Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, amesema kuwa hajaridhishwa na usimamizi wa miradi ya afya katika Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma hivyo waliohusika kutafuna fedha katika miradi hiyo kurejeshwa na kujibu tuhuma hizo.
Kauli hiyo ameitoa Mei 4,2021 Wilayani Chemba mkoani Dodoma mara baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Wilayani humo ambapo ametembelea Shule ya Sekondari Chemba, Hospitali ya Wilaya ya Chemba na Kituo cha Afya cha Hamai.
Waziri Ummy amesema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chemba haukusimamiwa vizuri na ndio maana baadhi ya majengo bado hayajakamilika kwa asilimia 100 huku akihoji Halmashauri hiyo kwanini hawakutumka fedha shilingi milioni 250 mpaka zikarudi hazina wakati ujenzi haujakamilika.
“Lazima tukubali ujenzi haukusimamiwa vizuri hakukuwa na usimamizi mzuri wanaohusika na manunuzi hawakusimamia vizuri ndio maana milioni 250 zikarudi lakini hapa hakuna hata wagonjwa kwa sababu huduma muhimu hakuna,mna wagonjwa 1000 tangu muanze kutoa huduma kuna shida hapa,”amesema Ummy
Ummy amesema wote waliohusika na wizi katika miradi hiyo atahakikisha anawawajibisha hata kama wamehama katika Halmashauri hiyo.
“Hii miradi imehujumiwa watu wametanguliza maslahi binafsi najua mmepiga sana hapa ninayomajina ya watu ambao wamechangia kuharibu miradi yetu afu wamehamishiwa sehemu nyingine sasa hata kama ulihamishwa mimi hili siliachi,tukithibitisha tutamchukulia hatua,”amesema.
Akiwa katika kituo cha afya cha Hamai,Waziri Ummy alipokelewa na wakazi wa Kijiji cha Hamai ambapo walidai huduma muhimu katika kituo hicho hazipatikani kama Xray,dawa,maji,gari la wagonjwa pamoja na kukosekana kwa wodi ya wanaume.
Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk. Binilith Mahenge amesema atahakikisha maji yanapatikana katika Hospitali ya Wilaya na katika kituo cha afya cha Hamai.