Na FREDRICK KATULANDA-MWANZA
MWILI wa mfanyabiashara na mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Josiah Mzuri, maarufu kama Super Sami, mkazi wa Mwanza, umepatikana wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.
Mwili huo ulipatikana juzi katika Mto Rubana, ukiwa umefungwa katika viroba na ukiwa umeharibika vibaya.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed, alisema mwili huo ulipatikana juzi jioni katika mto huo ulioko mpakani mwa Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara na Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Kamanda alisema hadi jana walikuwa wakishikiliwa watu watano kutokana na upelelezi uliofanyika.
Kwa mujibu wa Kamanda, baadhi ya wananchi waliokuwa mtoni hapo ndiyo waliuona mwili huo ukiwa umefungwa kwenye kiroba ambao walitoa taarifa polisi waliofika na kuutoa ndani ya maji.
“Jana (juzi) jioni, wananchi waliona kiroba ndani ya Mto Rubana kikiwa kimefungwa na baada ya kukitilia shaka, walitoa taarifa polisi ambao walifika na kukivuta kutoka mtoni.
“Baada ya kubaini ni mwili na kwa kuwa kulikuwa na taarifa za ndugu wa Josiah kutafuta ndugu yao, tuliwasiliana nao kuja kuutambua na waliweza kuutambua kwamba ni wa ndugu yao ambaye ni mmiliki wa mabasi ya Super Sami,” alisema Kamanda Mohamed.
Mohamed aliwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi liweze kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba wananchi kwamba kama kuna mtu mwenye taarifa zinazohusiana na kifo cha ndugu Josiah, basi awasiliane nami moja kwa moja anieleze na ninawahakikishia tutakuwa na usiri wa hali ya juu kwa watoa taarifa wote,” alisema.
Kaka wa mfanyabishara huyo, Amini Mzuri, alikiri kuutambua mwili wa ndugu yake na kusema ulikutwa ukiwa katika hali mbaya kwa kuwa ulikuwa umeshaanza kuharibika.
“Tumeutambua ni mwili wa ndugu yetu, umepatikana Mto Rubana, lakini kwa sasa tunangojea uchunguzi wa kina wa mwili huo… nadhani baada ya hapo tunaweza kuongea lolote,” alisema.
Mfanyabishara huyo anadaiwa kutoweka Februari 27, mwaka huu nyumbani kwake eneo la Mwananchi, Buzuruga, Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana, Mwanza.
Wakati anaondoka nyumbani kwake alikuwa na gari lake Nissan Patrol namba T 323 BSF ambalo lilipatikana Machi 9, mwaka huu likiwa limeteketea kwa moto katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Pembeni mwa gari hilo, kulikuwa na panga na kiberiti ambavyo inasemakana viliwekwa na waliohusika na uhalifu huo.
Taarifa zilizopatikana zinasema wakati Josiah anaondoka Mwanza, alielekea katika mji mdogo wa Ramadi wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya shughuri ambazo hazijawekwa wazi.
Kaka wa marehemu alikaririwa akieleza kuwa siku hiyo ya Februari 27, mwaka huu, ndugu yake huyo baada ya kuondoka nyumbani asubuhi, usiku saa 3.00 alimpigia simu mkewe akimweleza kuwa alikuwa njiani kurudi lakini alikuwa na mgeni.
Hata hivyo, ndugu huyo alisema hakurudi nyumbani hadi Machi 9, mwaka huu, gari lake lilipopatikana likiwa limeteketea kwa moto.
“Tumefanikiwa kuuona mwili huo, nathibitisha ni wa ndugu yetu na hivi hapa tunavyoongea tunangoja uchunguziu zaidi wa utalaam, tupo Hospitali ya Mkoa wa Mara ambako mwili wake utafanyiwa uchunguzi.
Wakati hayo yakiendelea, Machi 9, mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, alieleza kwamba baada ya gari la marehemu kupatikana walifanya uchunguzi wa awali na kujiridhisha kuwa ni mali ya mmiliki wa mabasi hayo ingawa miezi mitatu iliyopita, lilikuwa likimilikiwa na John Zephania.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.