27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAYAI YANAWEZA KUKUEPUSHA USIPATE KIHARUSI, KUNYONYOKA NYWELE UZEENI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


WATU wengi duniani wanaamini kuwa ulaji wa mayai ni hatari kwa afya kwani huweza kumsababishia mlaji kupata magonjwa mbalimbali hasa ya moyo.

Lakini huenda matokeo ya utafiti uliofanyika nchini China hivi karibuni uliohusisha watu 500,000 yakabadili mtazamo huo walionao watu wengi.

Utafiti huo unaeleza, ulaji wa mayai una faida lukuki kwa afya ya binadamu na husaidia kumkinga mtu dhidi ya magonjwa mengi ikiwamo ya moyo, saratani na kiharusi.

Kwa mujibu wa watafiti waliofanya utafiti huo, mayai yana virutubisho vingi muhimu ambavyo huhitajika katika mwili wa binadamu.

Wanasema mayai yana ‘utajiri’ mkubwa wa Vitamin A, B, B2, B5, B9, B12 na D pia yana kiwango cha juu cha protini na madini ya lutein na zeaxanthin.

Wanasisitiza kwamba ni muhimu mtu ale mayai yaliyondaliwa katika namna inayofaa ili kupata lishe bora na kinga dhidi ya maradhi tajwa.

“Mtu anaweza kufikiria zaidi kuhusu tahadhari ambazo zimekuwa zikitolea na wataalamu wa lishe, kilichobainika ni kwamba ulaji wa angalau yai moja kwa siku hakuongezi hatari ya kupata magonjwa ya moyo badala yake kuna faida,” anasema Profesa Nita Forouhi wa Chuo Kikuu cha Cambridge.

 

Mwaka 2007 wakfu wa Moyo Uingereza (BHF) uliondoa ushauri wake wa kuwataka watu wasile mayai zaidi ya matatu kwa wiki kutokana na kutokea kwa utafiti mpya kuhusu cholesterol.

Kwa mujibu wa ushauri wa Huduma ya Taifa ya Afya Uingereza (NHS), “ingawa mayai yana cholesterol, kiwango cha mafuta kutoka kwa mafuta na vyakula vingine tunavyovila huathiri zaidi kiwango cha chorestrol kwenye damu kuliko kinavyoathirika kutokana na ulaji wa mayai.”

Watafiti wanaeleza kuwa kimsingi mayai si chanzo cha matatizo ya kuwapo kwa kiwango cha juu cha choresterol kwenye damu bali yale mafuta  tunayoyatumia.

Kwa mujibu wa Heart UK, yai la kawaida (58g; 2oz) huwa na mafuta 4.6g na ni robo pekee ya mafuta hayo huwa mafuta mabaya, yaani yale yanayoongeza kiwango cha choresterol.

 

Wataalamu wa lishe

Daktari Frankie Phillips wa Chama cha Wataalamu wa Lishe Uingereza anasema: “Yai moja au hata mawili kwa siku hutosha kwa mahitaji ya mwili na kwamba watu hawapaswi tena kuwa na wasiwasi juu ya ulaji mayai.

Dk. Phillips anasema onyo pekee ambalo watu wanapaswa kulizingatia ni kula chakula cha aina moja pekee kwa wingi, kwa kuwa husababisha miili yao kukosa madini na virutubisho vingine vinavyopatikana kwenye vyakula vingine mbali na mayai.

“Ingawa mayai yana protini, lakini mwili pia hupata protini kutoka katika vyakula vingine, jambo la kuzingatia ni kwamba ulaji wa vyakula vyenye protini kupindukia unaweza kukusababishia ‘kuwa mzigo kwa figo.’

Kwa kuangazia jinsi tunavyopika mayai, mayai ya kuchemshwa ndiyo bora zaidi.

Wataalamu wengi wa lishe hupinga kukaangwa kwa mayai kwa sababu mara nyingi mafuta hutumiwa na hivyo kiwango cha cholesterol anachokula mtu huongezeka.

Wanasema mayai mabichi au yalivyopikwa kidogo tu pia ni sawa, mradi tu yawe yanatoka kwenye mazingira safi.

Wanasema mayai yaliyopikwa ndiyo njia bora zaidi ya kujikinga na maambukizi na kwamba si vema kununua mayai ambayo yamevunjika kwa kuwa yanaweza kuwa yameingiwa uchafu au bakteria.

“Wengi bado wanakumbuka jinsi ya kutumia maji kwenye bakuli ili kubaini iwapo yai limeharibika au la.

Iwapo litazama, ni bora na lisipozama limeharibika,” wanabainisha.

Wanasema mayai mengi huwa katika kiwango kizuri kwa siku 28 tangu yanapotagwa.

 

Daktari JKCI

Pedro Pallangyo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anasema mayai pia yana madini ya Zinc, Selenium, Iodine na Phosphorus.

Anasema vitamin hizo huwa na kazi tofauti katika mwili wa binadamu ambapo vitamin A husaidia macho kuweza kuona vizuri.

“Vitamin D yenyewe huhusika kwenye mifupa, B zina kazi nyingi kwenye vimeng’enya ndani ya mwili.

“Mtu akila yai moja maana yake anapata mjumuisho wote wa vitamin na madini muhimu yanayohitajika mwilini,” anasema.

Anasema ule weupe wa yai umerutubishwa kwa kiwango cha juu na protini na kile kiini chake kina mafuta hali inayowafanya wengi kuamini kwamba yana cholesterol nyingi.

Anasema kitaalamu mayai yanahusishwa na kuufanya mwili kuwa na afya njema, pia huusaidia kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

 

Kinga dhidi ya saratani ya kizazi

Anasema upo utafiti uliowahi kufanyika nchini Marekani ambao ulionesha kuwa mayai yana uwezo mkubwa wa kuwakinga wanawake dhidi ya saratani ya kizazi.

“Utafiti huo ulionesha wanawake wanaokula mayai sita kwa wastani kila wiki, walikuwa na uwezekano mdogo wa kupata saratani ya kizazi kwa kiwango cha asilimia 40 kushuka chini ikilinganishwa na wale wasiokula,” anasema.

 

Kiharusi

Anasema ulaji wa mayai mara kwa mara husaidia kumkinga mtu dhidi ya kiharusi. “Kiharusi kimegawanyika katika aina mbili, kuna kile ambacho husababisha kuvilia kwa damu kwenye ubongo, na kile ambacho damu huwa haivilii kwenye ubongo.

“Utafiti ule ulionesha kwa asilimia 26 mayai humsaidia mtu kumkinga dhidi ya kiharusi cha kuvilia damu kwenye ubongo,” anasema.

 

Moyo na mfumo wa fahamu

Anaongeza: “Upo utafiti pia uliowahi kufanyika na kubainisha kwamba mayai humkinga mtu kwa asilimia 18 asipate magonjwa ya moyo ukilinganisha na wale wasiokula.

Anasema mayai yana madini mengine muhimu ambayo husaidia kuilinda mifupa ya binadamu na kulinda mfumo wa fahamu.

“Hasa kipindi ambacho mtu anafikia uzee, mara nyingi hupata ugonjwa wa kutetemeka mwili na kusahau, wale wanaokula mayai mara kwa mara huwa na afya njema na nzuri ya ubongo kuliko wasiokula,” anasema.

 

Afya ya kucha, nywele

Daktari huyo ambaye pia ni mbobezi katika kufanya tafiti mbalimbali, anasema ulaji wa mayai pia unahusishwa na kusaidia kuimarisha afya ya nywele na kucha.

“Tafiti zimewahi kuonesha watu wanaokula mayai mara kwa mara wanakuwa na uwezekano mdogo wa kupoteza (kunyonyoka) nywele zao pamoja na kucha wakifikia umri wa utu uzima,” anasema.

Anasema kwa watu wanaougua saratani mara nyingi hupoteza nywele zao hasa wale wanaopata tiba ya mionzi, ikiwa watakula mayai mara kwa mara watapokea ile protini ambayo huipoteza kutokana na ugonjwa huo.

 

Unavyopaswa kuyaandaa  

Dk. Pallangyo anasema pamoja na kwamba mayai yana virutubisho hivyo muhimu hata hivyo suala la uandaaji wake ni jambo la kuzingatiwa ili mtu aweze kuvipata vyote.

Anasema kitendo cha kutumia moto mkali au kupika yai kwa muda mrefu kunaua ile protin iliyopo na hivyo kulifanya lisiwe na faida mwilini.

Anasema yai likipikwa kwa muda mrefu hupoteza vile virutubisho vyote muhimu na kulifanya lisiwe na thamani.

“Kimsingi ikiwa mtu anataka kupata vile virutubisho vyote muhimu ni vizuri akila yai likiwa bichi kabisa, pale vinakuwa havijabadilishwa, lakini likiwekwa jikoni huvipoteza kadiri linavyokuwa linazidi kupikwa,” anasema.

Anafafanua: “Yaani yai ambalo linakuwa halijapikwa muda mrefu jikoni, hubaki na virutubisho kuliko lile lililopikwa kwa muda mrefu.

Anasema tafiti zinaonesha kula wastani wa mayai matano hadi sita kwa wiki moja ni vema, au kula mawili hadi matatu inaweza kukufanya ukapata kiwango kikubwa cha colestero.

Anasema ni vema kula yai lilichemshwa, au kama litakaangwa basi iwe ni kwa kutumia mafuta ya mimea hasa alzeti na yawekwe kwa kiwango kidogo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles