchumi unakua, hali ya wananchi bado ni duni.
“Zaidi ya asilimia 70 ya wananchi ni wakulima na wafugaji, jambo ambalo limechangia mpaka sasa wengi wao kuendelea kuwa masikini, tunapaswa kuwa na mbinu ambazo zitasaidia kuwaondoa kwenye umasikini huo,” alisema.
Alisema atahakikisha hilo linafanikiwa kwa kutengeneza sera ambayo italeta ushirikiano baina ya wananchi, Serikali na sekta binafsi.
Sumaye alisema kutokana na hali hiyo, Serikali yake itatoa kipaumbele kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa za ndani iwe kwa matumizi ya chakula au mengineyo ili kuhakikisha wanapata masoko ndani na nje ya nchi.

VIWANDA
Akizungumzia kuhusu sekta ya viwanda, alisema atafufua viwanda vyote vilivyokufa na kujenga vipya ili viweze kutoa ajira kwa wananchi.
“Ikiwa viwanda vitafufuliwa, vitasaidia kutoa ajira jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza malalamiko ya ukosefu wa ajira nchini,” alisema.
Sumaye alisema bidhaa zitakazozalishwa nchini zitatengenezwa kwa ubora unaokubalika ili ziweze kupata masoko ndani na nje ya nchi.
Alisema nchi zenye viwanda ndizo zinazoongoza kwa utajiri na maendeleo duniani kote, hivyo kutokana na hali hiyo atatafuta wataalamu wa kutosha ambao watatumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji mali, rasilimali watu na ujuzi.

AJIRA
Sumaye alisema ajira kwa vijana ni tatizo kubwa, hivyo basi kufufuliwa kwa viwanda kutasaidia kuongeza ajira.

MIUNDOMBINU
Alisema ataboresha miundombinu ya barabara ili kuhakikisha shughuli za uchumi zinakwenda sawa na kwamba bidhaa zitakazozalishwa nchini zitasafirishwa ndani na nje ya nchi.

HUDUMA ZA JAMII
Sumaye alisema atasimamia kwa umakini huduma za jamii katika nyanja mbalimbali ya maji, elimu na afya.
Alisema ataboresha shule za sekondari za Serikali ili ziweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye vipaji maalumu.
Sumaye alisema katika kipindi chake hakutakuwa na shule ya binafsi itayofutwa na Serikali kwa sababu kufanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, Serikali yake itaongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa asilimia 20 ya bajeti mzima, jambo ambalo litasaidia kuongeza uwajibikaji.
Alisema mitaaala ya elimu itaangaliwa upya ili kuondoa mfumo wa zamani na kuingia kwenye mfumo wa mabadiliko unaozingatia maarifa.
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema atahakikisha huduma ya afya inatolewa kwa ubora zaidi ili kupunguza idadi ya watu wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Sumaye alisema vituo vya matibabu vitaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa tiba ili wananchi waweze kupata huduma stahiki.
Kwa upande wa sekta ya maji, alisema atahakikisha wananchi wa mijini na vijijini wanapata huduma hiyo bila matatizo yoyote.

DAWA ZA KULEVYA
Alisema Serikali yake haitafumbia macho biashara ya dawa za kulevya inayofanywa na baadhi ya watu wazito ama kwa fedha zao au kwa madaraka yao.
“Cha kushangaza, wenye biashara hawaendi kuleta, bali wanawatuma watu ili waweze kwenda kuchukua na kuja kuuza nchini, watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

BENKI YA NBC
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu uuzwaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC), kashfa ya rada, ndege ya rais na mengineyo, Sumaye alionekana kupata wakati mgumu.
Alijitetea kwa kusema wakati akiwa Waziri Mkuu, alifuata taratibu zote za kisheria za kufanya ununuzi na uuzaji wa hisa za NBC.
“Serikali ya awamu ya tatu ilifuata taratibu zote za kisheria wakati wa ubinafsishaji wa Benki ya NBC kwa sababu ilikuwa ikijiendesha kwa hasara,” alisema.
Alisema baada ya kubinafsisha, wanahisa walikuwa wanalipa kodi kiasi kikubwa tofauti na hapo awali, taarifa ambazo zilikuwa zinapatikana Benki Kuu (BoT).
Sumaye alisema benki hiyo haikuuzwa yote kama wananchi wanavyodhani, bali waliuza na kubakisha asilimia 30 ya hisa.

RADA
Akizungumzia kuhusu suala la rada ya Serikali, alisema uamuzi wa kuinunua ulitokana na baadhi ya makampuni ya ndege kutoka nje ya nchi kusitisha safari zao nchini kutokana na ukosefu wa rada.
“Nchi ilikuwa haina rada, huku baadhi ya makampuni ya kigeni yalianza kukataza ndege zake zisije nchini, jambo ambalo lilitufanya kufikia uamuzi wa kuinunua ili iweze kuwasaidia waongoza ndege,” alisema.
Alisema katika kipindi hicho, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliponea chupuchupu kugongana na ndege nyingine kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), jambo ambalo liliwafanya wachukue uamuzi huo.
Sumaye alisema tatizo si kununua rada, bali kama kuna watu walifanya makosa hao ndio wanapaswa kuadhibiwa.

RUSHWA CCM
Akizungumzia kuhusu rushwa ndani ya CCM, alisema ikiwa chama hicho kitapitisha jina la mgombea wa nafasi hiyo mlarushwa atakihama.
“Nimeanza kukemea rushwa ndani ya chama muda mrefu na kuonyesha msimamo wangu wa kuwa ninaichukia…, ikiwa litapitishwa jina la mlarushwa, nitahama chama, lakini ninaamini hawawezi kufanya hivyo,” alisema.

KUMILIKI ARDHI
Akizungumzia kashfa ya kumiliki ardhi eneo kubwa bila ya kulitumia, Sumaye alisema hadi sasa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshindwa kumpa hati ya umiliki wa ardhi, jambo ambalo linamfanya ashindwe kuliendeleza.

NYUMBA
Akizungumzia kuhusu uuzaji wa nyumba za Serikali, alisema uamuzi huo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya tatu.
Alisema baada ya kufikia mwafaka, waliunda tume tatu ambapo moja iliongozwa na Basil Mramba na Msekena ili kufanya tathmini ya nyumba hizo na gharama za ukarabati.
“Tume hizo zilipomaliza kazi tu, walipokea mapendekezo ya kuitaka Serikali kuuza nyumba hizo kwa wananchi waliokuwa wamekaa huku ikitoa masharti ya kutoziuza kwa miaka 25,” alisema Sumaye.

KIFO CHA NYERERE
Alisema hatasahau kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14, 1999.
Sumaye alisema kutokana na msiba huo hakulala kwa siku tatu mfululizo kutokana na kubanwa na majukumu usiku na mchana.

Dk.Kamani: Nitakuwa mkali kwa rushwa

Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Kamani, alitangaza nia hiyo jana jijini Mwanza, ambapo alisema kuwa ikiwata atafanikiwa atahakikisha anakuwa mkali katika kupambana na rushwa kwa vitendo na sio kwa maneno.
Alisema mambo atakayosimamia ni kuhakikisha anaondoa rushwa kwa kuimarisha uwezo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) pamoja na kumpa nguvu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Nitakuwa mkali kwa wala rushwa na wale wote wanaodokoa mali za Serikali, wananchi wanakosa imani na serikali inapoacha rushwa kutamba kila kona, sitakuwa na huruma na wala rushwa na watoa rushwa,”.
UKAGUZI HESABU ZA SERIKALI
Akizungumzia ufisadi unaobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema kuwa ofisi hiyo ndio jicho la Serikali hivyo atahakikisha inawezeshwa ili iweze kutekelez amajukumu yake ipasavyo.
Alisema kuwa ofisi ya CAG inapaswa itanue wigo wake zaidi na kufanya ukaguzi katika taasisi binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuwa baadhi yao yamekuwa yakitumia mwanya kupora fedha za wahisani.
MUUNGANO NA DIPLOMASIA
Alisema kuwa akifanikiwa kuwa Rais wa awamu ya tano atahakikisha anaulinda muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa manufaa ya watanzania na hatakuwa na mchezo kwa wale wote ambao watauchezea muungano uliopo wa Tanzania Bara na Zanzibar.
UTAWALA BORA
Akizungumzia utawala bora, alisema kuwa atahakikisha wataalamu waliokabidhiwa majukumu yao wanafanya kazi kwa weledi na kwa haraka badala ya kusubiri vikao kwani vikao hivyo vimekuwa vikisababisha usumbufu kwa wananchi.
SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alisema kuwa ili taifa lipige hatua lazima liandae wataalamu watakaobobea katika Sayansi na Teknolojia hivyo atahakikisha anatilia mkazo kwa wanafunzi kuzingatia masomo ya sayansi na kuwajengea uwezo wa kupata vitendea kazi.
NISHATI NA MADINI
Dk. Kamani alisema atahakikisha wachimbaji wadogo wanapewa kipaumbele kwa kuwajengea mazingira mazuri ambayo yatawawezesha kukopeshwa katika benki za biashara na kuhakikisha madini yanayopatikana hapa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi kama madini ghafi hali ambayo imesababisha serikali kupoteza mapato.
UWEKEZAJI
Kuhusu uwekezaji Dk. Kamani alisema kuwa atahakikisha anasimamia kikamilifu mazingira bora ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa kuweka muda mchache wa upatikanaji wa vibali vya uwekezaji na kuondoa mlolongo wa upatikanaji wa vibali.
MIFUGO NA UVUVI
Alisema kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo, bado mifugo hiyo naijamnufaisha mtanzania kwa kuwa mifugo imekuwa ikifugwa pasipo kuzingatia utaalamu huku wafugaji wakiuza mifugo na mazao yake kama malighafi.
GESI NA MAFUTA.
Alisema kuwa atahakikisha serikali inasimamia kikamilifu raslimali za gesi na mafuta ili ziweze kuwanufaisha watanzania kwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha utajiri kwa Taifa kutokana na fedha zitakazopatikana.
AJIRA KWA VIJANA.
Dk. Kamani alisema kuwa atahakikisha anaanzisha kitengo cha ugunduzi wa ajira ili kiweze kuwasaidia vijana kuweza kupata ajira ili waweze kuondokana na ukosefu wa ajira ambao umekuwa ukitishia usalama wa nchi.
VIWANDA NA BIASHARA
Waziri Kamani alisema iwapo atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania Serikali yake itaimarisha uchumi kwa kujenga viwanda vingi, vikiwemo vya nguo, nyuzi, nyama na maziwa ili kupanua ongezeko la ajira kwa vijana.
VIGOGO WALIOMSINDIKIZA
Hata hivyo baadhi ya vigogo kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) walijitosa kumuunga mkono Dk Kamani wakati akitangaza nia yake ya kuwania urais wa wamu ya tano.
Waliojitokeza kumsindikiza ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira ya Bunge, James Lembeli, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), James Musalika, Jacob Shibiliti, Deusdedit Mtambalike pamoja na John Mahewa.

…Profesa Muhongo na uchumi wa gesi

Mbunge wa kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema atainua uchumi wa Tanzania na kusimamia rasilimali ya gesi asili endapo atapitishwa na CCM kuwa mgombea urais.
Profesa Muhongo, alitoa kauli hiyo kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT), tawi la mjini Musoma jana wakati akitangaza rasmi nia ya kugombea urais.
Alisema kwa muda ambao amekuwa Waziri wa Nishati na Madini, amekuja na suluhisho la umasikini kutokana na Tanzania kuwa na rasilimali nyingi.
“Nimekuja hapa si kufanya kampeni ya urais, bali niko mbele yenu kwa niaba ya wananchi kuomba ridhaa yenu ya kuomba urais… sikuja kumsema au kumshambulia mtu kwani hata tukilumbana umasikini utaendelea kubaki palepale.
“Nimekuja na suluhisho la umasikini, tangu uhuru tumekuwa na tatizo la ujinga, maradhi na umasikini, kwa utajiri wa rasilimali zilizopo umefika wakati wa kuondokana na tatizo hili,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema nchi inakabiliwa na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, rushwa, siasa kutawala kila mahali, uonevu, dhuluma, uvivu na viongozi wengi kushindwa kujiamini.
Profesa Muhongo alisema matatizo mengine ni upungufu wa takwimu sahihi, kupungukiwa na ushindani katika taifa, masoko na ajira pamoja na dalili za kupungua kwa amani, upendo na mshikamano.
“Matatizo haya yote yanaweza kutatuliwa endapo tutakuwa na uchumi imara ambao utatokana na rasilimali tulizonazo, hasa gesi asilia ikisimamiwa na mtu mzalendo, mwaminifu na mwadilifu ambaye ni mimi.
“Ningependa kulinganisha uchumi wetu na nchi zilizoendelea kama India, China na Brazil na sipendi tujilinganishe na nchi za Kenya na Uganda… kwani sisi sote bado ni masikini,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema pato la uchumi kwa mwaka katika nchi ya India ni dola za Marekani bilioni 11.2, China ni trilioni 10.2 na Brazil ni trilioni 2.4, huku Kenya ikiwa ni dola bilioni 61 na Tanzania bilioni 48.
Profesa Muhongo alisema dira ya maendeleo hadi kufikia mwaka 2025, ni kutoka kwenye pato la mtu mmoja mmoja la dola 1,006 hadi 4,084 jambo ambalo linawezekana endapo rasilimali ya gesi itatumika vizuri.
“Wengi wanakuwa na hofu kuwa ni jambo ambalo haliwezekani, naamini naweza na ndiyo sababu sijaanza kusema nitawapa mishahara mikubwa au kuwajengea shule, natakiwa nikupe uchumi imara kwanza ndiyo yote yanawezekana.
“Wengi watajiuliza fedha za kutokomeza umasikini tutapata wapi, tutatumia rasilimali zetu kwani kwa upande wa madini tumechimba asilimia 10 tu na tayari tumegundua gesi asilia futi za ujazo trilioni 56 ambazo ni sawa na mapipa ya mafuta bilioni 10…. huu ni mtaji mkubwa ambao unahitaji kusimamiwa na wa kusimamia ni mimi pekee,” alisema.
Profesa Muhongo alisema uchumi wa gesi utaweza kuzalisha viwanda vitakavyoweza kuleta ajira hali itakayosababisha kutokomeza umasikini nchini.
Alisema yeye ni mwanachama mkongwe ambaye alijiunga na Chama cha TANU mwaka 1973, alipokuwa katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mwasisi wa CCM mwaka 1977.
“Mimi ni mwanachama mkongwe, kadi yangu ya TANU niliyoipata mwaka 1973 na risiti yake hii hapa… kadi yangu ya CCM niliyochukuwa wakati nipo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na risiti yake hii hapa… kama nimeweza nimevitunza hivi vitu kwa kipindi chote hicho, hata rasilimali zenu nitaweza kuzitunza.
“Wana CCM na wananchi wengine msio wana CCM, nawaomba mnipe ridhaa kwani kama ujuzi ninao, uzoefu ninao, ninajua vyanzo vyote vya kupata fedha, nisichokuwa nacho kwa sasa ni ridhaa yenu tu,” alisema Profesa Muhongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles