Amina Omari,TANGA
IMEELEZWA unywaji wa maziwa kwa watu wenye umri mkubwa huzuia maumivu ya misuli na kurudisha ute ulipotea kwenye misuli .
Hayo yamesemwa na Meneja Vyanzo vya Maziwa wa Kiwanda cha kuzalisha maziwa cha Tanga Fresh, Annadomana Nyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari na watafiti waliokuwa katika mafunzo ya habari za kisayansi yaliyoendeshwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia ..
Alisema tafiti zinaonyesha maziwa yana wingi wa madini ya proteni ambayo yanasaidia kuimarisha mifupa hasa kwa watoto na wazee.
Alisema iwapo wazee watakunywa maziwa katika kiwango stahiki, wataepukana na uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya mifupa ambao umekuwa changamoto kubwa kwao.
“Tatizo kubwa lililopo,Watanzania hatuna utamaduni wa kunywa maziwa, takwimu zinaonyesha mtu mmoja anastahili kunywa lita 100 kwa mwaka,mpaka sasa Watanzania wanakunywa lita 47 pekee kwa mwaka,”alisema Nyanga.
Alisema sasa wapo kwenye mpango wa kuwaelimisha wafugaji namna bora ya ufugaji bora ambao utawezesha kuongeza uzalishaji.
Alisema ili kufanikisha hilo, tayari wameshaanza ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Mifugo (TALIRI- Tanga) ili kuzalisha malisho bora.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TALIRI kituo cha Tanga, Zablon Nziku alisema kwa kutumia teknolojia mpya yauzalishaji wanauhakika watamaliza changamoto ya malisho kwa wafugaji.
Alisema kikwazo kikubwa cha wafugaji kutoendelea ni kutokana na ukosefu wa malisho ya uhakika, hasa kipindi cha kiangazi.