23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Baba amchoma kisu mtoto wa kambo kisha naye kujinyonga

Na Yohana Paul, Geita

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limethibitisha kutokea kwa tukio la mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina la Shija Mwanzalima (30) ambaye kwa sasa ni marehemu, mkazi wa mtaa wa Nyantorotoro, kata ya Nyankumbu wilayani Geita Mkoani hapa kumchoma kisu mwanaye wa kambo na kisha mwenyewe kujiua.

Akielezea tukio hilo juzi kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, (ACP) Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mwezi aprili ambapo binti aitwaye Rechel Erasto mwenye umri wa miaka mitatu na miezi mitano alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu na baba yake huyo wa kambo.

ACP Mwaibambe alisema baada ya kufanyiwa ukatili huo, mtoto huyo alipata jeraha kubwa tumboni na amelazwa hospitali ya mkoa wa Geita na hadi sasa hali yake inaendelea vizuri baada ya kushonwa na madaktari jeraha alilopata.

Kamanda wa Polisi aliongeza kuwa,  baada ya mwanaume huyo kumchoma kisu mtoto wake wa kambo, na yeye alichukua maamuzi ya kujichoma kisu tumboni na baadaye kuingia  chumbani kujinyonga na akafariki dunia.

“Mbinu aliyotumia huyu marehemu, alimtuma mke wake, kwamba aende dukani kumununulia mtoto dawa, kwa hiyo mke alipoenda dukani, huku nyuma yake ndio kukatekelezwa tukio hilo, mme akamjeruhi mtoto na yeye akajinyonga.

“Chanzo cha tukio hili ni msongo wa mawazo, huyu marehemu na huyu mwanamke wameoana hivi karibuni, huyo mtoto siyo wa kwake, baada ya kuoana walienda kupima afya hospitalini, na ikabainika mwanaume ana maradhi na mke yupo salama, na huyu mwanamme alikuwa anaishi kwa mwanamke,” alifafanua ACP Mwaibambe.

ACP Mwaimbambe ameitaka jamii kuacha kutenda vitendo vya ukatili wa aina hiyo kwani ni ishara kubwa ya mmomonyoko wa maadili na kama kuna mgogoro ama matatizo ndani ya familia ni vyema wahusika wakaitatua kwa njia ya mzungumzo zaidi badala ya kuelekeza visasi kwa watoto ambao hawana hatia.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji wa Geita, Carthbert Byabato alikiri uwepo wa ongezeko la  vitendo vya ukatili kwa siku za hivi karibuni na kuweka wazi changamoto hiyo inatokana  na ongezeko la msongo wa mawazo miongoni mwa watu hivyo aliishauri jamii kujitahidi kuishi kwa amani na utulivu kuepuka matukio hayo.

“Naishauri jamii yetu iweze kuwa na uvumilivu, kutofanya vitu kwa hasira, kwani kufanya maamuzi ukiwa na hasira inaweza sababisha ukafanya vitendo vinavyoweza kupelekea matatizo makubwa, hasa mtu kupata ulemavu kutokana na hivyo vitendo  vya ukatili na hata kusababisha kifo pale ukatili unapokithiri zaidi,”  alisema  Byabato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles