Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
UPELELEZI wa kesi ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, umekamilika.
Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii umekamilika, upande wa Jamhuri tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali,” alidai Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi.
Mahakama ilikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Oktoba 11, mwaka huu, kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Katika kesi hiyo, Halima anadaiwa kutenda kosa Julai 4, 2017, katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyopo Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni.
Anadaiwa kumtukana Rais John Magufuli kwa kusema “anaongea hovyohovyo , anatakiwa afungwe breki”, kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.