26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

MILANGO YA FAHAMU INAVYOPATA AJALI, KUATHIRI MWILI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


KILA mwanadamu ameumbwa na milango ya fahamu, milango ya fahamu ambayo inaonekana kwa nje ya mwili wake ipo mitano.

Ambayo ni pua, macho, sikio, ngozi na ulimi (mdomo). Hii hufanya kazi ya kupeleka taarifa kwenye ubongo kwa njia mbalimbali.

Ngozi hupeleka taarifa kwa njia ya kugusa, sikio – kusikia, pua – kunusa, ulimi – kuonja na macho – kuona.

Ulimi wa binadamu una vionjo vinne ambavyo ni utamu, uchungu, ugwadu na ukali.

Vionjo vyote hivyo hupeleka taarifa katika ubongo na hivyo wenyewe kutoa tafisiri juu ya kitu alichoonja mwanadamu iwapo ni kitamu, kikali, kigwadu au kichungu.

Hata hivyo pamoja na milango hiyo ya fahamu ambayo wengi wetu tunaifahamu na tunaiona kwa macho, ipo pia milango mingine ya fahamu ambayo yenyewe huwezi kuiona kwa macho ya kawaida wala kuigusa.

Mtaalamu wa Tiba ya Utengamao na Mazoezi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Rosemary Kauzeni, anasema wataalamu wa afya pekee wakiwamo wa tiba ya mazoezi ndiyo wanaoweza kuielezea milango ya fahamu isiyoonekana.

“Kuna ambao upo kwa ajili ya kufanya mwili uweze kupata uwiano, kitaalamu wanaita ‘vestibular sense’ wenyewe upo katikati ya masikio na kichwa cha mwanadamu.

“Mlango huu kazi yake kubwa ni kuhakikisha mwili unapata uwezo wa kukaa, kusimama, kutembea au kufanya jambo lolote pasipo kuanguka (kudondoka).

Dk. Kauzeni anasema mlango mwingine wa fahamu upo ndani kabisa ya ufahamu yaani kwenye ubongo.

“Huu hutafsiri na kutoa taarifa juu ya eneo alilopo mtu, kuna hali ya namna gani, labda ni joto au baridi na mambo mengine kama hayo,” anasema.

Anasema humsaidia mtu kupata hisia mbalimbali na kwamba ili mwili na ubongo ufanye kazi kwa ufanisi ni lazima milango yote ya fahamu isiyoonekana na inayoonekana ifanye kazi sawa sawa.

Anasema sehemu za mwili wa mwanadamu zimeungwa kwa viungio na katika viungio hivyo kuna vishipa vidogo vidogo vinavyoitwa kwa jina la kitaalamu ‘ligaments’.

“Vishipa hivi vinaunganisha misuli ya mwili na kuifunika na nyama, milango yote hii lazima ipeleke taarifa kwenye ubongo na inashirikiana kwa ukaribu,” anasema.

Anasema ubongo hupokea taarifa na kuzitafsiri kisha kugawa kazi kwa viungo vya mwili, kwamba kiungo kipi kifanye kazi gani na kwa wakati gani.

“Hivyo, utendaji bora wa milango ya fahamu huchangia utendaji bora wa ubongo na mwili kwa ujumla,” anasema.

 

Hupata athari

Daktari huyo anasema milango ya fahamu nayo huweza kupata athari mbalimbali kama ilivyo kwa viungo vingine vya mwili.

“Inapotokea imepata athari hufanya ubongo nao kushindwa kutafsiri vema taarifa ambazo hupokea na au kutoa tafsiri zisizo halisi,” anasema.

Anasema hali hiyo huweza kutokea iwapo ubongo unaweza kupokea taarifa nyingi zaidi au kidogo kuliko vile unavyopaswa kupokea.

“Inapotokea hali hiyo, yaani ubongo unapokea taarifa nyingi zaidi au kidogo tunasema ubongo umepata ajali.

“Hali hiyo inapotokea binadamu hujisikia vibaya. Si mara zote milango yote inaweza kuathirika, unaweza kuathirika mlango mmoja, miwili au mitatu na mingine ikaendelea kustahimili na isipate madhara kabisa.

 

Ubongo na idara zake

Anasema ubongo una idara zake ambazo hueleza namna gani mtu atende.

“Kuna idara zinatafsiri uoni, hisia za ngozi, vionjo. Milango ya fahamu inaposhindwa kufanya kazi sawa sawa husababisha utendaji kazi wa idara hizo nazo kutetereka,” anasema.

Dk. Kauzeni anasema wataalamu wameligawa tatizo hilo katika maeneo manne.

“Eneo la kwanza ni pale utendaji kazi wa mtu unapoweza kuvurugika kwa urahisi, kwa mfano sauti kidogo ikipenya masikioni mwake huwa kero kubwa na hata kudhani dunia yote imejaa sauti,” anabainisha.

Anasema milango ya fahamu inapofanya kazi yake vizuri ni rahisi mtu kuchuja sauti anayohitaji ipenye katika masikio yake.

“Yaani akikaa mahala hata kama kuna sauti nyingi kiasi gani, anao uwezo wa kuruhusu sauti moja pekee ipenye masikioni mwake na akaendelea kufanya kazi zake kama kawaida.

“Ndiyo maana anakuwa na uwezo wa kukaa; kwa mfano, darasani na kukawa na kelele nyingi zinapigwa na wanafunzi lakini akaendelea kujisomea na hata kufanya vema katika mitihani yake,” anasema.

Anasema mtu mwenye tatizo katika mlango wa fahamu wa ngozi wakati mwingine anaweza kulalamika anaumia hata anapoguswa na kitu fulani.

“Unakuta mtu analalamika hata akikatwa kucha, akinyoa nywele, ndevu au hata wakati mwingine anaweza kukwepa kuvaa baadhi ya nguo zake akidai zinamuumiza,” anabainisha.

Anaongeza: “Unakuta anachangua aina ya nguo za kuvaa kwa sababu zingine akivaa zinamuumiza kwani kiwango chake cha hisia huwa kipo juu mno kuliko kawaida.

“Wapo wengine huwa hawataki kutumia hata mashuka mazito (blanketi), au kuvaa sweta kwa sababu anaona zinamuumiza.”

Anasema tatizo jingine ni kukosa usingizi. Kwamba anakaa muda mwingi bila kupata usingizi na hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu hupata maumivu ya kichwa, yote hii ni kwa sababu milango yake ya fahamu inakuwa haifanyi kazi yake sawa sawa kwa pamoja,” anasema.

Dk. Kauzeni anasema wakati mwingine hushindwa kuhimili vionjo na anapoonja kitu chochote huona kero kubwa na wengine wakiona mwanga uwe mkali au mdogo kwao huwa ni kero.

 

Watoto

Anasema watoto wenye tatizo hilo mara nyingi hupenda kukimbia kimbia, kuruka ruka bila kujali kwamba wanaweza kuumia kulingana na mazingira waliyopo.

“Hupendelea kusukuma vitu ovyo kutoka sehemu moja hadi nyingine na wanaweza kushika kitu kigumu muda mrefu wakitembea nacho huku na huko,” anasema.

Anasema wakati mwingine wanapochukua kitu kutoka sehemu moja hadi nyingine hudondosha kila mara.

“Wakati mwingine wanapowekwa juu ya vitu kwa mfano, kwenye bembea huwa wanaogopa na hata wakitembea hupepesuka.

“Huonekana walegevu, huchoka haraka, hawana utulivu na wakikaa huwa hawakalii makalio (wanakaa kama vile wanataka kulala),” anasema na kuongeza:

“Watoto wenye tatizo hili ukiwabeba huwa ni wazito mno kama vile jiwe na uzito huo huwa upo zaidi katika eneo la kifua na mgongo.

“Ukiangalia unyao wao utaona hauna uvungu wenyewe huwa upo ‘flat’ hivyo ni muhimu wazazi kuwachunguza watoto wao,” anasema.

Anasema changamoto nyingine ambayo watoto wenye tatizo hilo hukabiliana nayo ni kupangilia shughuli zao.

“Hupata wakati mgumu kufanya kazi bila kusaidia mpangilio wa kazi husika, kama hawapewi mpangilio wa kazi husika huwa ni rahisi ‘kuvurugika’ kwa haraka na shughuli hiyo haitaweza kufanyika,” anasema.

Dk. Kauzeni anaongeza: “Kama tayari ni mwanafunzi utaona ushikaji wake wa kalamu si wa kawaida, yaani unakuta ameishika yote.

“Hata mpangilio wake wa mwili jinsi anavyokaa au kuandika huwa si wa kawaida, unakuta kama vile amelala kidogo,” anabainisha.

 

Watu wazima

Anasema kwa upande wa watu wazima mara nyingi huwa na hasira na wakati mwingine hupendelea kukaa kimya.

“Huwa hawapendi kuzungumza na utendaji wao wa kazi huwa hafifu pindi wanapobadilishiwa kazi hata kama awali alipangilia vizuri, awamu hiyo hataweza kuifanya tena.

“Hata mpangilio wao wa mwili huharibika na unapoharibika hujikuta wakipata maumivu ya viungo, mgongo, shingo, misuli kubana na kwenye viungio.

“Wengine misuli yao hulegea kupita kiasi na kujikuta mgongo nao ukilegea kwa sababu zile nyama za mgongo huwa hazishikilii tena uti wa mgongo ili uwe sawa,” anasema.

 

Visababishi

Anasema hadi sasa dunia haijatambua kwanini milango ya fahamu hupata ajali lakini viashiria vikubwa wametaja mazingira mtu anayokulia.

“Kuanzia tumboni mwa mama kama hakukuwa na uchangamfu wa kutosha mtoto kuweza kuzunguka na kucheza ukuaji wa mlango huwa mdogo.

“Baada ya mtoto kuzaliwa pia kunaweza kutokea shida kama mtoto hawezi kuwekwa kwenye mazingira yatakayomfanya milango yake ichangamke, ni namna gani ataweza kupata taarifa inavyotakiwa,” anasema na kuongeza:

“Wakati mwingine mazingira nayo yanaweza kuchangia mtu kupata tatizo hili, kwa mfano, ukiwa katika eneo ambalo lina kelele nyingi.

 

Uhusiano na magonjwa mengine

“Usafi nao ni jambo la msingi kulizingatia, kwa sababu kama mtu ana tatizo hili la milango ya fahamu, akakakutana na harufu kali labda ya choo ubongo wake unaweza kutafsiri tofauti.

“Anaweza kuanguka na kupoteza fahamu na mtu anapodondoka ikiwa atajipigiza kichwa chini misuli inaweza kupasuka na hivyo kumsababishia kupata tatizo la kiharusi,” anabainisha.

 

Mazoezi ni tiba

Anasema tatizo hilo linatibika kwa njia ya mazoezi na dawa maalumu ambazo wataalamu huwapatia wagonjwa.

“Mazoezi ni muhimu kwa afya, unapofanya mazoezi kwa mfano ya kutembea mwili huwa unawasiliana na ubongo  moja kwa moja.

“Ubongo ulivyoumbwa ni kama vile kifaa cha CPU kwenye kompyuta, wenyewe unaushughulisha mwili wa binadamu,” anasema.

Anasema katika kliniki yao kwenye Idara ya Tiba ya Mazoezi na Utengamao Muhimbili kwa siku huwa wanapokea na kutibu watoto 20 na watu wazima 10 wenye tatizo hilo.

“Matibabu huchukua hadi siku 14 na mtu hupona kabisa lakini hutegemea wakati mwingine kwa watoto huchukua hadi siku 30,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles