LONDON, England
TIMU ya Manchester United jana iliifunga Swansea mabao 4-0, katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu England, uliochezwa Uwanja wa Liberty, Wales.
Mabao ya Eric Bailly, Romelu Lukaku, Paul Pogba na Anthony Martial yaliipatia Manchester United ushindi wa pili katika kampeni yao ya kunyakua ubingwa msimu huu, baada ya kushinda mabao 4-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya West Ham.
Nyota hao wanaifanya United kuanza msimu wakiwa na mabao mengi zaidi katika michezo ya kwanza ya Ligi Kuu tangu msimu wa 1907/08.
Mabao nane kwenye michezo miwili yanaifanya United kuongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi sita.
United ilifunga bao dakika ya 45, baada ya Jordan Ayew wa Swansea kufanya makosa yaliyoigharimu safu ya ulinzi, ambapo Eric Bailly aliandika bao la kuongoza.
Bao la pili la United lilifungwa na Lukaku dakika ya 80, kabla ya Paul Pogba kufunga la tatu dakika ya 82 na kuhitimishwa na Anthony Martial dakika ya 84.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, alisema: “Tunajiamini, kwa kuwa tunafahamiana kila mmoja, ni msimu wa pili, unatakiwa kubadili kikosi ukiwa kocha kwa mara ya kwanza.
“Ndiyo, kwenye mwaka wa kwanza tulishinda taji, lakini sasa tunajiamini na rahisi kwetu kufanikiwa.”
Kabla ya ushindi huo, United hawakuwa na rekodi nzuri dhidi ya Swansea katika michezo ya hivi karibuni. Mchezo wa mwisho katika Uwanja wa Old Trafford Aprili mwaka huu, kikosi hicho cha Paul Clement kilipata ponti ya muhimu kubaki Ligi Kuu England.
Sare hiyo ilikuwa ya 10 katika Uwanja wa Old Trafford msimu uliopita, ilikuwa moja ya mechi ambazo Mourinho alichemka kwa msimu wake wa kwanza.