OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI
IKIWA zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, Bunge na magavana wa mikoa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Desemba 23, mwaka huu Serikali ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo sasa inatumia kadi ya turufu ya uzalendo katika kampeni za uchaguzi huo.
Mzizi wa mabishano katika kampeni ni vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya hapo Desemba 2016 na Mei 2017 dhidi ya wakuu 16 wa serikali ya nchi hiyo. Mmoja kati ya wakuu hao waliowekewa vikwazo ni mgombea wa urais kwa tiketi ya kambi ya serikali, Emmanuel Ramazani Shadary.
Kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa ni kwamba Shadary, alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamo wa Waziri Mkuu alikuwa rasmi ni mwenye dhamana ya polisi na usalama wa taifa pamoja na kazi ya kuowanisha shughuli za magavana wa mikoa. Kwa hivyo yeye alibeba dhamana ya kukamatwa wapinzani, matumizi ya nguvu za kupita kiasi na kuzidisha vipambe moto vita vya kienyeji katika mikoa ya Kasai.
Umoja wa Ulaya uliwawekea vikwazo watu hao 16 ikiwa ni pamoja na kuwapiga marufuku wasiingie katika nchi za Umoja huo. Vikwazo hivyo vitachunguzwa upya baada ya kumalizika uchaguzi, ama virefushwe au viondoshwe.
Serikali ya Kinshasa imekasirishwa na hatua hiyo na Waziri wa Mambo ya Kigeni, She Okitunda, aliwaambia mabalozi wa nchi za Ulaya kwamba vikwazo hivyo vinakwenda kinyume na sheria, havina heshima na ni kuingilia katika kampeni za uchaguzi wa Kongo. Alisema pindi vikwazo hivyo havitaondoshwa kabla ya uchaguzi, basi serikali yake itachukuwa hatua za kulipiza ili kulinda heshima ya utawala wake.
Kinshasa haijataja ni hatua gani hizo, lakini hayo ni maneno ya kawaida yanayotolewa na serikali hiyo dhidi ya nchi za Magharibi. Umoja wa Ulaya na Kituo cha Carter cha Marekani, kinyume na ilivyokuwa hapo kabla, mara hii hawakualikwa kuwa waangalizi wa uchaguzi.
Marekani nayo imeungana na vikwazo hivyo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya. Pia Denis Mukwege, daktari wa magonjwa ya kinamama huko Kongo na pia mshindi wa mwaka huu wa zawadi ya amani ya Nobel, alisema kwamba kudai kuviondosha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya wakuu wa Kongo ina maana ya kwamba uhalifu uliofanywa upite bila ya kupewa adhabu.
Ilitajwa kwamba hakuna sababu ya kimsingi ya kudai kuondoshwa vikwazo hivyo. Wapinzani muhimu wamezuiliwa kuwania uchaguzi. Pia kunakumbushwa mkasa wa kuuliwa mabingwa wawili wa Umoja wa Mataifa, Zaida Catalan, wa kutokea Sweden na Michael Sharp, wa kutokea Marekani, hapo Machi 2017 katika eneo la Kasai. Inadaiwa naduru za habari katika Umoja wa Ulaya kwamba kuna uwezekano Shadary huendaalihusika kwa namna moja au nyingine na mauaji hayo.
Kutokana na duru za habari za Serikali ya Kongo ni kwamba wafanyakazi hao wa Umoja wa Mataifa walitekwa nyara na waasi na baadaye wakauliwa. Lakini punde baadaye Radio ya Ufaransa, RFI, ilisema kwamba Serikali ya Kongo ililenga kuwanasa Catalan na Sharp: na kwamba mkalimani wao aliyeandaa safari yao hadi kwenye eneo walikotekwa alikuwa mtu aliyekuwa anaitumikia Idara ya Usalama ya Kongo.
Kashfa hiyo tayari imetajwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Kongo ambayo inashughulikia kuuliwa wafanyakazi wanne waliokuwa pamoja na mabingwa hao wawili wa Umoja wa Mataifa. Novemba 22, mkalimani huyo anayeshukiwa alikiri kwamba yeye anamshukuru Shadary kwa kumpatia kazi ya ukalimani. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Sweden, Margot Wallström, ametangaza kwamba nchi yake inazingatia uwezekano wa kutumia njia za kisheria kutaka utolewe waranti wa kimataifa ili Shadary akamatwe.
Kwa upande mwingine, kila siku ya uchaguzi ikikaribia kunaripotiwa visa vipya vya kushangaza katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati. Usiku wa kuamkia alhamisi iliyopita Bohari Kuu la Tume ya Uchaguzi ya Kongo (CENI) liliungua moto. Ndani ya bohari hilo kulikuwamo asilimia 70 ya masanduku, makaratasi na mashine za kupigia kura kwa ajili ya Mji Mkuu wa Kinshasa ulio na wakaazi milioni 12. Pia magari mengi yaliyoegezwa karibu na jengo la ghorofa moja la CENI yaliteketea.
Tume ya Uchaguzi ilisema kisa hicho kitachuguzwa na ikahakikisha kwamba zoezi la uchaguzi litasonga mbele kama ilivyopangwa. Makamo wa Waziri Mkuu, Henri Mova, baada ya kutembelea mahala palipotokea mkasa huo, alisema: Hakika Uchaguzi wa Desemba 23 utafanywa. Angalau hilo tunaweza kuwahakikishia wananchi, tutapigania ufanyike.
Hatahivyo, wapinzani wengi wanaamini kuna mizengwe nyuma ya moto huo. Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa Kibelgiji ni kwamba bohari hilo lilikuwa linalindwa na wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa rais. Dakika chache tu kabla ya jengo hilo kuanza kuwaka moto, saa nane za usiku, wanajeshi hao waliondoshwa.
Pierre Lumbi, mkuu wa timu ya kampeni ya mgombea wa upinzani, Martin Fayulu, ameilaumu kambi ya serikali kusababisha moto huo. Nao Muungano wa kambi ya Serikali, FCC, wa Emmanuel Ramazani Shadary unadai kwamba Fayulu ndiye aliyechochea kitendo hicho cha kihalifu. Yeye ndiye aliyetoa mwito kwa wafuasi wake kuharibu vifaa vya uchaguzi. Upinzani unadai kwamba serikali inataka kuusingizia kuhusu moto huo kama sababu ya kutaka kuufuta uchaguzi.
Desemba 23 ni siku ya kihistoria. Kutoka siku hiyo Joseph Kabila hatakuwa tena rais baada ya kukaa madarakani kwa miaka 17. Tangu mwanzo wa mwezi huu wagombea wa urais wamekuwa wakisafiri kwa ndege huku na kule ndani ya nchi hiyo kubwa ili kuomba kura. Katika miji mingi, wagombea wa upinzani wanaongoza kwa kuungwa mkono. Mji wa Bukavu wenye wakaazi milioni moja umejaa mabango yenye picha za wagombea.
Ubishi uko katika suala la matumizi ya mashine za elektroniki wakati wa kupiga kura. Upinzani unasema uchakachuaji ni rahisi kufanyika ikiwa mashine hizo zitatumika, haziaminiki. Unataka badala yake watu watumie karatasi za kura. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ni kwamba sasa karibu mashine 8000 kati ya 10368 zilizotengwa kwa ajili ya Kinshasa zimeteketea kwa moto. Mji mkuu huo wa Kongo ni ngome ya upinzani.
Leila Zerrougui, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani katika Kongo (Monuscu), alisema atawatuma wanajeshi wa kuweka amani kuwalinda wagombea wa upinzani. Alisema kumekuwapo visa vingi vya kuwazuia wagombea kuhutubia mikutano ya hadhara ya kampeni. Aliitaja miji ya Kindu, Lubumbashi na Kalemie, yote hiyo ni ngome za Muungano wa Serikali. Inasemekana watu wawili waliuwawa Jumanne iliyopita huko Lubumbashi wakati wa mkutano wa kampeni. Huko Kindu, Mji Mkuu wa Mkoa wa Maniema anakotokea Shadary, ndege ya Fayulu ilishindwa kutua wiki iliyopita. Jeshi liliweka mashine za kubebea mizigo na helikopta kwenye njia ya kutua ndege.
Umoja wa Mataifa umeisihi Serikali ya Kongo isitishe utumiaji nguvu na hotuba kali za uchochezi kabla ya uchaguzi. Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu, Michelle Bachelet alisema katika taarifa yake wiki iliyopita: Ninaingiwa na wasiwasi juu ya ripoti zinazohusu matumizi ya nguvu kubwa, ikiwa ni pamoja na majeshi ya usalama kufyatua risasi katika mikutano ya vyama vya upinzani. Naitaka Serikali itoe ishara wazi kwamba vitisho na utumiaji nguvu dhidi ya Upinzani wa kisiasa havitastahamiliwa.
Tutumai kwamba onyo hilo litasikilizwa.