23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Urais CCM ni mgumu

coverSHABANI MATUTU NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM
MCHAKATO wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umekuwa mgumu kutokana na chama hicho kutangaza hatua sita muhimu za kumpata kada atakayepeperusha bendera yao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Inaelezwa utaratibu huo huenda ukawa kizingiti kwa baadhi ya wagombea kujikuta wakitupwa nje hatua za awali za mchujo kwa majina yao kushindwa kufika katika vikao vya uamuzi kwa mujibu wa kanuni za chama hicho.
Hatua hizo zilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye alipokuwa akizungumza na wahariri wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd katika ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari.
Nape alizitaja hatua hizo sita ambazo kila mgombea atakayeomba kuteuliwa na chama hicho ni lazima apite, kuwa ni vikao vya Sekretarieti, Kamati Ndogo ya Maadili, Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu wa Taifa.
Kutokana na hatua hizo, alisema iwapo kuna mgombea ataondolewa katika mchujo huo asimbebeshe lawama kiongozi yeyote, ila anatakiwa kujitafakari kwa kutumia Katiba ya CCM, kanuni za uchaguzi na sheria za chama.
Nape alisema mlolongo mzima wa uteuzi wa mgombea utafuata taratibu zote na atakayekubalika na mfumo huo hakuna atakayemzuia.

WAGOMBEA WACHANGA

Akizungumzia wagombea wachanga kujitosa kwenye mbio za urais, Nape alisema ili mtu aweze kuteuliwa na chama ni lazima awe anatambulika na si mgombea mchanga kama wengine wanavyofikiria.
Alisema kutokana na hali hiyo, CCM haiwezi kuokota wanachama wake kutoka mtaani, bali huangalia sifa na historia ya mgombea ndani ya chama.
“Ni vigumu kwa mgombea kuweka matofali ili aongeze urefu aweze kutosha, bali kitakachoangaliwa ni sifa stahili kwa mgombea anayetafutwa kwa kuwa tunaamini ndiye anatarajiwa kuwa mwenyekiti wetu wa chama, hivyo haiwezekani kuwa na mwanachama wa miaka mitatu halafu aombe nafasi ya kugombea urais tumpe.
“Na huyu ni lazima ajiulize je, anatosha kwenye nafasi ya urais na kutosha kuwa mwenyekiti wa chama chetu? Kila mahali kuna kanuni zake, huwezi kusilimu leo na kuwa sheikh, hili kwetu CCM halipo na kama kuna watu wana fikra za aina hii wanajidanganya,” alisema Nape.

RATIBA YA UTEUZI

Akizungumzia kuhusu ratiba ya uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM, Nape alisema kuna uwezekano mkubwa wa ratiba za uteuzi wa vikao vya chama kusogezwa mbele kutokana na kuingiliana na ratiba za vikao vya Bunge la Bajeti linalotarajiwa kufanyika kuanzia Aprili hadi Juni.
Alisema mbali ya hili, ratiba hizo za CCM pia zimeingiliana na mchakato wa kura ya maoni ya kupata Katiba Mpya unaotarajiwa kufanyika Aprili 30.
“Nimesema kuna uwezekano, sina uhakika. Lakini nadhani ndiyo maana Kamati Kuu iliyokaa Zanzibar haikutoa ratiba ya mchakato wa uteuzi ndani ya chama na ikasema inatoa ratiba ya shughuli za kawaida halafu hii ya mchakato ndani ya chama itafanyika baadaye,” alisema.
Pamoja na hatua hiyo, aliviomba vyombo vya habari kukisaidia chama hicho kushusha joto la kisiasa ambalo alisema linatarajiwa kuwa kubwa ndani na nje ya chama hicho hasa kuelekea katika uteuzi wa mgombea urais.
“Iwapo mtapewa jambo hakikisheni mnaripoti vizuri kwa kujiridhisha ili kupunguza joto linalopanda hivi sasa, hivyo mnatakiwa kuchambua taarifa mnazopewa kwani nyingine huwa na nia ya kuchochea,” alisema.
Alisema ushindani wa ndani unakuwa mkubwa zaidi kuliko wa nje, na hilo linaweza kuwa na sababu nyingi, lakini kubwa ni kwamba mgombea wa urais atakayeteuliwa kutoka CCM ndiye atakuwa rais wa awamu ya tano.
“Kwa vyovyote vile wadau wote watakuwa wanaangalia kwa macho yote mchakato wa ndani ya chama na hao watahusisha wadau wa ndani ya chama na nje ya chama, lakini hata wadau wengine duniani kutokana na ukweli kwamba wapo waliowekeza matrilioni ya fedha katika gesi, hao watakuwa makini kuona mchakato unakwendaje na utaathiri vipi uwekezaji wao,” alisema.
Nape alirejea kauli yake kuwa anaamini bila wapinzani CCM ingekufa, kwa kuwa wamesaidia kuwakumbusha na kuwarekebisha katika mambo mengi ambayo baada ya kurekebisha wamefanikiwa.

CCM KUPENDELEWA NA DOLA

Akizungumzia malalamiko ambayo yamekuwapo kwa muda mrefu kuhusu suala la CCM kutegemea kubebwa na dola, alisema limekuwa gumu kubadilika kutokana na suala hilo kuathiriwa na historia.
“Historia ni ngumu kubadilika sasa, labda kesho kwa sababu kabla ya mfumo wa vyama vingi CCM ilikuwa kila mahali, hivyo ukilinganisha muda tulionao kutoka mfumo wa vyama vingi, ni vigumu kubadili mara moja alama za CCM.
“Nimekuwa nikipambana na vyombo vya dola kwenye shughuli zetu za chama na hata kuwaambia kwamba hiyo si shughuli ya Serikali, lakini wamekuwa hawanielewi kwa kuwa ni vigumu sana kwao kutenganisha hilo, unakwenda kwenye sherehe za chama wao ndio wanataka kukagua jukwaa, mimi nawaambia tupisheni, lakini tunagombana sana wakiniita mkorofi.
“Wanapenda kuonekana wao pale mbele, lakini nawazuia na kuwaambia kwamba ile ni shughuli ya chama na tunafikia mahali wanakataa na kusema kuwa ‘huyu ni rais akidhurika wewe utajibu’, lakini nakataa na kuwaeleza kuwa pamoja na urais wake huyu ni mwenyekiti wetu wa chama,” alisema Nape.
Alisema CCM hailewi na kupendelewa na dola kwa kuwa wao ni miongoni mwa makada wanaokerwa na dola inayotengenezwa ndani ya chama hicho kwa kuwa haivumilii.
“Mimi ni miongoni mwa watu tunaochora mstari wa kukataa dola kuingilia shughuli za chama, sijui hatua hiyo itakwenda hadi wapi ila ninachokifanya ni kupambana nikishirikiana na Katibu Mkuu Kinana.
“Kama tungekuwa tunatumia dola vibaya mimi na Katibu Mkuu wangu tusingekuwa tunalala katika nyumba za wageni za kawaida katika ziara, lakini tunafanya hivyo kwa sababu ya kuondoa matumizi ya dola tukiamini kuwa ni salama ya CCM, lakini pia tusisahau siku CCM ikitoka hivyo hivyo ndivyo vitawahudumia watakaoshinda,” alisema.
Alisema viongozi wa chama hicho wamekuwa hawakubali kulemazwa na dola na ndiyo sababu Katibu Mkuu wake, Kinana anapopanda ndege au treni ya Serikali huwa analipia.

CHAMA KUPASUKA

Nape alisema chama hicho hakiwezi kupasuka kutokana na watu kutoelewana kwa sababu ya kugombea nafasi na kuwa wanaosema wakikatwa wataondoka kwenye chama hicho, watajikuta wakiondoka wao, wake zao na watoto wao.
“Watu wengi wanasema CCM mwaka huu itapasuka, mimi nawaambia tutakwenda kwenye mchakato wa kusaka mgombea urais na tutatoka tukiwa kitu kimoja.
“CCM kupasuka kwake si kirahisi hivyo kama ambavyo watu wanakuona leo, nimeangalia 1995, nimeangalia mwaka 2005, joto lilikuwa namna hii, watu wanasema kitapasuka, asipoteuliwa fulani kitapasuka… tutafanya hivi, lakini mwisho wa siku tunatoka tukiwa kitu kimoja,” alisema Nape.
Alisema katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, hakuna aliyedhani kuwa Waziri wa Uchukuzi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kama angeweza kukaa meza moja na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, lakini viongozi hao walikaa pamoja na kukubaliana mmoja akawa mwenyekiti wa Bunge la Katiba na mwingine Kamati ya Uandishi wa Katiba.
“Na wale wana tofauti zao, mwingine Magharibi na mwingine Mashariki, na wamefanya kazi pamoja Katiba imepatikana, watu walidhani hawa watu hata kusalimiana hawasalimiani, watu wengine walidhani kambi za urais zingeharibu Bunge la Katiba, mahali ambapo hata kura moja ilikuwa muhimu,” alisema.
Nape alisema kutokana na mtizamo huohuo, CCM bado itaishangaza dunia.
Alisema suala siyo nani kuwa mgombea, ila suala la muhimu ni mfumo wa chama.
“Naendelea kusema mwaka 2015 CCM itashangaza watu katika ushindi wake na kuwa wamoja wenye mshikamano, tofauti na watu wanavyodhani. Kama kuna mgombea anafikiria kwa sababu ya kukatwa atatoka, atatoka yeye na mke wake na watoto wake, hawa wote wanaomzunguka ikifika mahali dakika moja wanageuka.
“Kupasuka hampasuki kwa sababu ya kugombania nafasi, chama kinapasuka kwa sababu ya tofauti za kiitikadi, ndani mnafika mahali mnashindwa kuelewana kwa ‘principal’, watu watatoka lakini siyo nafasi, mimi nina uhakika gani kwamba nikitoka na wewe tukienda huko nitapata ninachotaka?
“Mkipishana misingi chama kitapasuka, nimeona wengi walitoka wakafikiri wataondoka na watu, leo wamerudi, mpasuko uliozaa Chadema ulikuwa ni mpasuko wa imani, walishindwa kuelewana Mtei (Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei) na Mwalimu (Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere),” alisema Nape.

KUHUSISHWA NA MEMBE

Nape alisema hana mgombea na kwamba kwa nafasi yake kazi yake ni kujenga chama ili atakayekuja akiendeleze.
Alisema watu wanamuhusisha na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, huku wakisahau kuwa yeye na kiongozi huyo ni kama ndugu yake na wanatoka eneo moja mkoani Lindi.
“Mimi sina mgombea, kazi yangu na Kinana (Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana) ni kuchonga mtumbwi watakaokuja kuutumia hao watakaokuja, tukiuchonga kwa kumwangalia Nape, anaweza kuja mkubwa zaidi ya Nape.
“Mimi ni refa, nikiamua kuwa mgombea lazima nijiuzulu nafasi yangu kwanza, na siku zote mimi nikisema nakuunga mkono, nakuunga kweli, kama sikuungi, sikuungi,” alisema Nape.
Alisema hali hiyo ya kila mtu kufanya kazi yake ndiyo itakayoifanya CCM isipasuke.
“Katibu Mkuu wewe refa usibebe mtu, Nape refa usibebe mtu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles