Na Norah Damian, Dar es Salaam
Umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka miaka 37 mwaka 1978 na kufikia miaka 65 mwaka 2018.
Akizungumza leo Jumatano Februari 28, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Makadirio ya Idadi ya Watu kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2035, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa, amesema hayo ni mafanikio makubwa.
“Vifo vya watoto wachanga vinaendelea kupungua kwa kasi kubwa, mwaka 2016 kulikuwa na vifo 43 kwa kila watoto hai 1,000 lakini mwaka huu vimepungua hadi 33 na tunatarajia mwaka 2030 kutakuwa na vifo 17,” amesema Dk. Chuwa.
Ripoti hiyo pia inaonyesha idadi ya watu kwa mwaka huu imefikia milioni 54.2 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2021 itafikia milioni 59.4.
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema wingi au uchache wa watu si tatizo bali tatizo ni pale kasi ya ongezeko hilo inapozidi kasi ya uchumi na kusababisha taifa kushindwa kumudu mahitaji ya watu.