25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

UNDANI WA UBINAFSISHAJI VIWANDA WAANIKWA NA MZALENDO MKEREKETWA

  • KIWANDA CHA BILIONI 16 KILIUZWA MILIONI 462

Na LYAMUYA STANLEY

AMINI usiamini bali hili limetokea hapa nchini Tanzania ambako kiwanda kilichojengwa kwa jumla ya shilingi bilioni 16, kiliuzwa moja kwa moja kwa shilingi milioni 462 tu pamoja na malighafi na magari.

Kiwanda hiki si kingine bali ni cha madawa mjini Moshi kilichokuwa chini ya Shirika la Viwanda vya Madawa nchini yaani (National Chemical Industries, NCI) kikijulikana kama Moshi Pesticides Plant (MPP) ambacho kiliuzwa kwa bei ya asilimia tatu (3%) ya gharama za ujenzi wake na kamati ya kubadilisha mfumo wa mashirika nchini kwa lugha ya Kiingereza ikijulikana kama Parastatal Sector Reform Committee (PSRC) mwaka 2003.

Haya yalisemwa na mfanyakazi mmoja katika kiwanda hiki ambaye kwa sababu za kiusalama hakutaka kujitambulisha kwani kulitaja jina lake kunaweza kupelekea kitumbua chake kuingia mchanga. Lakini ukweli lazima usemwe kuona mali ya umma ilivyotapanywa na kuhujumiwa na hivyo itakuwa kazi kuvirejesha tena kwa Serikali.

Mfanyakazi huyo mzoefu wa miaka mingi kuanzia wakati kikijengwa chini ya NCI ameajiriwa na mwekezaji, alisema alishuhudia ubinafsishaji wa kiwanda husika kwa mshangao mkubwa kwani kwa uelewa wake hakukuwa na sababu zozote za kimsingi kama si hujuma ya kukiuza kiwanda husika kilichojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 16 kwa mwekezaji kwa gharama ya shilingi milioni 462 tu. “Ni wizi mtupu,” anasema.

Akizungumzia wakandarasi waliohusika na ujenzi wa kiwanda hicho aliyataja makampuni ya J.S. Khambaita Construction enzi hizo ikiwa mjini Moshi iliyohusika na ujenzi wa kiwanda husika (civil works) na Kampuni ya TECNI MONT spa kutoka nchini Italia ambayo ilihusika kuleta mitambo na kuifunga katika kiwanda husika.

Akielezea uwepo sasa hivi wa kampuni husika nchini alisema J.S. Khambaita alishazifunga ofisi zake mjini Moshi wakati Kampuni ya TECNI MONT spa iliondoka nchini na kurudi Italia baada ya kumaliza shughuli ya kufunga mashine na mitambo katika kiwanda husika.

Alipoulizwa nini lilikuwa dhumuni kubwa ya kukijenga kiwanda hicho mjini Moshi alisema lilikuwa kuwapatia wakulima wa Afrika ya Kati na Mashariki mahitaji yao ya madawa ya kilimo kwa bei nafuu.

“Si hili tu bali ujenzi wa kiwanda husika ulilenga pia na kuongeza ajira pamoja na kipato serikalini kupitia kodi mbali mbali,” alisema.

Akizungumzia bidhaa zilizokuwa zikizalishwa na kiwanda husika kabla ya kubinafsishwa alisema kiwanda hicho kilikuwa kikizalisha jumla ya tani 1,500 kwa mwaka za mruturutu (Blue Copper or Copper Oxy Chloride) ambazo wateja wake wakubwa walikuwa wakulima wa kahawa na wale wa mboga mboga kwa matumizi ya kuondoa fangasi na kutu katika majani ya mimea.

“Kwa upande mwingine kiwanda kilizalisha jumla ya tani 3,000 kwa mwaka za madawa ya kuua magugu (herbicides) kitaalamu ikijulikana kama Atrazine ambazo wateja wake wakubwa walikuwa viwanda vya sukari vya TPC na Kilombero.

Akiongelea bidhaa nyingine ambayo ilitarajiwa kuzalishwa na kiwanda hiki kabla ya kubinafsishwa aliitaja kuwa dawa ya unga ya kuua wadudu na kuongeza kuwa hata hivyo bidhaa hii haikuwahi kuzalishwa.

Akiongelea ubinafsishwaji wa kiwanda hicho, alisema PSRC ilikiuza moja kwa moja kiwanda husika kwa kampuni moja yenye makao yake mjini Nairobi nchini Kenya iliyojulikana kama Twiga Chemical Industries na kuongeza kuwa hilo lilifanyika mwaka 2003.

Akifafanua alisema ubinafsishaji huo ulikuwa na masharti ambapo PSRC ilitakiwa kuyafuata masharti yaliyowekwa na Twiga Chemicals Industries na si vinginevyo.

Akiyataja baadhi ya masharti hayo alisema moja lilikuwa kwamba malighafi zote zilizokuwa katika maghala hapo kiwandani hayakujumuishwa katika ubinafsishaji huo na yalitolewa bure kwa mwekezaji. Huenda kuna maofisa wa NCI walilipwa lakini hakuna anayejua.

“Ilisikitisha mno pale ilipoeleweka kuwa mwekezaji alipewa bure malighafi zilizokuwepo kiwandani ambazo alizitumia kuzalisha madawa aina ya mortutu (Blue Copper) na ile ya kuua magugu dawa ambazo ziliuzwa kwa wakulima wa kahawa nchini na viwanda vya kuzalisha sukari nchini hivyo mwekezaji akafanikiwa kilaini kurudisha pesa zake zote kiasi cha shilingi milioni 462 ambazo awali alizitoa ili kukinunua moja kwa moja (outright purchase) kiwanda hiki cha Moshi Pesticides Plant,” alisema huku akiongeza kuwa hii ilikuwa sawa na kumpa bure mwekezaji kiwanda husika.

Alilitaja sharti jingine lililowekwa na mwekezaji kuwa PSRC kuchukua jukumu lote la kuwaachisha kazi na kuwalipa mafao yao wafanyakazi wote ambao idadi yao ilikuwa themanini na nane (88) kwa mwaka huo 2003.

“PSRC kama ‘kipofu’ iliyakubali masharti husika na wafanyakazi wote 88 waliachishwa kazi mwaka 2003 na kulipwa notisi ya mshahara wa mwezi mmoja, likizo mshahara wa mwezi mmoja na nauli ya kurudi nyumbani,” alisema kwa uchungu  mkubwa huku akisisitiza kuwa malipo hayo yalikuwa kiduchu sana.

Si haya tu aliongeza kuwa hata nyumba nane (8) za wafanyakazi zilizokuwa mali ya MPP zote zikiwa vyumba vitatu; vya kulala, chumba cha kulia chakula, sehemu ya kufulia nguo, vyoo na bustani nzuri kila moja ikiwa ndani ya robo tatu ya ekari pia ziliuzwa kwa bei ya kutupwa.

“Nyumba hizi ambazo zilijengwa kwa thamani ya shilingi milioni 25 kila moja mwaka 1996, ziliuzwa  kwa watu binafsi kwa shilingi milioni 5 tu,” alisema na kuongeza kuwa huu ulikuwa wizi wa mali ya umma mchana kweupe na atafurahi sana kama hatua zitachukuliwa.

Akiongelea ni nini kingine mali ya MPP iliuzwa kwa bei chee na PSRC aliyataja magari mawili aina ya FIAT 682 yenye uzito wa tani kumi (10) ambayo yaliuzwa kwa watu binafsi wakazi wa jijini Dar es Salaam kwa bei isiyojulikana kwani menejimenti ya kiwanda kwa wakati huo ilipewa maagizo ya kuyauza magari husika kwa wahusika kwa bei iliyopangwa kwenye maagizo husika na kuongeza kuwa kwa upande wake mwekezaji alirithi magari mawili aina ya Land Rover ambayo baadaye aliyauza kwa watu binafsi.

Mfanyakazi huyu ambaye aliendelea kuajiriwa na mwekezaji alisema kinachomfanya aliye machozi ni pale anapokumbuka ukweli kuwa hata Hati ya Kumiliki Ardhi (Title Deed) ya kiwanda husika inaaminika iliwekwa rehani katika taasisi fulani ya fedha ili kuchukua mkopo ambao ulitumika kujenga kiwanda cha madawa jijini Nairobi eneo la viwanda likijulikana kama Ruaraka Estate mali ya Twiga Chemical Industries na kwa hili akasema siku zote kwenye nchi ya vipofu ukiwa na macho lazima uwe mfalme.

Kuhusu hali ilivyo katika kiwanda wakati huu alisema kiwanda husika ambacho kabla ya kuuzwa kwa mwekezaji kilikuwa na idadi ya wafanyakazi themanini (80), sasa kina wafanyakazi kumi (10), idadi ambayo inajumuisha pia walinzi.

“Hakuna umeme kiwandani kwa sasa kwani umeme ulikatwa na Tanesco tangu mwaka 2009 kutokana na kutokulipia ankara za umeme kwani mazoea ya kunyonga vya kuchinja hawezi.

“Mwekezaji haoni sababu ya kulipa deni la Tanesco ili umeme urejeshwe kiwandani badala yake amenunua jenereta ndogo kwa ajili ya kufanya uzalishaji mdogo wa madawa,” alisema.

Kuhusu uzalishaji unaoendelea kiwandani hapo kwa sasa alisema mwekezaji huingiza malighafi ikijulikana kitaalamu kama (semi finished blue copper au technical copper) na kinachofanyika ni kuichanganya na kuifunga katika vifungashio vidogo na kuongeza kuwa uzalishaji huo hauzidi tani ishirini (20) kwa mwaka madawa ambayo huuziwa wakulima wa kahawa. Mengi ya madawa hayo hayafanyi kazi ya kuua wadudu sawasawa.

“Dawa ya kuua magugu ijulikanayo kitaalamu kama Herbicides Atrazine, huzalishwa kiwandani mara nne kwa mwaka kila mara zikizalishwa jumla ya lita elfu moja na mia tano (1,500) tu ambazo huuziwa wakulima wa mahindi mkoani Mbeya,” alisema.

Akitoa majumuisho ya maelezo yake alisema awali ya yote zoezi zima la kukiuza kiwanda husika lililofanywa na PSRC halikuwa na umakini wowote na PSRC walifanya kama mzaha kwani hawakuelewa thamani halisi ya kiwanda husika. Na kama walielewa basi walifungwa macho kwani kila kitu hufanywa kwa sababu.

“Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania hana budi kutuma hapa kiwandani timu mpya ya wataalamu waje kutathmini upya thamani ya kiwanda hiki ambacho mmiliki wake kwa sasa ni kampuni ya Twiga Chemicals Industries yenye makao yake jijini Nairobi na Dar es Salaam,” alisema.

Kuhusu ni nani anayemiliki kampuni ya Twiga Chemical Industries alimtaja Alnoor Jamal mwenye asili ya Kiasia ambaye pia anamiliki Hoteli ya New Africa iliyopo jijini Dar es Salaam  na anayemiliki  ndege binafsi na mahoteli lukuki nchini Kanada, Marekani na Lusaka, Zambia. Inasemekana ana undugu na Waziri wa Fedha wa zamani wa Tanzania, Amir Jamal, aliyekufa Uingereza na kuzikwa Kanada.

“Jamal ni bilionea ambaye mali zake duniani zina thamani ya mamilioni ya Dola za Kimarekani na makazi yake ni nchini Kanada. Mara ya mwisho kuja kiwandani hapa ilikuwa ni miaka mitano (5) iliyopita alipokuja na ndege yake na kutua uwanja mdogo wa ndege mjini Moshi,” alisema.

Akizungumzia sakata hili ambapo kiwanda kilichojengwa kwa jumla ya shilingi bilioni 16 kiliuzwa kwa shilingi milioni 462 tu Ofisa mmoja katika ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, Gerald Chami, alisema Serikali kwa sasa inashughulikia suala husika na masuala yanayofanana na hayo.

Chami ambaye anaongoza Idara ya Maelezo na Mawasiliano na Umma (Head of Public Relations and Communications) ndani ya ofisi za Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, alisema zoezi linaendelea nchi nzima sasa hivi ambapo mashirika ya umma yaliyopo, mashirika na viwanda vya umma vilivyobinafsishwa au kuuzwa moja kwa moja yote yanapitiwa upya ili kujua hali halisi na ni nini kinafanyika katika mashirika au viwanda husika vilivyobinafsishwa na kuona kama kweli mikataba ilitekelezwa kikamilifu (monitoring and evaluation exercize).

“Matokeo ya awali yameanza kuonekana kwani baadhi ya mashirika au taasisi zilizokuwa zimebinafsishwa tayari makampuni 11 yamerudishwa serikalini na Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuagiza hivyo baada ya kuonana na wahusika. Kiwanda cha Mwanza Tanneries mnunuzi amerudisha mwenyewe kwa ridhaa yake kuwa ameshindwa kazi.

Mfano mzuri ni yaliyokuwa maghala na vinu vya kusagia na kuhifadhi nafaka ambayo awali yalikuwa mali ya Shirika la Taifa la Usagaji (National Milling Corporation) katika miji ya Arusha, Iringa na Dodoma ambayo yalibinafsishwa na kupewa watu binafsi tayari yamerudishwa serikalini na kukabidhiwa kwa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (National Cereal Board) ambayo ni Taasisi ya Serikali,” alisema Chami.

Akiongelea mifuko ya Hifadhi za Jamii ambazo hufanya kazi zinazofanana alisema zoezi hilo la kuyafanyia tathmini linaendelea na kuongeza kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile NSSF, GEPF, PPF na  LAPF inaweza kuunganishwa na kuwa shirika moja ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Wadadisi  wanahoji kwanini ajira za watu hazipewi umuhimu? Vipi ushindani  uliokuwepo ili kuboresha stahiki za mafao?

Chami aliwahakikishia Watanzania mabadiliko makubwa ya kuleta hali mwanana nchini kwa maisha ya watu wake.

“Mambo mazuri yanakuja kwa umma wa Watanzania na uwe na subira kwani zoezi hilo pia limeyapitia mashirika na viwanda vilivyouzwa moja kwa moja kwa watu binafsi baadhi vikiwa vinafanya kazi sasa au havifanyi kazi kabisa,” alijumuisha Ofisa huyu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles