NA MWANDISHI WETU
MFALME wa Masauti Bongo, Christian Bella ‘Obama’, yupo mbioni kuachia wimbo mpya wa mapenzi ambao utazinduliwa rasmi siku ya wapendanao ‘Valentine Day’ kwenye Ukumbi wa Dar Live.
Akizungumza na gazeti hili, Bella ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), alisema ameamua kutoka kivingine baada ya kutoa wimbo wa Nani Kama Mama na kufanya vizuri katika soko la muziki wa dansi.
“Nilifurahishwa na mapokezi ya wimbo wangu wa Nani Kama Mama pamoja na nyimbo nyingine za mapenzi kama vile Nakuhitaji, Msaliti, Hanitaki Tena, Safari Siyo Kifo na nyingine nyingi hivyo mashabiki wangu wakae tayari kupata kitu kipya,” alisema Bella.
Mbali na kutambulisha wimbo huo mpya ambao ni maalumu kwa wapendanao, Bella pia atawapa burudani mashabiki wake ambapo ataimba kwa kutumia vyombo ‘live’ nyimbo zake zilizowahi kutamba.
Mfalme wa muziki wa taarabu, Mzee Yussuf na kundi lake la Jahazi Modern Taarab, litatumbuiza usiku huo wa wapendanao ambao pia watapata nafasi ya kupiga picha na mastaa hao.