26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Umoja wa Mataifa wamsifu Machar kurudi nyumbani

Riek MacharNEW YORK, MAREKANI

UMOJA wa Mataifa (UN) umesifu hatua ya kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar kurudi nchini humo kuunda serikali ya mpito, ikiwa ni sehemu ya mpango uliolenga kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili.

“Kurejea nyumbani kwa Makamu wa Rais kunapaswa kuwa mwanzo mpya kwa nchi hiyo na kuelekea mpango wa kubadilisha utawala,” Mkuu wa Jopo la Usalama la UN, Herve Ladsous aliliambia Baraza la Usalama la Umoja huo jana.

Baraza hilo lenye nchi 15 wanachama lilikutana kujadili vita nchini humo, huku Machar akiapishwa kurejea katika nafasi yake ya umakamu wa rais katika serikali mpya inayoongozwa na Rais Salva Kiir.

Mafanikio hayo yametokana na juhudi za kimataifa ‘kuwalazimisha’ waasi na serikali kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kudumisha amani, ambayo yalitiwa saini Agosti, 2015.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Machar ataongoza pamoja na Kiir katika serikali ya mpito ambayo itaandaa Uchaguzi Mkuu.

“Ni muhimu pande zinazohusika kutumia nafasi hii kuonyesha walivyojitolea kutekeleza makubaliano ya amani kwa manufaa ya nchi na wananchi wao,” alisema Ladsous.

Balozi Msaidizi wa Sudan Kusini katika UN, Joseph Mourn Malok alisema Serikali mpya inatarajiwa kuundwa baada ya majadiliano ya wadau nchini humo na itachukua siku moja au mbili ili kuyakamilisha.

Machar alirudi nchini humo Jumanne jioni na kuapishwa kuwa makamu wa rais wa taifa hilo jipya zaidi duniani na kutoa wito wa amani baada ya vita vya zaidi ya miaka miwili.

“Tunahitaji kuwaleta watu wetu pamoja ili waungane,” alisema Machar ambaye alilakiwa na mawaziri pamoja na mabalozi aliposhuka katika ndege ya UN.

Awali, kiongozi huyo alitarajiwa kuwasili Aprili 18, lakini akachelewa na kuzua hofu kuhusu hatima ya makubaliano ya amani.

Baada ya kutua katika uwanja wa ndege alienda moja kwa moja hadi Ikulu ambako aliapishwa na hasimu wake, Rais Salva Kiir.

“Nimejitolea kutekeleza makubaliano haya ili hatua ya maridhiano ya kitaifa ianze haraka iwezekanavyo, watu wawe na imani kwa nchi ambayo waliipigania kwa muda mrefu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles