UPANDE wa Jamhuri umedai upelelezi wa kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam (RAS), Theresia Mbando inayomkabili wabunge wa Kawe, Ubungo, Ukonga na wengine umekamilika.
Hayo yalielezwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa Serikali, Flora Massawe alidai kesi hiyo ilikuwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Shaidi alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Oktoba 12, mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Washtakiwa katika kesi hiyo, ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga), Diwani wa Kata ya Kimara, Ephrein Kinyafu (Chadema), Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (Chadema) na mfanyabiashara Rafii Juma.
Washtakiwa wote wanadaiwa kutenda kosa hilo la kujeruhi Februari 27 mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee wilayani Ilala wakati wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Dar es Salaam.
Ilidaiwa washtakiwa hao kwa pamoja, walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha.
Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana kwa masharti kwamba wajidhamini wenyewe kwa kutia saini dhamana ya Sh milioni mbili kila mmoja.