NA OSCAR ASSENGA – TANGA
NISHATI ya umeme imeelezwa kuwa ni kiungo muhimu katika kuchochea uwekezaji wa viwanda nchini na utasaidia kuinua kwa kasi uchumi wa Watanzania.
Hayo yalielezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, juzi katika Baraza Kuu la 47 la wafanyakazi wa shirika hilo mjini hapa, ambapo alisema kwa kutambua umuhimu huo wanatahakikisha malengo ya uchumi wa viwanda yanatimia.
Alisema watahakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika maeneo mbalimbali nchini bila vikwazo vya namna yoyote ili azma hiyo iweze kutimia kwa vitendo na hivyo kuchochea kasi ya uchumi.
“Kama mnavyojua Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kukuza uchumi wa viwanda, hivyo nishati ya umeme ni kiungo muhimu katika kuchochea uwekezaji wa viwanda ambao utasaidia harakati za maendeleo,” alisema.
“Hivyo napenda kuihakikishia Serikali kwamba tunatambua wajibu tulionao katika kutimiza malengo hayo kwa kuongeza uwajibikaji na ufanisi
kazini ambao ndio utakuwa dira ya kufikia mafanikio,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema tangu kuanzishwa kwake, baraza hilo limekuwa ni sehemu muhimu kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali kwa masilahi ya wafanyakazi ambao wamewaamini kuwawakilisha.
“Baraza hili limesaidia shirika kujua changamoto na kero zinazowakabili mahali pa kazi na kwa pamoja ufumbuzi wake na changamoto hizo zimepatiwa ufumbuzi kwa faida ya wafanyakazi na shirika kwa ujumla,” alisema.