31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

MIAMBA 16 HAKUNA KULALA VPL 2017-18

 

Na MOHAMED KASSARA

-DAR ES SALAAM

WATANI wa jadi, Simba na Yanga wamepiga kambi visiwani Zanzibar wakiendelea na maandalizi yao ya pambano la Ngao ya Jamii, timu nyingine 14 hazijalala, badala yake zinaendelea kujifua kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pambano la Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga ambalo ni maalumu kwa ajili ya kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara litapigwa Agosti 23, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo zimegawana visiwa vya Zanzibar, ambapo Simba imejichimbia mjini Unguja wakati Yanga ikijificha Pemba zikijinoa kwa ajili ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

Kabla ya kutimkia Zanzibar, Simba ilikuwa nchini Afrika Kusini ambako ilipiga kambi ya wiki mbili na kujipima nguvu na vigogo wa soka nchini humo, Orlando Pirates na kupoteza kwa bao 1-0, wakatoka sare ya bao 1-1 na Bidvest Wits, kabla ya kurejea nyumbani na kucheza michezo mingine miwili ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports na Mtibwa Sugar, michezo yote hiyo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye kila mchezo, kabla ya kuelekea Zanzibar ambapo ilicheza mchezo mmoja ambao ililazimishwa suluhu ya 0-0 na Mlandege FC.

 

Kwa upande wa Yanga ilisafiri hadi mkoani Morogoro na kupiga kambi ya  siku 10. Ikiwa huko ilicheza mchezo mmoja dhidi ya Moro Kids ambao waliibuka na ushindi wa mabao 5-0, kisha kurejea Dar es Salaam na kuifunga   Singida United mabao 3-2 na kufungwa na Ruvu Shooting mabao 2-1, kabla ya kwenda Zanzibar na kuifunga Mlandege FC mabao 2-0.

 

Wakati hayo yakijiri kwa vigogo hao, timu nyingine zimekuwa zikihaha huku na kule kuweka kambi kujiandaa na ligi hiyo.

Azam FC

Timu hiyo ilianza maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao kwa kufanya ziara nchini Rwanda, ambapo walipata fursa ya kucheza na mabingwa wa soka nchini humo Rayon Sports na kupoteza kwa kufungwa mabao 4-2.

Baada ya kurejea nchini, Azam ilifanya ziara mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo ilianza kwa kufungwa na Njombe Mji mabao 2-0, kisha ikiifunga Lipuli mabao 4-0 kabla ya kukamilisha ratiba kwa kulazimishwa suluhu 0-0 na Mbeya City.

Azam haikuishia hapo, ilivuka mpaka hadi Uganda ambapo ilipiga kambi ya siku 10.

Ikiwa nchini humo, Azam FC ilifanikiwa kucheza mechi tano za kirafiki, ikianza kwa sare ya mabao 2-2 na timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, ikaambulia sare nyingine ya bao 1-1 KCCA kisha ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu za URA, Onduparaka na Vipers FC.

Kagera Sugar

Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza kwenye nafasi ya tatu, nyuma ya Kagera Sugar iliyokamata nafasi ya tatu, Simba iliyoshika nafasi ya pili na Yanga iliyotwaa ubingwa, ilianza maandalizi yake msimu ujao kwa kupiga kambi jijini Dar es Salaam.

Baada ya kujifua kwa wiki mbili, Kagera Sugar ilirejea nyumbani Bukoba kabla ya kutimkia nchini Burundi kukamilisha programu ya maandalizi.

Lipuli FC

Timu hiyo ambayo ilipanda Ligi Kuu msimu uliopita, ilizindua maandalizi yake ya msimu mpya jijini Dar es Salaam.

Tayari imecheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu za Singida United na Azam FC.

Timu hiyo inayofundishwa na kocha Selemani Matola ambaye ni kiungo wa zamani wa Simba kwa sasa wanaendelea kujifua nyumbani kwao mkoani Iringa wakisubiri kuikabili Yanga katika mchezo wa ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

Majimaji FC

Majimaji wao wameamua kubakia  Ruvuma hususani katika Manispaa ya Songea yalipo makao yako makuu wakijifua kwa ajili  ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbao FC

Timu hiyo ambayo iliwashangaza wengi msimu uliopita baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) nayo  imeamua kusalia jijini Mwanza yalipo makao yake makuu ikijiwinda kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya City

Mbeya City wao wanaendelea na maandalizi ya msimu mpya wakiwa katika viunga vya Jiji la Mbeya yalipo makao yao makuu.

Hivi karibuni iliibuka mabingwa wa michuano ya Ujirani mwema iliyoshirikisha timu mbalimbali za kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mbeya City ambayo pia inafahamika kama Wagonga nyundo wa Jiji la Mbeya walipata fursa ya kutoka nje ya jiji hilo na kufanya ziara mkoani Morogoro, ambapo walicheza mchezo mmoja wa kujipima nguvu dhidi ya Wakata miwa,  Mtibwa Sugar na kushinda mabao 2-0.

Mtibwa Sugar

Ikitokea katika mashamba ya miwa, Mtibwa Sugar ilizindua maandalizi yake ya msimu mpya kwa kupiga kambi jijini Dar es Salam. Baada ya kambi hiyo wakata miwa hao walirejea mkoani Morogoro na kucheza mchezo mmoja dhidi ya Mbeya City na kuchapwa mabao 2-0.

Baada ya kucheza mchezo huo, Mtibwa iliendelea na mazoezi yake Turiani mkoani humo kabla ya kurejea tena Dar es Salaam kucheza mchezo wa kirafiki na Simba ambao walichapwa bao 1-0, kwa sasa wamerejea tena Munungu kumalizia kusuka mikakati ya ushindi msimu ujao.

Mwadui FC

Mwadui imejificha mkoani Shinyanga yalipo makao yake makuu ilijifua kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwadui ilipima makali yake kwa kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Mbao FC na kuibuka na ushindi wa mabao 5-3.

 

 

Ndanda FC

Vijana wa Ndanda wenye maskani yao mkoani Mtwara, wanaendelea na maandalizi ya msimu mpya kimya kimya wakilenga kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi cha Ndanda kinatarajia kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting ambao umepangwa kupigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utaenda sambamba na tukio la kutambulisha wachezaji wapya watakaoichezea Ndanda msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Njombe Mji FC 

Huyu ni mgeni mwingine katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufanikiwa kupanda daraja ikitokea Ligi Daraja la Kwanza.

Njombe Mji ilianza maandalizi ya msimu mpya ambapo ilifanya ziara katika baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kutambulisha jezi zao na kucheza michezo ya kirafiki.

Pia ilipata fursa ya kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Azam FC na kuchapwa mabao 2-0.

Tanzania Prisons

Maafande hao wa Jeshi la Magereza wenye maskani yao mkoani Mbeya, wanaendelea kujifua vikali, lakini wameamua kuibakia jijini humo hadi pale msimu mpya wa Ligi Kuu utakapoanza.

Wajela jela walipata fursa ya kujipima na kikosi cha Azam FC.

Ruvu Shooting

Maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa  kutoka mkoani Pwani hawako nyuma kwani walianza mapema maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wanajeshi hao walijipima ubavu na Yanga kwa kucheza nayo mechi ya kirafiki na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Timu hiyo leo inatarajia kushuka dimbani tena kuikabili Ndanda katika pambano la kirafiki kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo itafungua kampeni zake kwa kuumana na Simba.

Singida United

Singida United inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, ilipanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita ikitokea Ligi Daraja la Kwanza.

Kikosi cha Singida United kinaweza kuwa ndicho kilichoweka rekodi ya kuanza mapema maandalizi yake ya msimu mpya baada ya kupiga kambi ya mwezini mmoja mkoani Mwanza.

Kikosi hicho hadi sasa kimecheza mechi kadhaa za kirafiki zikiwemo dhidi ya Yanga, ambapo kilipoteza kwa kuchapwa mabao 3-2, kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli FC.

Singida itafungua pazia la Ligi Kuu kwa kuikabili Mwadui FC.

Stand United

Timu hiyo ilichelewa kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania kutokana na kuwa katika mchakato wa kusaka kocha.

 

Baada ya kufanikiwa kumwongezea mkataba Athumani Bilal, sasa inaendelea kujifua nyumbani kwake Shinyanga  tayari kwa heka heka za msimu mpya.

Lakini kabla ya kujituliza Shinyanga, kikosi cha Stand United kilifanya ziara katika mikoa ya Mara na Mwanza na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles