24.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 15, 2024

Contact us: [email protected]

WAKWERE HUTUMIA MATUSI KUENZI MABABU NA MABIBI

Na Hamisa Maganga -aliyekuwa Chalinze


DESEMBA 30 nilialikwa kuhudhuria unyago wa mtoto wa wifi yangu. Shughuli hiyo ilifanyika Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambako ni chimbuko la kabila la Wakwere.

Nilipopata mwaliko nilifurahi mno, kwanza kwa sababu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria shughuli za aina hiyo, pili nilitamani kujua wanachofundishwa watoto hao, hasa ukizingatia kuwa mtoto aliyekuwa anachezwa ni wa kiume mwenye umri wa miaka sita.

Kabla ya hapo, mtoto huyo alikuwa amefanyiwa jando (kutahiriwa) nyumbani kwao Chanika, Dar es Salaam, na baada ya kupona alipelekwa Chalinze na kuwekwa porini kwa muda wa siku saba kufundishwa mambo mbalimbali.

Shughuli ilikuwa ni ya mkesha, na waalikwa tulitakiwa kufika eneo la tukio siku moja kabla.

Wakati nakaribia kufika eneo la tukio, nilishuhudia watoto watatu wakiwa porini katika kibanda kilichokuwa kimejengwa kwa nyasi, nikamuuliza mwenyeji wangu aliyenipokea barabarani kulikoni? Akasema hapo ndipo watoto wanapopatiwa mafunzo na makungwi.

Mbele kidogo nikashuhudia kina mama takribani sita wakiwa wamemzunguka binti ambaye kwa makadirio ya haraka haraka anaweza kuwa na umri kati ya miaka 15 au 16.

Sikusita kuuliza tena kinachoendelea katika eneo hilo, nikaambiwa kuna mwali wa kike ambaye naye kesho yake atatoka nje pamoja na wale watoto niliowaona kwenye kibanda cha nyasi.

Nilipofika eneo la tukio, shughuli mbalimbali zilikuwa zikiendelea huku akina mama na akina baba wakiimba nyimbo.

Baada ya muda nikaona akina mama wale waliokuwa na mwali wa kike porini wakirudi, wakiambatana na mwali wao aliyekuwa amebebwa matiti yakiwa nje, huku wakiimba nyimbo zilizoambatana na matusi ya nguoni.

Hali hiyo ilinishangaza mno, nikajiuliza kwanini wanaimba nyimbo za aina hii bila aibu huku watoto wakiwasikia?

Sijakaa sawa, akina baba nao wakaingia wakitokea porini huku nao wakiimba nyimbo za matusi, nikajikuta nalazimika kuwatafuta wazee na kuwahoji ni kwanini wanafanya hivyo mbele ya watoto.

 

Mkunga wa ngoma

Caroline Selemani (75), ni mkunga wa ngoma, ambaye pia ni miongoni mwa wabibi waliokuwa wakimfunda mwali wa kike.

Akizungumzia sababu ya kumtembeza binti hadharani akiwa matiti wazi anasema:

“Huu ndio utamaduni wetu, tumeuenzi kutoka vizazi na vizazi, hivyo hatuwezi kuuacha.

“Mtoto anapovunja ungo (balehe) ni sharti achezwe ngoma, hii ndio asili yetu.”

Anasema binti akiwa ndani hufundishwa mambo mbalimbali, ikiwamo suala la usafi na kutoogopa wanaume.

“Tunamwambia mambo ya kawaida, kwamba ameshakua hivyo asimwogope mume. Akitoka hapo ni ruhusa kuwa na mwanamume na hata akipata ujauzito kabla ya ndoa huwa haina shida atapokewa nyumbani bila ya matatizo yoyote,” anasema mkunga huyo.

Anasema kuwa kabla ya kuchezwa, binti huwa haruhusiwi kusimama na wanaume na endapo ikitokea amefanya hivyo na akapata ujauzito, basi hufukuzwa nyumbani.

Hata hivyo, anasema kabla ya kuchezwa, watoto wa kabila la Wakwere huogopa kuwa na uhusiano na wanaume, hujitahidi kujitunza hadi pale wanapowekwa ndani.

Caroline anasema iwapo binti akipata mume baada ya kuchezwa, siku ya ndoa yake kinachofanyika ni kuozeshwa tu kwa kuwa mambo yote anakuwa ameshafundishwa, ikiwamo jinsi ya kumtunza na kumuhudumia mume.

 

Nyimbo za matusi

Kuhusu matusi wakati wa sherehe za unyago, anasema ni jambo la kawaida katika mila yao hivyo, mtoto akichezwa ni lazima watukane.

Anasema ni lazima wanaume watukane na wanawake watukane, yaani wanajibizana kwa matusi bila kujali waliopo katika eneo la tukio ni kina nani.

Naye kungwi wa kiume, Komba Carlos, anasema kutukana ni mila waliyoirithi kutoka kwa wazee wao, hivyo wanapotaka kucheza watoto ni lazima wafanye tambiko la kimila ambalo linapofanyika ni lazima kutukana.

Anasema wasipotukana madhara yake huwa ni makubwa na mtoto anaweza kudhoofika pindi anaponema.

“Usipotukana mtoto akitoka kunema jioni ni lazima atalegea kama mtu anayeumwa, hatoweza kufanya chochote na hata akienda hospitali ugonjwa hauonekani,” anasema Carlos.

 

Muda wa kuwekwa ndani

Kuhusu muda wa binti kukaa ndani kabla ya kuchezwa, Caroline anasema siku hizi hawakai siku nyingi kwa sababu ya kusoma.

“Zamani ilikuwa ukivunja ungo unakaa ndani miaka yote hadi utakapochezwa, lakini siku hizi haiwezekani kwa kuwa mabinti wengi hufaulu na kuendelea na elimu ya sekondari.

“Hivyo, huwa tunawaweka kuanzia siku tatu hadi tano ili wasiache kwenda shule kwa muda mrefu,” anasema.

 

Kuzungushwa kifua wazi

Caroline anasema kuwa binti kukaa kifua wazi ni jambo la kawaida siku ya kuchezwa kwani huonyesha jinsi alivyo kigoli.

“Kuonyesha matiti ni kawaida, haijalishi nje kuna nani, hata kama kuna baba yake, kaka, wajomba na wengine, ni ruhusa kuona… ndio mila yetu,” anasema Caroline.

 

Unyago kwa watoto wa kiume

Akizungumzia kitendo cha watoto wa kiume wenye umri kati ya miaka sita na kuendelea kuchezwa, Carlos anasema kitendo hicho kinawajengea uelewa na kuheshimu wazazi.

Anasema mtoto wa Kikwere anapofanyiwa jando, ni lazima akakae porini siku saba ili kujifunza mambo mbalimbali, ikiwamo kuheshimu wazazi na kutoka siku ya nane.

“Mtoto akienda porini akirudi ni lazima awe na adabu, asipoelewa kile anachofundishwa adhabu yake huwa ni viboko hadi anakuwa sawa.

“Mtoto akitoka porini na bado akawa na tabia mbaya, mzazi anapeleka mashtaka kwa kungwi, baadaye ikitokea mtoto mwingine anatakiwa kuchezwa hujumuishwa nao na kuadhibiwa,” anasema.

Anasema pamoja na mambo mengine, watoto hao hufundishwa jinsi ya kumridhisha mwanamke wakati wa tendo la ndoa.

“Mtoto akiwa mkubwa ni lazima aoe, sasa kuoa kuna mambo mengi, hivyo ni lazima tumuandae mtoto mapema kuhusu namna ya kuishi na mwanamke na kumridhisha,” anasema Carlos……

Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTAMZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles