Elizabeth Hombo, Dodoma
Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni, wamewataka viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Kanisa Katoliki, kutoijibu serikali kuhusu barua waliyopewa na Msajili wa Vyama ya kukanusha waraka wao.
Akizugumza na waandishi wa habari kwa niaba ya kambi hiyo leo jijini Dodoma, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia amesema mamlaka za nyaraka za makanisa hayo ni mamlaka ya kibiblia.
Amesema makanisa hayo makubwa nchini yamekuwa yakitoa huduma kubwa katika jamii hivyo kwa jambo lililofanywa na msajili wa vyama kisaikolojia wamedharauliwa.
“Sisi tunawashauri viongozi hawa wa dini kutowajibu serikali halafu tuone wanachukua hatua gani,” amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Kibamba, John Mnyika amesema serikali inapaswa kukanusha barua hiyo na kwamba jambo hilo halitakwisha watatumia kanuni za bunge ndani siku 10 kuomba miongozo hadi pale serikali itakapotoa majibu.
“Naibu Spika ametumia madaraka vibaya kwa kumkingia Waziri Mkuu asilijibu hili bungeni. Jambo hili haliwezi kuisha leo katika siku hizi 10 tutahakikisha tutauliza maswali, kuomba miongozo hadi serikali itakapowajibika na tutalifanya kwa umoja wetu hadi haki ya viongozi hawa ipatikane,” amesema Mnyika.