Na Amina Omari, Tanga
SERIKALI imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuhakikisha inapambana na maradhi mbalimbali nchini.
Imekuwa ikitekeleza mpango wa Maendeleo ya afya ya msingi kwa kipindi cha miaka 10 kutoka 2007 hadi 2017 ukiwa na lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma bora za afya.
Mpango huu unalenga hasa katika kuhimiza upatikanaji wa huduma ya afya ya msingi kwa wote, kuwezesha na kushirikisha jamii katika utoaji wa huduma za afya.
Akizungumza na MTANZANIA, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema utekelezaji wa mpango huo umesaidia kuleta mabadiliko makubwa ya utoaji huduma za afya kutoka katika zahanati, vituo vya afya hadi hospitali za wilaya.
Waziri Ummy anasema kabla ya kuja kwa mpango wa MMAM, Tanzania ilikuwa na jumla ya zahanati 4679, vituo vya afya 481 pamoja na hospitali 219 pekee.
“Mafanikio ya MMAM yamewezesha serikali kujenga vituo vya kutolea huduma takribani 7,000 vikiwa katika ngazi mbalimbali kwenye maeneo tofauti nchini, ikiwa ni pamoja na maboresho ya huduma za afya hususani kwa mama na mtoto,” anasema.
Anasema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusogeza karibu huduma za afya katika maeneo ya vijijini na
pembezoni ambapo wananchi wameweza kupata huduma kwa urahisi.
Anasema kupitia mpango huo, Serikali ilikuwa imejizatiti kuhakikisha zahanati na vituo vyake vya afya ambavyo ndizo nguzo kuu za huduma hiyo, vinahudumia vema wananchi.
“Awali kulikuwa kuna uwazi katika huduma za afya, hasa kwa maeneo ya pembezoni ambapo wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma lakini utekelezaji wa MMAM umeweza kumaliza tatizo hilo,” anasema.
Anaongeza wamefanikiwa kuongeza watoa huduma wanaodahiliwa kutoka katika vyuo vya serikali kutoka madaktari 400 hadi kufikia 1,000 katika ngazi mbalimbali wakiwamo wauguzi, waganga wakuu na wasaidizi.
Anasema pia wamefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto. Hii ni kwa sababu ya kuwapo kwa huduma ya dharura katika vituo vya afya.
“Tulilenga kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 578 hadi kufikia 175 katika kila kizazi hai 100,000 na watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka vifo 112 hadi kufikia 41,”anabainisha.
“Katika eneo hilo la uzazi salama ndipo tulidhamiria kuhakikisha kwanza kila mjamzito anahamasishwa kuhudhuria kliniki wakati wote wa ujauzito ili kuweza kupata ushauri wa kitaalamu,” anasema Ummy.
Licha ya kwamba mpango huo umefikia ukingoni kutokana na mafanikio yalipatikana, Waziri Ummy anasema kwa sasa wapo kwenye mapitio ya mpango huo kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI.
Anasema Serikali inampango wa kujenga vyumba 150 vya upasuaji katika hospitali mbalimbali nchini kwa kipindi cha mwaka 2017/18.
Anasema mpango huo unatarajiwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, ambapo pamoja na mambo mengine pia watahakikisha kila kituo cha afya na zahanati zinakuwa na dawa za uzazi salama.
Anaongeza kuwa moja ya vipaumbele vya serikali ni kuhakikisha wananchi wa hali ya chini wanaboreshewa huduma ikiwemo za afya na kila mjamzito anapata fursa ya kupata mtoto kama ilivyo matarajio yake.
“Naamini tukiboresha afya ya msingi katika vituo vyetu, tutaweza kumaliza changamoto ya vifo vya wajawazito na
watoto chini ya umri wa miaka mitano,” anasisitiza Waziri Ummy.
Anasema licha ya jitihada za maboresho ya huduma za afya, takwimu zinaonesha asilimia 61 ya wajawazito wanajifungulia hospitali wakati asilimia 40 wanajifungulia majumbani.
“Tunajua kuna wataalamu ambao si rasmi wanaofanya kazi za ukunga nje ya mifumo na hiyo inatokana na upungufu uliopo katika sekta hiyo, lakini nia yetu ni kuendelea kuhamasisha wananchi waone umuhimu wa kutumia hospitali zetu,” anasema.