28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

UNAWEZA KUUGUA SARATANI YA TEZI DUME UKAHISI UTI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


KUTOKANA na dhana mbalimbali zinazozungumwa na watu kuhusu ugonjwa wa tezi dume, MTANZANIA limeona ni vema kuzungumza na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Mark Mseti ambaye anafafanua kwa kina  kuhusu ugonjwa huo, dalili zake na tiba.

Dk. Mseti anasema tezidume ni kiungo muhimu kilichopo ndani ya mwili wa mwanamume, chini kidogo ya kibofu cha mkojo kikiuzunguka mrija wa kutolea haja ndogo.

Anasema kiungo hicho hutengeneza majimaji maalumu ambayo huambatana na mbegu za kiume wakati wa tendo la ndoa zikilinda mbegu hadi kulifikia yai la mama na kutengeneza mtoto.

Kwa kawaida tezidume huwa na ukubwa unaolingana na punje ya njegere au mbaazi na huongezeka ukubwa kutokana na mambo mawili, kuongezeka kwa umri au kupata saratani.

Anasema inaweza kuongezeka hadi kufikia ukubwa wa tunda la shufaa (apple). Anasema inapotokea tezidume limepata saratani, dalili kadhaa hujitokeza ambazo hufanana kwa ukaribu na dalili za magonjwa yanayoshambulia njia ya haja ndogo.

 

Takwimu za WHO

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kila mwaka wagonjwa wapya milioni 14.1 hugundulika kati ya hao milioni 8.2 hufariki dunia ikiwa ni sawa na asilimia 13.

WHO inakadiria kwamba vifo hivyo vinategemewa kuongezeka kufikia milioni 22 ifikapo 2030.

 

Hali ilivyo nchini

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Oktoba, 2017 zinaonesha kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hugundulika wakiwa na magonjwa ya saratani.

Waziri Ummy Mwalimu anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokadiriwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, inayokadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.

Taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kipindi cha mwaka 2006 hadi 2015 zinaonesha saratani inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ni ya mlango wa kizazi yenye asilimia 34 ikifuatiwa na ya ngozi (kaporsis Sarcoma) asilimia 13.

Saratani nyingine na asilimia zake kwenye mabano ni matiti (12), mfumo wa njia ya chakula (10), kichwa na shingo (7).

Saratani ya matezi (6), damu (4), kibofu cha mkojo (3), ngozi (3), macho (2) tezi dume (2).

Hata hivyo asilimia 80 ya wagonjwa hufika Ocean Road wakiwa katika hatua za mwisho za  ugonjwa na kufanya matokeo ya matibabu kutokuwa mazuri.

 

Tezi dume kuhusishwa na tendo la ndoa

Dk. Mseti anasema zipo tafiti ndogondogo ambazo zimewahi kufanyika duniani ambalo zinathibitisha ukweli uliopo juu ya suala hilo.

“Ingawa hakuna utafiti mkubwa uliofanyika kuthibitisha mtu anapofanya ngono mara ngapi kwa wiki hawezi kupata saratani hiyo.

“Lakini zipo tafiti ndogo ndogo ambazo zinaeleza mwanamume ambaye ni ‘sexually active’ (hufanya ngono mara kwa mara) ana uwezekano mdogo wa kupata saratani ya tezidume kuliko mwingine.

“Hata hivyo, hii haimaanishi mtu awe mzinzi, kwa sababu akiwa na wapenzi wengi atapata magonjwa hasa ya zinaa ikiwamo Ukimwi na kuyaweka maisha yake hatarini zaidi.

“Inashauriwa angalau mwanaume ashiriki mara tatu kwa wiki ingawa wapo wengine wanaojiweza zaidi ya hapo,” anasema.

 

Dalili

Anasema zipo dalili nyingi zinazojitokeza katika hatua ya awali ambazo hazimsababishii usumbufu wa aina yoyote mhusika, ndiyo maana wengi hufika hospitalini wakiwa wamechelewa.

Anataja dalili hizo kuwa ni kutoa mkojo ambao hauna nguvu, mkojo unaokatika-katika licha ya kwamba kuna baadhi ya wanaume ambao tangu wamezaliwa hupata mkojo wa aina hiyo.

Dk. Mseti ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba na Mifumo ya Kulipia (bima za afya) ORCI, anataja dalili nyingine kuwa ni kushindwa kutoa mkojo pindi tu anapofika chooni.

“Yaani anahisi kabisa kutoa haja ndogo lakini akifika chooni mkojo hautoki, inabidi asubiri… aubembeleze na wengine hadi wajikamue ndipo utoke, si dalili nzuri.

“Kitendo cha mkojo kutoka huku ukiwa unawasha washa au kuchoma choma inaweza kuwa dalili ya awali ya saratani, ingawa inaweza pia kuwa dalili ya magonjwa mengine kama UTI na yale ya kuambukiza hivyo ni muhimu kuwahi hospitalini,” anasema.

Anataja nyingine kuwa ni mkojo kushindwa kutoka vema na kwamba wapo ambao hulazimika kujikamua na kujikuta wakipata maumivu ya tumbo na mkojo kutoka ukiambatana na maumivu makali.

“Inapofikia hapo maana yake ni kwamba tayari saratani ya tezidume imekua na sasa imeubinya (imekandamiza) ule mrija wa mkojo hivyo unashindwa kabisa kupita ipasavyo.

“Kwa kawaida mkojo huwa unatoka mweupe hasa mtu anapokuwa anakunywa maji ya kutosha, lakini unapotoka ukiwa na damu damu ni dalili ya hatari.

 

Visababishi

Anasema sababu kuu ni kuzaliwa jinsi ya kiume kwamba kila mwanaume ana uwezekano wa kupata saratani hii.

“Umri unapoongezeka hasa kuanzia miaka 50 na kuendelea muhusika anaweza kupata saratani hii, pia unywaji wa pombe kupita kiasi, unene uliopitiliza ni miongoni mwa visababishi,” anasema.

Anasema wengine hurithi iwapo katika familia au ukoo kuna ndugu wa damu aliyewahi kuugua.

 

Hukua taratibu

Anasema ugonjwa huu hukua taratibu mno na inapoonekana maana yake huwa imeanza muda mrefu.

“Wengi walikuwa wanaogopa baada ya kusikia kipimo ni kidole lakini wasiogope kwa kuwa hicho ni kipimo cha juu mno, awali tunafanya cha PSA (cha damu).

 

Uchunguzi

Anasema miongoni mwa vipimo wanavyotumia ni pamoja na ‘ultra sound’ ili kuona tezidume limekua kwa ukubwa gani.

Kipimo kingine ni kidole ambacho hupapasa tezidume kwa ndani.

Anasema kipimo cha damu (Full Blood Picture) hutumika kuchunguza viungo vingine vya mwili ikiwamo ini, figo na vingine iwapo vinafanya kazi sawa sawa.

Kingine ni PSA (Prostate Specific Antigen), ambacho ni cha mwisho.

Anafafanua kwamba PSA ni kemikali maalumu inayotengenezwa na tezidume, ambapo kipimo cha damu hutumika kupima kiwango cha kemikali hiyo mwilini.

“Kwa kawaida, mwanaume aliyekamilika kiwango cha kemikali yake huwa ni kati ya sifuri hadi nne hiki ni kiwango cha kawaida na huashiria hana tatizo.

“Lakini inapokuwa zaidi ya nne hadi 20 humaanisha kemikali hiyo imetengenezwa kwa wingi na matokeo hayo yanatoa tafsiri kwamba kuna hali isiyo ya kawaida kwenye tezidume.

Anasema mara zote ukuaji wa tezidume usio wa saratani (Benign Proestate Hypertrophy – BPH) dalili zake huwa zinafanana na ukuaji wa tezidume ulio saratani.

“PSA test zipo aina mbili, kuna qualitative PSA test, hii hutuonesha iwapo kile kiwango kimezidi au la na kuna quantitative PSA test  ambacho hutuonesha idadi – zipo ngapi.

“Kuna watu huwa wanafika hadi 1000 wakati ‘normal range’ (kiwango cha kawaida) haitakiwi kuzidi nne, hapo mgonjwa atalazimika kumuona daktari bingwa wa upasuaji wa mkojo ambaye atamfanyia kipimo maalumu cha ‘cystescopy’.

 

Kipimo cha cystescopy

 

Anasema daktari huingiza mpira wenye kamera kwenye njia ya mkojo hadi sehemu ya ndani akiangalia ile njia jinsi ilivyo na kwenda hadi kwenye kibofu kwani dalili zinaweza kuashiria kuna shida kwenye kibofu au tezidume.

Anasema iwapo atabainika kuwa na uvimbe kwenye tezidume, hufanyiwa kipimo kingine cha ‘biopsy’ ambacho daktari huchukua sampuli (kinyama) kutoka kwenye ile tezidume na kuifanyia uchunguzi maabara.

 

Matibabu

Anasema mgonjwa hufanyiwa upasuaji kwa njia ya mikono au kwa teknolojia, lakini huwa kuna ‘risk’ ikiwamo kupoteza nguvu za kiume ikiwa baadhi ya mishipa itakatwa.

“Hapo tunatibu kwa njia ya vichocheo, ili tezidume ikue huwa inasimamiwa na homoni ya kiume iitwayo testosterone inayotengenezwa kwenye korodani kwa amri ya homoni nyingine inayotengenezwa kichwani kwenye ‘Pituitary gland’.

“Tunafanya upasuaji na kukata mawasiliano, kuzuia homoni inayotoka kichwani hatua hiyo itafanya tezidume inywee na ile PSA itashuka, tunaweza pia kufanya upasuaji mdogo wa kuziondoa kabisa zile korodani,” anasema.

Matibabu mengine ni sindano, vidonge ambavyo humeza kila siku ili kuzuia uzalishaji wa homoni hiyo.

Anasema tiba hiyo hufanya kazi

Ndani ya miaka miwili hadi mitatu baada ya hapo huwa haiwezi tena kuzuilika na tezidume huendelea kukua.

“Inapofikia hatua hiyo, huwa tunawabadilishia tiba na kuanza kuwapatia ile ya chemotherapy (tiba ya dripu ya saratani) kwa mizunguko sita kila baada ya wiki tatu, mgonjwa hupata madhara kadhaa.

“Huchoka mwili, hunyonyoka nywele lakini huwa ni kwa kipindi kile cha tiba, akimaliza basi nywele huota kama kawaida na kule kuchoka huisha,” anabainisha.

Anataja tiba nyingine kuwa ni ya mionzi ya variation yenye uwezo wa kuzia uzalishaji wa seli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles