25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA MZAZI KATIKA MAISHA YA MTOTO

NA DK. CHRIS MAUKI,

NAJUA kuna nadharia mbalimbali kuhusu malezi na namna ya kuwakuza watoto wetu. Wako wanaoamini kwamba mzazi anatakiwa kuhakikisha kesho ya watoto wake imekaa sawa ili watoto hao wasijekuhangaika mbeleni na hiyo ndiyo kazi ya mzazi bora kwa mtazamo wao.

Wapo wanaoamini kwamba mzazi anatakiwa awepo muda wote kuhakikisha mtoto ana makuzi bora na si kupoteza muda kwenye mali na vinginevyo wakati mtoto akiharibika.

Pamoja na nadharia hizi tofauti tofauti, leo ninakujia na mambo muhimu yatakayobadili mtazamo wako juu ya malezi.

Kiu yangu ni kwamba, kila mzazi mwenye mtoto achukue nafasi yake kwa uaminifu mkubwa kuhakikisha mtoto au watoto waliochini yake hawajutii chochote katika maisha yao ya kesho.

Ni muhimu sana kufahamu kwamba, ushawishi wa baba kwenye malezi unakwenda hadi kizazi cha nne baada yake, hapa utaona ulivyo umuhimu wa uwepo wa baba kwenye maisha ya mtoto.

Nitakupa mifano ya watu mashuhuri ambao watu wengi wanawafahamu au wanafahamu mikasa yao.

Wazazi wa mwimbaji maarufu duniani, Whitney Houston, Emily (Cissy) na John Houston, walitengana wakati mtoto wao Whitney akiwa shule ya watoto wadogo “kindergarten”.  Whitney akiwa na mpenzi wake, Boby Brown, walikuwa wakivuta dawa za kulevya mbele ya mtoto wao mdogo, Bobbi Kristina, akiwa na umri wa miaka mitano.

Katika umri wa miaka 22, Bobbi amefariki kwa mkasa wa dawa za kulevya, mama yake Whitney amefariki akiwa na umri wa miaka 48 kwa kisa hicho hicho cha dawa za kulevya tena katika mazingira ya kufanana.

Wako watu mashuhuri wengi, wako watu wa kawaida wengi sana na wako hata usiowajua wengi waliopotea kabisa kimaisha kwa sababu ya kukosa uwepo wa malezi ya baba maishani mwao.

Kama tunavyoamini kwamba ni ngumu kushughulikia mambo yanayowahusu wazee wetu waliopita, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba tunaweza kushughulikia na kujibidisha kwa ajili ya maisha ya watoto na wajukuu zetu wajao mbele yetu.

Hakuna muda mwingine kuacha huu tulionao sasa. Mara nyingine kati ya vitu vinavyomzuia mwanamume kuwa baba bora ni ile hali ya kutokuumaliza uvulana ulio ndani yake.

Ili kuwa kwenye kumbukumbu za watoto wako kesho basi hauna budi kuwepo katika maisha yao leo. Ile hali tu ya kuwa na watoto, eti na wewe unaitwa una watoto au mtoto haikufanyi kuwa baba bora, lakini ukiwatunza au kumtunza yule uliyenaye basi unapata sifa ya kuwa baba bora.

Wapo wengi wetu ambao tumezaliwa, kukuzwa na kulelewa katika mazingira yasiyo mazuri kabisa kifamilia, lakini hii haitufanyi na sisi tuziharibu familia zetu au tuharibu malezi ya wale wanaokua na kulelewa chini ya mikono yetu.

Kwa mfano yako mambo rahisi kabisa ambayo wengi tunayapuuzia, lakini yana madhara sana kwenye malezi ya watoto, hakuna haja ya ninyi wazazi kufokeana na kurushiana maneno au ngumi mbele ya watoto wenu.

Kwanza nini kinatokea hadi mnyanyuliane mikono? Tunaweza kabisa kuwazuia watoto wetu kuumia hisia zao hususani sisi wazazi tunapokuwa na tofauti zetu.

Kama ulikuwa haujui basi fahamu leo kwamba jinsi ulivyo leo ni zao la utoto wako, jinsi ulivyo leo au namna unavyojiona haitofautiani sana na vile walivyokuwa wanakuona waliokuzunguka ukiwa mtoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles