MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili waweze kurejea makwao na kuendelea na shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa baada ya juzi UNHCR kuiomba Tanzania kutowarudisha kwa lazima wakimbizi wa Burundi waliowahifadhi kwa kuwa nchini kwao hali bado si salama.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi kwenye Kituo cha Maonyesho cha Yokohama nchini Japan baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, katika mazungumzo hayo, Majaliwa amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia mikoa inayokaliwa na wakambizi kutokana na kuharibiwa mazingira.
“Hata hivyo Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na UNHCR kuimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu.” Taarifa hiyo ilimkariri Majaliwa
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Grandi amesema amefurahishwa na utayari wa Serikali ya Tanzania kuwapokea wakimbizi na usikivu wa Rais Dk. John Magufuli katika kushughulikia changamoto zao.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Japan akimwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano huo wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ambao ulihitimishwa jana.
Waziri Mkuu alikuwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.